loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanzania yapata soko la maziwa Kenya

KAUNTI ya Migori nchini Kenya imekumbwa na uhaba mkubwa wa maziwa na kuagiza asilimia 10 ya mahitaji yao kutoka Tanzania.

Bodi ya Maziwa Tanzania imesema mahitaji hayo ni fursa kubwa ya biashara ya maziwa kwa Tanzania, hivyo imejipanga kuhakikisha  yanauzwa kwa utaratibu rasmi kwa manufaa ya wananchi na nchi.

Mtendaji wa Kilimo katika kaunti hiyo, Valentine Ogongo alisema juzi kuwa uzalishaji wa maziwa katika eneo hilo haujafikia mahitaji na takwimu za Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi zinaonesha kuna uzalishaji wa lita milioni 25 za maziwa kwa mwaka ikiwa ni chini ya mahitaji ya lita milioni 88 kwa mwaka.

Kutokana na upungufu huo, kaunti hiyo imelazimika kuingiza takribani asilimia 10 za maziwa yanayohitajika kutoka Tanzania, huku asilimia 20 ya maziwa yake yakipatikana kutoka Trans Mara, Nandi na Homa Bay.

Ogongo alisema uhusiano mzuri kati ya Kenya na Tanzania umerahisisha kuingizwa kwa maziwa nchini humo.

“Tunategemea maziwa kutoka Trans Mara, Nandi na hata kutoka Tanzania. Wakulima wetu wana uwezo wa kupata maziwa kutoka nchi jirani kwa sababu ya uhusiano mzuri kati ya nchi hizi mbili, " alisema Ogongo.

Ongezeko la idadi ya watu, mabadiliko ya hali ya hewa, aina ya malisho wanayopatiwa ng'ombe yametajwa kama sababu zinazochangia upungufu wa maziwa katika kaunti hiyo.

Kutokana na uhaba huo, serikali ya kaunti hiyo imeshirikiana na Benki ya Dunia na wadau wengine kukuza uzalishaji wa maziwa.

Kaunti hiyo ilizindua mpango wa kutoa ng'ombe wa maziwa kwa wakulima wa miwa na tumbaku mwaka 2014, ambapo waliwekwa katika vikundi vya watu 10 na kupewa ng'ombe mmoja, huku wakulima wengine wakipewa ndama kama kianzio cha kufuga.

Akizungumzia biashara hiyo, Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Noel Byamungu alisema wanatafuta kwa kiasi kikubwa soko la nje la bidhaa hiyo lakini kwa utaratibu maalumu.

“Kwa sasa nchi haijaanza kusafirisha maziwa nje ya nchi lakini katika kaunti hiyo ambayo iko mpakani na inapakana na kabila moja la Tanzania inawezekana kufanyika kwa biashara  hata hivyo siyo rasmi hivyo tunafuatilia ili kuanza kuuzwa rasmi,” alisema.

Byamungu alisema hiyo ni fursa kubwa ya kuuza bidhaa hiyo nje hivyo ni lazima nchi kuwa na taarifa ya kiasi kinachouzwa na kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kufanya biashara na kupata vibali rasmi.

“Kuna maziwa mengi katika maeneo hayo na bodi ilikuwa ikishangaa yanaenda wapi, hii ni taarifa muhimu kwetu tutafuatilia ili kuweka utaratibu mzuri na kupata takwimu sahihi licha ya kuwa kutokana na ushindani wa kibiashara kwa maziwa inaweza kuwa changamoto,” alisema.

NAIBU Waziri wa Mawasiliano na ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi