loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Miji 45 nchini kuwa ya kisasa

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amewahakikishia Watanzania kuwa Mradi wa Miji ya Kimkakati (TSCP) utakapokamilika miaka mitano ijayo, sura ya nchi itabadilisha kwa kuwa na miji ya kisasa.

Amesema kupitia mradi huo, maeneo takribani 45 yataguswa yakiwemo ya halmashauri kama vile Nzega, Mafinga, Handeni na nyinginezo.

Waziri Jafo aliyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula (CCM) aliyetaka kujua mradi huo mkubwa ulioanzishwa na serikali utakaogusa maeneo ya Mwanza na Mbeya, utaanza lini.

Akijibu swali hilo, Jafo alimpongeza mbunge huyo kwa kitendo chake cha kushirikiana na Tamiseni na kuibadilisha kwa kiasi kikubwa sura ya jiji la Mwanza na kuwa kama ilivyo sasa.

“Kama nilivyosema katika hotuba yangu ya bajeti katika mwaka wa fedha 2020/21 tutakuwa na ile miradi itakayogusa miji takribani 45 nchini ikiwemo halmashauri za Nzega, Mafinga, Kasulu na Handeni na kupitia mradi huu mkakati unaenda kubadilisha nchi yetu katika miaka mitano ijayo, miji yetu itakuwa ya ajabu,” alisisitiza.

Awali, katika swali lake la msingi, Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi (CCM), alitaka kujua ni lini serikali itaanza ujenzi wa barabara za lami na kufunga taa za barabarani katika Mji wa Mafinga chini ya Mpango wa Uendelezaji Miji Nchini.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Tamisemi, Festo Dugange alisema mradi wa TSCP umetekelezwa katika Halmashauri za Majiji ya Tanga, Dodoma, Mbeya, Arusha na Mwanza na Halmashauri za Manispaa za Mtwara Mikindani, Ilemela na Kigoma Ujiji kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 355.5 sawa na Sh bilioni 799.52.

Alisema Mradi wa Kuendeleza Miundombinu katika Miji 18 (ULGSP), umetekelezwa katika Halmashauri za Manispaa za Morogoro, Tabora, Moshi, Sumbawanga, Shinyanga, Songea, Iringa, Mpanda, Lindi, Singida, Musoma na Bukoba na Halmashauri za Miji ya Kibaha, Babati, Geita, Korogwe, Bariadi na Njombe.

Alieleza kuwa miradi hiyo ya TSCP na ULGSP ilimalizika muda wake Desemba mwaka jana.

“Serikali inaendelea na mazungumzo na Benki ya Dunia kwa ajili ya kuanza kutekeleza programu nyingine ya kuendeleza miundombinu itakayohusisha halmashaur 26 zilizokuwepo kwenye programu zilizomalizika pamoja na halmashauri nyingine 19 za miji ikiwemo Mafinga,” alieleza.

NAIBU Waziri wa Mawasiliano na ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi