loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Warangi hujivunia asili yao, ni wapole na wakarimu

KATIKA mwendelezo wa makala za utamaduni, mila na desturi za makabila mbalimbali, leo tunaangazia jamii ya Warangi, mojawapo kati ya makabila yanayopatikana mkoni Dodoma.

Warangi wapo kati ya Babati na Kondoa lakini makazi yao hasa ni katika Wilaya za Chemba na Kondoa. 

Kondoa ni mojawapo ya maeneo yenye historia kubwa Tanzania na Afrika, na Mji wa Kondoa ni wa kihistoria katika ukanda huu. Ulianza kama kituo cha kupumzikia watumwa waliokuwa wakipelekwa pwani.

Njia moja ya watumwa ilipitia katika mji huu na kumbukumbu yake ni mtaa unaoitwa Ubembeni.

Asili ya kuitwa hivyo ni kutokana na kukaliwa na kabila la Wabemba toka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo pale biashara ya utumwa ilipopigwa marufuku. 

Na asili ya neno Kondoa linatokana na mto unaopita karibu na mji, ambao Warangi waliuita Mkoondo wa Iraangi. Pia mji wa Kondoa hujulikana kama ‘Ula’.

Hapa palikuwa na soko la zamani, na biashara iliyofanyika hapo ni ile ya kuuziana na kununuliana vitu. Mahali hapo kwa Kirangi paliitwa “Wula” ikiwa na maana “Nunua”.

Mitaa ya Mji wa Kondoa ina majina ya matukio au watu maarufu wa wakati ule; mfano ‘Ubembeni’ kama nilivyodokeza hapo juu. Mabaki ya kabila la Wabemba bado wapo hadi sasa.

Pia kuna mitaa kama ‘Iboni’, eneo kulipokuwa na mtu maarufu sana na mtawala wa eneo hilo. Mtu huyu aliheshimika kwa hekima na busara zake. Au ‘Kwapakacha’, jina la mtawala aliyeitwa Pakacha ambaye alikuwa kiongozi wa kimila wa eneo hilo.

Asili

Tumezoea kuwaita Warangi sanjari na lugha yao ya Kirangi lakini wao kimatamshi halisi ya lugha yao ni ‘Valangi’ na wanaongea ‘Kilaangi’. Warangi ni kati ya makabila yaliyotokea Mijikenda (nchini Kenya), walipoingilia wakati wanasafiri wakitokea nchini Ethiopia. 

Hadi leo, kwa mwonekano Warangi wanafanana sana na Wahabeshi, wana sura nyembamba, pua ndefu na nywele za kuchanganya asili ya Asia na Afrika.

Safari ya Warangi haikuwa rahisi sana, kwanza ukichukulia umbali waliotoka na pia mabadiliko ya hali ya hewa ukiwemo ukame, waliokumbana nao kwenye maeneo mbalimbali waliyopita.

Hali hiyo iliwasababisha wabuni mbinu mbalimbali za kutafuta maji wakati wa kiangazi, walipofanikiwa kupata maji katika eneo husika waliamini mahali hapo panafaa kuishi na walilowea.

Katika safari yao iliyowafikisha mahali walipo, walitangamana na makundi mbalimbali ya makabila mengine, yakiwemo yale ambayo kwa asili hayatulii sehemu moja.

Lakini wamefanikiwa kubaki kama walivyo japokuwa kuna athari ndogo ndogo za lugha yao kimatamshi.

Baadhi ya makabila wanayopaka nayo ni Wamasai, Wasandawe, Wairaqw, Waburunge, Wasi, Wagorowa na Wambugwe. Licha ya lugha yao kuathiriwa kwa mbali na makabila wanayotangamana nayo, lakini ndugu wa Warangi, si kwa lugha tu bali hata kwa asili, ni Wambugwe.

Nasaba

Warangi si wengi sana kwa idadi lakini pamoja na uchache wao kinachofanya watambulike kuwa wapo, ni ile hali ya kujivunia asili yao. Maana sifa yao kubwa ni kukuza na kupenda sana kuongea lugha yao.

Mrangi huzoeshwa kuongea lugha yao tangu akiwa mdogo na hivyo kumjengea mtoto hulka ya kujivunia asili yake.

Ukibahatika kufika kwenye maeneo ya kiini cha eneo la Irangi kule Kondoa, kwenye maeneo ya Bereko, Kikilo, Kisese, Masange, Mnenia, Chandama, Chemba, Goima, Mrijo, Kolo, Soera, Changaa, Thawi, Kingale, Suruke, Dalai na meneo mengine utashangazwa na baadhi ya mambo yao.

Hata sehemu wanazofanya biashara za mazao hutumia sana lugha yao ya Kirangi. Hawa ndio Warangi, jamii ya watu wanaopenda kujiweka karibu mno kwenye mambo yao na hujivunia sana asili yao, na si rahisi kugubikwa na jamii nyingine.

Namna yao ya kulinda hadhi yao ni kwa upole na si ubabe, kwani kati ya makabila yenye sifa ya upole na ukarimu wa kiwango cha juu, Warangi ni kabila mojawapo.

Kama nilivyosema awali, ndugu wa Warangi ni Wambugwe, hivyo Mrangi akiongea na Mbugwe wanasikilizana na kuelewana lakini Mrangi hapendelei kuongea Kimbugwe, hata kama anaelewa yanayotamkwa na Mbugwe yeye atajibu kwa Kirangi.

Warangi katika kujivunia mambo yao husema kuwa ukiisikiliza lugha ya Kimbugwe inapoongewa ni sawa na kumsikiliza  mtoto mdogo wa Kirangi anavyojifunza kuongea.

Warangi na Wambugwe ni watu wa asili moja, ilitokea kwamba Warangi walipofika Babati waligawanyika makundi mawili wakati wakielekea mahali walipo hivi sasa.

Mgawanyiko huo ndiyo ulizaa sehemu mojawapo ya Wambugwe, kutokana na kutelekezwa na wenzao mahali hapo baada ya kwenda kuwinda kanga.

Inabainishwa kwamba, vijana wa jamii ya Kirangi walikwenda kuwinda kanga kwenye maeneo ya pembezoni na walipofikia, yaani Babati. Walikawia kurudi na waliporudi hawakuwakuta wenzao, walioendelea na msafara wao na hivyo wao waliachwa.

Hawakujihangaisha kuwafuata bali waliamua kubakia mahali hapo, ndipo wakajulikana kwa jina la watu walioachwa kwa sababu ya kuwinda kanga. Kwa lugha ya Kirangi ndege aina ya kanga anayefanana na kuku, huitwa ‘mbuwe’.

Basi wale watu kutoka jamii za Kirangi walioachwa kwa sababu ya kunogewa kuwinda mbuwe, wakajulikana kama Wambugwe tangu wakati huo.

Ndiyo maana ukisikiliza lugha ya Kimbugwe na Kirangi zina muingiliano wa karibu. Laiti isingekuwa mambo ya kuwinda kanga pengine wangeendelea kuwa wamoja. 

Utamaduni na chakula

Chakula kikuu cha Warangi ni ugali wa mahindi au uwele, na mboga zinazotumika ni kama vile maziwa (masusu), mlenda (kirumbu) na nyama.

Warangi hujishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara; mazao ya chakula ni kama uwele, mtama, mahindi n.k. na mazao ya biashara ni kama vile karanga, alizeti, njugu mawe na kunde.

Vazi rasmi la kabila hili ni kaniki, lakini wengi wanavaa mavazi ya Kiarabu yakiwemo hijabu, kanzu na n.k.

Kuhusu ngoma, Warangi wana aina ya ngoma iliyowambwa ngozi ya mnyama wa porini hasa dikidiki. Kwa Kirangi huitwa “ntangasa”. 

Ngoma hiyo ni kama mdundiko wa Kirangi ambao huchezwa na watu wa kabila hilo, mara nyingi mchana hasa wakati wa sherehe kama harusi na kadhalika.

Majina yao mara nyingi huendana na wakati uliopo, kwa mfano: Mwasu (jua), Mbula (mvua), Nchira (ngozi), Nyange, Ndudya, Kichiko (masika), Salala (kimvua kidogo), Mnjira, Kifuta, Mwapwani, Ichuka, Luji, Kidunda n.k.

Ndoa na uhusiano

Awali Warangi walipenda kuoana baina ya jamii zao wenyewe, na kama ilitokea wakaoana na jamii nyingine za pembezoni, basi yule mtu wa jamii hiyo ndiye aliyegubikwa na silika zao na si wao kugubikwa na silika za ugeni.

Na hata sasa hali hiyo inaendelea kwa jamii hii. Si tu watakuvutia kwa namna hiyo lakini ukweli ni kwamba, Warangi wamebarikiwa kuwa na maumbile ya kuvutia sana, maana wengi wao ni ‘wambuji’ (warembo) na wenye rangi mchanganyiko.

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari.

0685 666964 au bhiluka@gmail.com

WATANZANIA kama walivyo watu wa mataifa ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

1 Comments

  • avatar
    IBEDE PETER
    14/02/2021

    Aliyetoa maelezo amejitahidi kwa kiasi kikubwa,ila kwa upande wa majina ya Kirangi hapo amejaribu kidogo sana. Nilitegemea achanganue majina ya kike na ya kiume.Mfano majina ya kike;Luji~Maji ya mto,Huki ~asali, Mbula~mvua nk Majina ya kiume Isaka~pori au msitu,Majala~njaa, Isuja~pombe au kitu kilichochujwa,Lubuvu~kipindi cha kiangazi,Msami~anayehamahama nk Kuna haja ya kufanya utafiti zaidi,ila hata hivyo umetusaidia sana ktk mambo mengi.

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi