loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Vijana wajengwe kuwa wazalendo kwa nchi yao

URITHI wa kweli kwa kizazi cha sasa na cha baadae ni kukijenga katika misingi ya maadili na uzalendo kwa taifa ili kuimarisha usalama wa nchi leo na kesho.

Yapo mataifa yalioamua kuwekeza katika urithi huu kwa watoto na vijana kutambua kuwa, katika vipaumbele vyovyote, nchi yao ni namba moja na leo tunayashangaa mataifa hayo namna yalivyopiga hatua kimaendeleo

Mfano ulio dhahiri ni nchi ya Jamuhuri ya Watu wa China. 

Kwa tuliobahatika kuishi China, ni ukweli ulio wazi kuwa, kazi kubwa ilifanyika miaka ya zamani kujenga kizazi cha wachapakazi, kilicho tayari kupigania nchi kwa gharama yoyote na kuiweka ya kwanza katika kila jambo huku wakiisifia kama vile hakuna nchi nzuri duniani kama China.

Hali hiyo imewawezesha kuufanya uzalendo kuwa sehemu yao ya maisha na hiyo, imeisaidia China kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kasi na wepesi zaidi kwa kuwa, katika kila mpango wa maendeleo, hakuna anayepinga, bali wote wanakuwa na nia moja ya kulitekeleza kwa manufaa ya taifa na si kwa maslahi binafsi.

Kutokana na msingi huo, China imekuwa mfadhili wa nchi nyingi duniani zikiwamo za Afrika na Tanzania ikiwemo. 

Hizi ni pamoja na zile ambazo katika miaka ya mwishoni mwa 1970 na mwanzoni mwa miaka ya 1980, kiuchumi zilikuwa sawa na baadhi ya nchi hizo.

Katika hotuba zake, Rais John Magufuli, amekuwa akihimiza suala hili kwa juhudi kubwa ili kujenga kizazi cha watu wanaopenda kufanya kazi, wenye uchungu na nchi yao, viongozi watetezi wa wanyonge na wanaohakikisha wanatumia rasilimali za nchi kwa maslahi ya nchi na jamii kwa jumla.

Rais amekuwa akisisitiza Tanzania si masikini jambo ambalo ni la kweli kabisa.

Hata hivyo, ili rasilimali za nchi zilifikishe taifa kwenye mapinduzi makubwa ya kiuchumi kutoka uchumi wa kati ilipo hadi wa juu, lazima kupata kizazi cha wazalendo kweli kweli; kizazi kinachojihoji kimelifanyia nini taifa na si taifa limekifanyia nini. 

Kimsingi, bila uzalendo kwa vizazi vya sasa na vijavyo, hata miradhi hii mikubwa na ya thamani inayotekelezwa na serikali nchini, inaweza isiwe na tija kwa siku za usoni na malengo ya kuitekeleza sasa yasitimie.

Ndiyo maana jamii yote lazima ihakikishe inaunga mkono na kushirikiana na serikali kujenga vijana wazalendo wanaolitetea na kulisema vizuri taifa hili ama iwe wakati unaofaa, au usiofaa.

Hii iwe tofauti na ambavyo kwa miaka ya hivi karibuni, baadhi ya Watanzania wamejitahidi ‘kuipaka matope’ nchi katika ramani ya kimataifa ingawa, hila zao mara zote ‘zimegonga mwamba.’

Ndio maana ninasema, mambo makubwa tunayoyaona sasa yakifanywa na Serikali, yatakuwa na manufaa kwa jamii kama kila mmoja atanuia kujenga vijana wenye uzalendo wa kweli kwa taifa na hili, kuwa urithi wa kwanza kwa Watanzania.

Ndiyo maana ninaipongeza serikali kwa kuanzisha Somo la Historia ya Tanzania na kulifanya kuwa la lazima kwa elimu ya awali hadi kidato cha sita kwa Lugha ya Kiswahili. Hii nayo, ni hatua muhimu ya ujenzi wa uzalendo kwa taifa.

MAENEO mengi hapa nchini hususani mijini ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi