loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tari, makampuni binafsi yanajipanga kuzalisha alizeti kwa wingi

FAMILIA nyingi nchini hupenda kutumia mafuta ya alizeti kwa sababu yanatajwa kutokuwa na lehamu (cholesterol) na pia yana harufu nzuri kwenye chakula.

Kutokana na mafuta hayo kupendwa, uhitaji wake kwa jamii umekuwa mkubwa, hali inayosababisha bei yake kuwa juu kidogo kulinganisha na mafuta mengine.

Kwa umuhimu huo, serikali imefanya zao la alizeti kuwa miongoni mwa mazao ya kimkakati na hivyo imeongeza nguvu ili lilimwe kwa wingi na kwa njia ya kisasa zaidi.

Lengo kuu ni kupunguza pengo la mafuta ya kula yanayozalishwa nchini, hatua inayosabisha sehemu kubwa ya mafuta kuagizwa nje ya nchi. Mahitaji ya mafuta ya kula nchini ni tani 570,000 lakini tani 205,000 pekee ndizo zimekuwa zikizalishwa nchini.

Takwimu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) zinaonyesha kuwa zao la alizeti kwa sasa linachangia tani 143,500 za mafuta ambayo ni sawa na asilimia 70 ya mafuta yote ya kula yanayozalishwa nchini kwa sasa. Asilimia 30 nyingine ya mafuta inatokana na mazao mengine kama vile chikichi, karanga, ufuta, pamba na nazi.

Pamoja na mchango huo mkubwa, alizeti ni zao la muda mfupi, hupandwa kati ya miezi mitatu hadi minne na kustawi katika maeneo mengi hususani yale yanayopata mvua kidogo.

Maeneo yanayolima alizeti nchini kwa wingi, zao ambalo hutoa mafuta yenye kiasi kidogo cha lehemu na hivyo kuwa bora kwa afya za walaji, ni Singida, Dodoma, Manyara, Iringa, Morogoro, Tabora, Shinyanga, Simiyu na Rukwa.

Mratibu wa Utafiti wa Alizeti Kitaifa kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Ilonga kilichopo Kilosa, Morogoro, Frank Reuben, anasema serikali imeendelea kuweka mkazo mkubwa kwenye uzalishaji wa zao hilo kutokana na umuhimu wake.

Rais John Magufuli alipokuwa akizindua Bunge la 12, alilitaja zao la alizeti kuwa miongoni mwa mazao yatakayopewa msukumo mkubwa katika kipindi cha pili cha utawala wake, 2020-2025.

Reuben anasema hata Ilani ya uchaguzi ya CCM inahimiza kuongeza uzalishaji wa alizeti nchini  na pia inaagiza uhamasishaji mkubwa wa ujenzi wa viwanda vidogo ili kuongeza thamani ya alizeti vijijini.

“Jitihada za namna hii zimeonekana katika kipindi cha 2015-2020 ambapo inaelezwa kupitia ukurasa wa 31 (d) wa ilani kwamba, katika kipindi hicho viwanda kadhaa vya kuchakata alizeti vilianzishwa na kufufuliwa katika maeneo mbalimbali ya nchi,” anasema Reuben.

Februari 5 mwaka huu asilimia 93 ya wabunge waliochangia hotuba ya Rais Magufuli ya uzinduzi wa Bunge la 12 walizungumzia sekta ya kilimo huku zao la alizeti pia likiguswa.

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, akieleza mkakati wa miaka mitano wa kuinua kilimo nchini, anasema serikali inatarajia kuwekeza Sh bilioni 179 kwa ajili ya utafiti, uendelezaji na uzalishaji wa mbegu mbalimbali.

Kuhusu alizeti, Bashe anasema Wizara inawekeza katika utafiti kwa ajili ya kuendeleza mbegu aina ya chavua huru na chotara na kwamba mbegu za asili zinatunzwa wakati wizara ikiandaa sheria maalumu ya kuzilinda.

Mratibu Reuben anasema mkakati uliopo kati ya Tari na makampuni binafsi ya uzalishaji wa alizeti ni kufikia tani zaidi ya milioni mbili za mavuno ambazo zitachangia tani 700,000 za mafuta ya kula ifikapo mwaka 2025.

“Tunaangalia namna ya kushirikiana katika uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora za alizeti kwa bei nafuu ili kuchochea kilimo cha alizeti nchini,” anasema.

Anasema Tari inawaelekeza wadau wao wa maendeleo kutoa matarajio na makadirio ya mahitaji yao ya kila msimu unaofuata ili kuwaandalia mbegu za kutosha za madaraja mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya kila msimu.

Huku hayo yakiendelea, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na shirika la maendeleo la Uholanzi inaandaa Jukwaa la Alizeti nchini ambalo litawaleta pamoja wadau wote wanaojihusisha na uzalishaji, usindikaji na usambazaji ili wawe na mwelekeo wa pamoja katika kutimiza malengo ya kuzidisha uzalishaji.

Kuhusu mkakati wa kampuni yake, Mkurugenzi wa Temnar Co. Ltd iliyopo mkoani Mtwara, John Julius, anasema kampuni hiyo ina mpango wa kuongeza uzalishaji wa alizeti kufikia tani 600 na kusababisha wakulima 2,000 kuwa na soko la uhakika.

“Kiasi hiki cha alizeti itakayozalishwa yote itanunuliwa na Temnar na kusindikwa kupata mafuta ya kula takribani lita 200,000. Hii itapunguza uhaba wa mafuta kwa Kanda ya Kusini na nchi yetu kwa ujumla.

“Mpango wetu ni endelevu na Temnar tunatarajia kuongeza idadi ya wakulima na uzalishaji wa alizeti kufikia wakulima 7,000 ifikapo mwaka 2025 na uzalishaji wa mafuta ya kula kufikia lita 600,000,” anasema.

Anaeleza kuwa kampuni hiyo inashirikiana na Tari-Ilonga kwa kipindi cha miaka mitano sasa ili kupata mbegu na ushauri wa kitaalamu.

“Tari Ilonga imetupatia mbegu bora ya Record ambayo inafanya vizuri kwenye mikoa yetu ya Kusini na wakulima wanaipenda sana. Mwaka 2020 tumechukua mbegu na mwaka 2021 tumeshaomba kuandaliwa mbegu za kutosha. Hii mbegu ya Serikali inapatikana kwa bei nafuu na inatupa tija nzuri ya mavuno pamoja na mafuta. Tutaendelea kuipanda na kuichakata kwenye kiwanda chetu cha mafuta,” anasema.

Naye Ofisa Uzalishaji wa Kampuni ya Highland Seed Growers Ltd, Iddi Kapiteni, anasema kampuni yao ina mikakati ya kuendeleza zao la alizeti nchini kwa kulima mbegu za alizeti kutoka eka 50 za sasa hadi 200.

“Tutatoa elimu kwa wakulima tunaoingia nao mkataba wa kutulimia alizeti ili waongeze tija kwa eka. Tutaendelea kuwatambua na kuwafuatilia wakulima watakaonunua na kupanda alizeti yetu ili tuwape utaalamu waongeze uzalishaji kwa eka.

“Vilevile, kampuni yetu itaendelea kuwa karibu na watafiti wa zao hili kutoka Tari-Ilonga ili tuweze kuwapatia mrejesho wa matatizo kutoka kwa wakulima ili wayashughulikie haraka,” anasema.

Naye Ofisa Tathmini na Ufuatiliaji wa Shirika la Agricultural Development Denmark Asia (ADDA) la Dodoma, Frank Chipanta, anasema shirika hilo lina mpango wa kuwafikia wakulima 15,000 wa alizeti katika mkoa wa Dodoma ili kuwawezesha kupata soko la alizeti yao ya kilimo hai sambamba na mafunzo ya mbinu bora za kilimo hai cha zao hilo.

Anasema watawaunganisha pia wakulima na watafiti wa Tari Ilonga, kuunda vikundi na kuwapa elimu ya ujasiliamali kupitia wawezeshaji ngazi ya jamii ambao ni Mtandao wa Wakulima Wadogo (Mviwata).

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya BioSustain Tanzania Limited iliyopo mkoani Singida, Dk Riyaz Haider anaeleza umuhimu wa kuzalisha mbegu za ndani ya nchi na kulinda mbegu za asili.

Anasema kampuni hiyo inafanya kazi na wakulima wa alizeti wapatao 4,000 kwenye wilaya za Ikungi, Manyoni, Itigi, Mkalama, Singida na Iramba ambao wanatarajiwa kufundishwa kilimo bora cha alizeti ili kuendana na mabadiliko ya tabianchi.

“Pia Kampuni inawekeza kwenye kiwanda cha kusindika mafuta ya alizeti na tunategemea kikamilike mwaka 2022. Kiwanda hiki kitaongeza ufanisi wa uchakataji wa mafuta ya alizeti kutoka tani 50 mpaka tani 100 kwa siku. Pia tutajenga ghala la kuhifadhia,” anasema.

Anasema wataendelea kuzalisha mbegu za ndani kwa kushirikiana na Tari kama ambavyo wamefanya kwa mwaka 2018 na 2020.

“Kampuni yetu inaamini kwamba Tanzania itakuwa nchi inayouza mafuta na mbegu bora kwenye soko la dunia hasa kipindi hiki ambacho Serikali imeamua kulinda hata mbegu za asili. Nchi yetu ina uwezo wa kufanya vizuri zaidi kwenye zao la alizeti,” anasema.

Tari pia imekuwa ikishirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) pamoja na Jeshi la Magereza ili kufanikisha maendeleo ya kilimo cha alizeti nchini. Tari imekuwa ikishirikiana na majeshi hayo, siyo tu kwenye alizeti bali hata kuzalisha mazao mengine ikiwemo chikichi, mahindi, mpunga na maharage.

Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti Ilonga, Dk. Joel Meliyo anasema uzalishaji wa mbegu bora za mazao ya mafuta hasa alizeti ni mojawapo ya majukumu ya kitaifa ya kituo hicho.

Anasema Tari kwa kushirikiana na wadau wengine inapaswa kuzalisha mbegu za kutosha ili kupata mafuta yatakayokidhi mahitaji ya nchi na ziada kwa ajili kuuza nje.

Anasema wanapanga kuzalisha tani 4,500 ya mbegu za daraja lililothibitishwa ubora kitakachotosha kupanda ekari 3,750,000 ambazo zitatoa mavuno yanayotosheleza mahitaji.

WATANZANIA kama walivyo watu wa mataifa ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi