loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wauza mafuta ya kupikia msipandishe bei kuumiza walaji

TANGU mwishoni mwaka jana 2020, kumekuwa na upungufu wa mafuta ya kupikia jambo lililosababisha baadhi ya bidhaa nyingine zinazotegemea  kutumia mafuta  kuwa na mabadiliko mbalimbali katika bei na hata upatikanaji wake kuwa wa gharama kubwa zaidi.

Inafahamika kuwa mafuta ya kupikia ni kiungo muhimu kwa mwili wa binadamu, ingawaje wataalam wa afya wanashauri pia kutumika kwa mpangilio maalum usioweza kuleta madhara kiafya.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey  Mwambe anasema nchi haina uhaba wa mafuta ya kupikia na kuwataka watakaopandisha bei ya bidhaa hiyo kufutiwa leseni.

Amewaonya  mawakala na wafanyabiashara wa jumla kuhakikisha kuwa bei ya bidhaa hiyo haitopandishwa, jambo litakalosababisha wananchi kuendelea kuhangaika kwa ajili ya upatikanaji wake.

Kauli ya Waziri huyo inatia moyo wananchi ambao kila kukichwa wamekuwa wakiulizana namna ya kupatikana kwa bidhaa  kwa gharama halisi  ambayo hata wajasiriamali wa bidhaa mbalimbali wamekuwa wakiyatumia kwa ajili ya kutengenezea bidhaa zao.

Kwa mfano mjasiriamali aliyekuwa akiuza andazi moja kwa shilingi 100 amejikuta akipandisha  na kuuza kwa sh 200, kadhalika aliyekuwa akikaanga samaki naye akiwa na gharama zake kulingana na alivyoweza kuipata bidhaa hiyo lakini pia kwa mamalishe chakula kuwa na tofauti.

Aidha, katika mitandao mbalimbali ya kijamii, hoja ya kukosekana kwa mafuta imekuwa ikijadiliwa kila kona ya nchi, huku wanawake mbalimbali wakiulizana kutaka kujua kama kuna unafuu wa bei kwa bidhaa hiyo kwa walioko  mikoa  mingine ili kuona uwezekano wa kuifikia na kuendelea na shughuli zao za mara kwa mara.

Kutokana na  hali  hiyo, ni muhimu mawakala wa bidhaa hiyo  kutambua kuwa serikali imeshakiri kuwa  hakuna uhaba wa mafuta  na tayari zimeingizwa tani 48,250 kati ya Desemba mwaka jana na januari mwaka huu ilhali mahitaji ya nchi ni tani 30,000 kwa mwezi.

Kwa  kipindi cha mwezi mmoja zimeingizwa meli mbili moja ikiwa na tani 21,800 na nyingine ikiwa na tani  26,450, lakini pia Februari  17 mwaka huu itakuja meli nyingine  na mafuta  hayo ni tofauti  nay ale yanayozalishwa nchini.

Pamoja na tani hizo kuingizwa nchini, lakini bado katika  kipindi hicho kwenye masoko mbalimbali bado walaji wamekuwa wakiipata bidhaa hiyo kwa gharama kubwa tofauti na hali ilivyokuwa awali, jambo ambalo wafanyabishara na mawakala wanahitajika kuliangalia kwa umakini.

Ikumbukwe kuwa mafuta hayo yalipanda kutokana na  bidhaa hiyo kupanda katika soko la dunia ambapo kulichangiwa na kushuka kwa uzalishwaji kutokana na kuibuka  kwa maambukizi ya virusi vya Corona, ambapo nchini mbalimbali zilifunga  utendaji na usafirishaji jambo lililopunguza  bidhaa hiyo inayoingizwa nchini.

Ni vyema kwa wakati huu, mawakala   kuonesha ushirikiano wa kusambaza bidhaa hiyo hatua itakayoondoa mwanya kwa wafanyabiashara kutumia fursa hiyo kuendelea kupandisha bei ya bidhaa hiyo huku wananchi wakiendelea kuipata kwa gharama iliyo kubwa.

Aidha ni vyema mamlaka zitakazobaini kuwepo kwa mawakala  watakaohusika kupandisha bei hiyo ya mafuta kuhakikisha inawafutia leseni  jambo ambalo litakuwa fundisho kwa wengine kuacha vitendo hivyo ambavyo  ni vya kuwalaghai wananchi.

Kadhalika wafanyabiashara nao wasitumie fursa hiyo kuficha bidhaa hiyo wakidhani kuwa ni eneo ambalo wataweza kujipatia fedha zaidi, badala yake washiriki bega kwa bega kuhakikisha  bidhaa hiyo inawafikia wananchi kwa gharama ambazo sio za kuwaumiza bali zile ambazo ni halisi.

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi