loader
MEENA ALLY Mtangazaji anayewanasa vijana kwa vionjo vyake

MEENA ALLY Mtangazaji anayewanasa vijana kwa vionjo vyake

KAUTHAR Ali Rashid  al maarufu kama "Meena Ally"  ni mwanahabari kijana mwenye vipaji vingi vinavyovuta kama vile ua bora linavyovuta kundi la nyuki kuja kuchukua chamvua.

Akiwa amezaliwa Zanzibar Mei 13, 1993 mwanadada huyu alianza kazi za habari akiwa na umri wa miaka 16, wakati alipofanya udahili katika Televisheni ya East Africa na baadaye kujiunga nayo alipomaliza shule.  Jina Kauthar ndilo lililoandikwa katika usajili wa uzazi.

Alipata elimu yake ya habari Dar es Salaam School of Journalism, Meena Ally ametambulika zaidi kwa vijana kupitia kipindi cha “Niambie” kilichokuwa kinawezeshwa na BBC Media Action.

Mtangazaji huyu  kijana ni machachari na ameweza kujizolea umaarufu  katika  mioyo ya vijana na watu wazima kutokana na namna yake ya kutangaza  vipindi  mbalimbali na vyenye kufikisha ujumbe  uliokusudiwa katika mazingira salama na yenye mvuto.

Meena ambaye muda wote wa mazungumzo ungelipenda kuendelea kuwa naye kutokana na ucheshi wake, kupenda  kutania anawafanya hata walio karibu naye kujisikia vyema.

Hivi  karibuni Mtangazaji huyo amejinyakulia Tuzo ya  Watu kwa kuwabwaga watangazaji wenzake  wa kike   ambao ni wakongwe kama Dj Fetty wa Clouds FM, Dina Marious  na Sofia wote kutoka  Efm Radio na Salma Dakota  wa Wasafi Radio.

Tuzo hiyo iliyofahamika kwa jina la 'Tanzania Consumers Choice Award’ ilishindanisha watu katika  makundi  ya fani  mbalimbali ambayo walikuwa wakipigiwa kura na mashabiki wao.

“Ushindi huu umenipa hamasa kubwa sana katika kuongeza  juhudi  zaidi  kwenye kazi zangu  huku lengo langu ni kutaka kung'ara zaidi hapa nyumbani   na katika siku za  usoni ninaamini kwamba  milango ya nje ya nchi itakafunguka  ili niwe Balozi mzuri wa nchi,”anasema Meena .

Mbali na ushindi pia kwa upande wa  mitindo ya mavazi  Vunja Bei  walimuona na  kumpa ushindi  kwa kuibuka kidedea.

Anasema maendeleo yake katika tasnia yametokana na juhudi zake na usaidizi mkubwa wa maeneo anayofanyia kazi kama Shirika la Utangazaji la BBC, Boss Ciza  wa Clouds Media na Uongozi wa Clouds Media Group.

“Hawa wamenishika mkono na kuniongoza,” anasema Meena.

Meena akifafanua zaidi kuhusu kipindi cha Niambie ambacho ndicho kilichompa umaarufu mkubwa alisema kilianzishwa wakati muhimu katika kuelekea Uchaguzi Mkuu Tanzania na Meena Ally alishiriki katika kampeni kubwa ya kuelimisha vijana kwa nini ni lazima kupiga kura na pia mchakato mzima wa kupiga kura unavyokuwa.

Anasema katika kipindi hicho walikuwa na kazi kubwa ya kuelimisha vijana kutambua mchakato wa kupiga kura. na waliona faida kwani kuna makundi mengi ya WhatsApp ilianzishwa na  wanajadiliana masuala mbalimbali yanayohusu uchaguzi.

“Tuna kazi kubwa ya kuwasaidia  vijana kujitambua, kujitathmini na kuwa mbele katika harakati za kuwa mzalendo na pia kushiriki katika fursa mbalimbali za kwania uongozi,” anasema Meena.

Kauthar au Meena amejikita zaidi katika shughuli za upashanaji habari zaidi kwa kubuni bidhaa za habari ambazo zinazungumza masuala ya vijana na wanawake zikikuza uelewa wa haki zao.

 

“Kuanzia mwaka 2015 nilifanyakazi na  BBC Media Action nikiandaa kipindi cha “Niambie”  na baadaYe nikajiunga na Clouds FM, mimi na Millard Ayo tunawaletea wasikilizaji wetu kipindi cha ” Amplifier”. Niambie na Amplifier kina mamilioni ya wasikilizaji Afrika Mashariki  na duniani kote,” anasema  Meena au tuseme Mina ikiwa ni kifupi cha  Muhaymina  jina alilopewa na wazazi wake.

Kutokana na mwenendo wake bomba katika sekta ya habari mwaka  2020 alitajwa na Jarida la   Citizen  kama mwanamke mwenye ushawishi mkubwa katika dunia ya digitali 2020 - 2021.

Meena katika maisha yake amekuwa akipigana tu sio kuuonesha vijana wanaweza lakini pia kushiriki kivitendo katika ubunifu na kuhakikisha bidhaa anazotengeneza zinabaki katika historia kama bidhaa bora inayovuta na inayopeleka ujumbe kwa nguvu kubwa.

Miongoni mwa mafanikio yake ni matangazo ya Tigo Fiesta 2018/2019 yaliyompatia wafuasi wengi sana kutokana na staili yake ya kutumia vichekesho katika uwasilishaji wake. Matangazo yaliyotumika yalikuwa mafupi, yanayopendeza na yanayotoa ujumbe murua wenye kumvuta mtu kubaki akitaka kujua zaidi au kushiriki katika tukio huku akiwapa wafuasi wake misemo mbalimbali ikiwamo  huu wa ‘hatuli kushiba tunakula kumaliza.’ 

Meena pia alishawahi kushiriki kama Mtangazaji ndani ya  shoo kali ya Bongo Star Search (BSS).

Kati ya mwaka 2011 na 2014 Meena alikuwa anafanya kazi katika televisheni ya  East Africa  na katika hili atakumbukwa sana kwa kipindi cha “Uswazi”. Kipindi hiki huelezea vituko uswahili yaani katika maeneo huru yasiyopimwa yenye vurugu nyingi na  vijana walikuwa wanakihusudu kwa namna kinavyoonesha pilikapilika za kumudu maisha uswahilini.

Kazi nyingine alizofanya Meena  ni pamoja na kuwa mshehereshaji. Aidha kwa nafasi hiyo alikuwa katika moja ya mikutano muhimu ya jukwaa la watangazaji na wasambazaji  (Broadcasters and Distributors Forum -BDF) kwa mwaka 2018, lililofanyika Ukumbi wa Nkrumah , Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam. Mkutano ulikutanisha watengeneza maudhui na waandalizi wamaudhui hayo, wizara ya habari, utamaduni na vijana na mgeni rasmi alikuwa waziri wa wizara hiyo wakati huo Dk Harison Mwakyembe.

Meena katika kuwafanyia uanaharakati vijana  alishiriki katika jukwaa la Ignite lililoendeshwa na BBC Media Action mjini London, Uingereza na waandishi walikutana kuelezeana uzoefu  na changamoto zinazowakumba vijana sasa duniani.

Alishiriki pia  katika mradi wa Malkia wa Nguvu uliokuwa na lengo la kuonesha fursa za ujasirimali kwa wanawake na pia kuhimiza washiriki katika harakati za kujinasua katika ukatili na ukosefu wa haki.

Kitu kimoja ambacho Meena anasema hatakaa asahau pale alipoamua kwenda televisheni ya Zanzibar kwa ajili ya majaribio ya sauti. Kipindi hicho alikuwa anasoma High View International ya mjini Zanzibar, pamoja na kwenda kwenye televisheni pia alienda Zenji FM Radio kwa kusudio hilo hilo.

Meena amesoma katika shule mbalimbali Zanzibar na Dar es Salaam  kabla ya kujiunga  na Chuo cha Uandishi wa Habari cha  Dar es Salaam kusaka Stashahada ya Uandishi wa habari.

Leo hii Meena  anatembea kifua mbele kutokana na mafanikio yake katika kuwatengeneza vijana kujitambua na kushiriki fursa mbalimbali za kiuchumi nchini na hasa matumizi ya Tehama katika kubadili maisha yao.  Mwaka 2019, alipata tuzo ya Mwanamke wa mfano, tuzo iliyotolewa na Shirika lisilo la kiserikali la  Zanzibar Mwanamke Chakarika.

mdada huyu amekuwa championi wa kupigania haki za vijana na wanawake kupitia tasnia ya habari na pia mdada huyu ni muigizaji na amekuwa katika tamthilia inayorushwa katika televisheni ya Sitco.

Mwaka 2019  na 2020 Meena alijikita sana katika kufanya kazi  na vijana na kutoka na ukweli huu  alifanikiwa kuzunguka nchi  nzima  kupitia miradi mbalimbali  iliyowahusisha vijana ikiwa ni pamoja na kutoa elimu namna ya kujilinda  na  mimba za utotoni na kujikinga na maambukizi ya maradhi kama vile UKIMWI.

Meena anakiri kuwa akiwa jukwani amekuwa akifanya kila ubunifu ili kuhakikisha kwamba wasikilizaji wake wanamuelewa. “Ukiwa na vijana na usipojua lugha yao ukazungumza nao kwa lugha hiyo watakuacha.”  

Akizungumzia kuhusu  malengo yake ya baadaye anasema kuwa safari yake bado ni ndefu  kwa sababu kila siku amekuwa anajaribu jambo jipya huku akitolea mfano wa kuwa miongoni mwa waigizaji kwenye tamthilia ya Mjumbe iliyokuwa ikirushwa na  kituo cha Azam TV  mwaka 2020 na kupitia tamthilia hiyo amefanikiwa kujiongezea  mashabiki.

Mipango yake ya baadaye ni kujiendeleza  na  pia ana ndoto za  kuing'arisha nchi kimataifa zaidi na kwenda  kufanya kazi kwenye mataifa ya nje  kama mtangazaji wa kimataifa na kufahamika duniani kote.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/ef61b63429486b7d1545fc374d8a5f0f.jpg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Beda Msimbe

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi