loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

  Waziri ataka mikataba viwanda vya sukari

WAZIRI wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Gerald Kusaya, awasilishe kwake mikataba yote ya viwanda vya sukari ili ajiridhishe na utekelezaji mikataba ya kubinafsishwa.

Alitoa agizo hilo wakati akizungumza na menejimenti ya kampuni ya sukari ya Kilombero na wakulima wa miwa wa wilayani Kilombero, Morogoro.

Aliutaka uongozi wa kiwanda cha sukari Kilombero uharakishe mchakato wa uwekezaji kuongeza uwezo wa kuchakata miwa inayozalishwa na wakulima wadogo ili nchi ijitosheleze kwa bidhaa hiyo.

Profesa Mkenda alisikitishwa na taarifa ya Bodi ya Sukari Tanzania kuwa viwanda vya sukari vya Kilombero, havinunui wastani wa tani 350,000 za miwa ya wakulima wadogo ambazo kama zingechakatwa zingezalisha tani 35,000 za sukari.

"Hatuwezi kuwa mateka katika suala la uzalishaji sukari kwa kumtegemea mzalishaji mmoja. Tatizo wakulima wana miwa hainunuliwi na mwekezaji halafu nchi inaendelea kutoa vibali kwa mwekezaji kuagiza sukari nje ya nchi wakati anatakiwa kuongeza uwezo wa viwanda vyake kuchakata miwa ya wakulima" alisema Profesa Mkenda.

Wakati akizungumza na wakulima wa miwa wa wilayani Kilombero kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Sukari,  walimweleza kuwa mwekezaji kampuni ya sukari Kilombero hanunui miwa yote takribani tani 800,000 wanazozalisha.

Profesa Mkenda alisema, takwimu za uzalishaji miwa zinaonesha wastani wa tani 350,000 hazijanunuliwa na mwekezaji, Kampuni ya Sukari Kilombero na kwamba  zingetosha kuzalisha sukari tani 35,000.

Alisema kama kiasi hicho kingezalishwa nchi ingeagiza nje sukari tani 5,000 pekee kati ya 40,000 za upungufu wa sasa.

Aliagiza uongozi wa kiwanda cha sukari Kilombero uharikishe mchakato wa kuongeza uwezo wa kiwanda kuchakata miwa kutoka tani 629,000 mwaka 2018/2019 hadi tani 800,000 msimu huu ili miwa yote ya wakulima inayozalishwa itumike kuzalisha sukari.

Alipongeza hatua zilizochukuliwa na Rais John Magufuli alipoingia madarakani mwaka 2015 kudhibiti uagizaji sukari kutoka nje ili kutoa fursa kwa wawekezaji wa ndani 

"Kabla Rais Magufuli hajaingia madarakani nchi ilikuwa ikiagiza sukari tani 125,000 kutoka nje lakini kutokana na hatua za udhibiti serikali imefanikiwa kupunguza uagizaji wa sukari hadi wastani wa tani 40,000 mwaka 2020 ili kutoa fursa kwa viwanda vya ndani kuzalisha " alisema Profesa  Mkenda.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kiwanda cha Sukari cha Kilombero, Balozi mstaafu Ami Mpungwe, alisema kiwanda hicho ni kielelezo kizuri cha faida ya ubinafishaji kutokana na kuongeza uwezo wa kuzalisha sukari kutoka tani 28,000 mwaka 1998 hadi tani 128,000  mwaka 2020 kwa viwanda vyote viwili ( Kilombero I na Kilombero II)

Balozi Mpungwe alisema, Kampuni ya Sukari ya Kilombero inaendeshwa kwa ubia kati ya Kilombero Holdings Ltd (Mauritius) yenye hisa asilimia 75 na Serikali ya Tanzania yenye hisa asilimia 25 na inategemea miwa ya wakulima wadogo kwa asilimia 50 kuzalisha sukari.

"Kama kuna mtu ana fikra kuwa wakulima wadogo tunawadharau siyo kweli, tunawategemea sana ili viwanda vyetu viendelee na sasa tunalenga kufikia kununua miwa ya wakulima asilimia 60 baada ya upanuzi wa kiwanda mwaka 2023" alisema.

Balozi Mpungwe alisema wameanza kushawishi wabia wake kujenga kiwanda kikubwa, kitakachowezesha kuongeza uchakataji wa miwa ya wakulima na kwamba Sh bilioni 584 zinahitajika.

Alisema kiwanda hicho kinatarajiwa kukamilika mwaka 2023 na kitakuwa uwezo wa kuchakata tani 420 za miwa kwa saa, tofauti na sasa kwa kuwa zinachakatwa tani 220 kwa muda huo.

Takwimu za kiwanda hicho, zimeonesha kuwa hadi Februari 15 wamechakata tani 612, 000 za miwa kutoka kwa wakulima na wanatarajia ifikapo Machi watakapofunga msimu wafikishe tani 645,000.

Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Lazaro Londo, alisema, wakulima wanataka viwanda vya sukari vinunue miwa yote inayozalishwa takribani tani 300,000 ili upungufu wa sukari uishe.

"Kitendo cha kuwapa vibali wawekezaji hawa kuagiza nakisi ya sukari nje, inasababisha miwa ya wakulima kukosa soko, kwani kitendo cha kuagiza sukari nje makampuni yanapata faida kubwa huku wakulima wakiendelea kuwa masikini" alisema Londo.

WATANZANIA kama walivyo watu wa mataifa ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi