SPIKA wa Bunge Job Ndugai amepiga marufuku wabunge kutumia nembo ya Bunge katika nyaraka zao binafsi kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa la jinai.
Amesema kwa mujibu wa sheria na kanuni za Bunge, nembo hiyo ya Bunge inatumiwa pekee katika nyaraka za spika au watendaji wa Bunge hilo hivyo yeyote asiyehusika katika kundi hilo akiitumia wakiwemo wabunge amefanya kosa la jinai.
Spika Ndugai aliyasema hayo bungeni Dodoma leo mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu bungeni.
Alisema tayari alishatoa katazo kwa wabunge la kutotumia nembo hiyo lakini kwa bahati mbaya baadhi yao wameendelea kuitumia katika nyaraka zao binafsi.