loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali yaanza kutafsiri sheria kwa Kiswahili

SERIKALI imeanza mchakato wa kuzitafsiri sheria mbalimbali kutoka Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili ili kuwasaidia wananchi katika upatikanaji wa haki katika masuala mbalimbali.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geoffrey Pinda kwenye warsha ya siku tatu iliyoandaliwa na Shirika la Huduma za Msaada wa Kisheria (LSF).

Warsha hiyo ilihudhuriwa na wajumbe 45 kutoka nchi tisa za ukanda wa Afrika Mashariki kwa ajili ya kujadili namna bora ya kuboresha mifumo ya upatikanaji haki kupitia huduma za msaada wa kisheria katika ukanda huo.

“Lugha ni moja ya vikwazo kwa wananchi kutopata haki inavyotakiwa, hivyo kwa kuwa lugha ya Kiswahili haitumiki katika maeneo ya kutolea haki, serikali imeamua kuzitafsiri sheria katika Kiswahili ili kuwasaidia wananchi katika masuala ya kisheria na utoaji haki.”

“Kikwazo kingine katika upatikanaji wa haki ni mazingira yasiyo rafiki ikiwamo vita, rushwa, ubaguzi wa rangi na ukabila, hivyo maazimio mtakayoyafikia kwenye mkutano huu mtayawasilisha kwenye serikali zenu kwa ajili ya kufanyiwa kazi,” alisema Pinda.

Alisema kwa kuwa baadhi ya mashirika yanayotoa huduma za msaada wa kisheria yameacha wajibu wao wa msingi wa kuwasaidia wananchi na badala yake yameanza kukumbatia maslahi binafsi, mwaka 2017 serikali iliamua kuunda sheria ya wasaidizi wa kisheria ili waweze kufanya kazi kwa utaratibu uliowekwa kisheria katika kuwasaidia wananchi.

Pinda alisema mkutano huo ambao unawaleta pamoja wataalamu na wabobezi wa mifumo mbadala ya utoaji haki na mifumo ya utoaji haki katika jamii, watoa msaada wa kisheria na wajumbe wa kamati za Mahakama kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Somalia na Sudan Kusini, utasaidia katika kupata uzoefu mbalimbali miongoni mwa nchi washirika.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala alisema LSF inatoa msaada wa moja kwa moja wa kisheria kwa watu zaidi ya 70,000 kwa mwaka kutoka makundi yasiyo na uwezo wengi wao wakiwa wanawake, lakini kwa ujumla  hutoa elimu ya kisheria kwa watu milioni tano kwa mwaka.

Mkurugenzi wa Programu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Sheria (IDLO), Roland Friedrich alisema shirika lake limekuwa likihamasisha utawala wa sheria na maendeleo endelevu ili  kuondoa changamoto katika jamii na kukuza upatikanaji wa haki na kuwafanya wananchi hususani wanawake, watoto na makundi maalumu kudai haki zao kupitia mifumo rasmi na isiyo rasmi inayotoa haki.

BENKI ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imepongeza uthubutu ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi