loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

VIOLET LONGO: Corona ilinifanya nione uchungu wa mikopo

LICHA ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19 kwa Kiswahili Uviko-19) kuacha athari mbaya kwa wajasiriamali, wanawake wajasiriamali wameendelea kujituma katika shughuli zao za kujiongezea mapato.

Mmoja wa watendaji katika Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), anayekataa kutajwa kwa vile si msemaji, anasema: “Katika kipindi cha corona (Covid-19) umoja na mshikamano uliongezeka kwa baadhi ya familia, hali iliyotoa fursa kwa wanaume wengi kushiriki shughuli mbalimbali za nyumbani zilizokuwa zimeachwa kwa wanawake pekee.”

Diwani wa Kata ya Mwanga, Kigoma Mjini, Sharon Mashanya, amenukuliwa katika mitandao ya kijamii akisema: “Mwanamke akisimamia kitu, atahakikisha kinafanikiwa kwa vyovyote vile…”

Miongoni mwa wanawake walioendelea kujituma katika ujasiriamali wao na ‘kuvuka kigingi’ cha Covid-19 katika shughuli zao, ni Violet Longo; Mama wa watoto watatu anaowalea peke yake mkoani Njombe.

Violet anayeishi eneo la Idundilanga wilayani Njombe, kabla ya kujiunga na shughuli za ujasiriamali kwa kuanzisha kiwanda cha mikate, alikuwa anafundishi katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Njombe.

Katika mazungumzo na HabariLEO hivi karibuni, Violet anasema: “Nilianza kazi hizi kwa kuwa napenda kufanya biashara na upishi ni fani yangu niliyoisomea kwa ngazi ya certificate (cheti) na diploma (stashahada).

Anasema: “Nilianza na mtaji binafsi kisha, nikaanza kukopa ili kuboresha biashara. Wakati huo ili nipate mkopo, ilibidi kuweka rehani mali zangu za nyumbani kama makochi na TV.”

“Baada ya kurasimisha makazi yangu yaani nyumba, kupitia uwezeshaji wa Mkurabita (Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania chini ya Ofisi ya Rais-Ikulu), nilipata hati yangu ya hakimiliki ya kimila.”

“Nikaanza kuitumia kama dhamana kukopa benki maana hati hizi zinakubalika bila shida. Mwanzoni nilikopa Sh milioni sita na kisha, nikakopa tena Sh milioni 10 katika benki moja hapa Njombe (haitaji) na hadi sasa, bado ninapambana na marejesho ya mkopo.”

Violet Longo anasema, yeye ni mmoja wa wajasiriamali wanawake walioathirika na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19) ulioikumba Tanzania na nchini nyingine duniani, na kuwasababishia wanawake mateso mbalimbali yakiwamo ya kiuchumi.

Uchunguzi wa HabariLEO umebaini kuwa, hali hiyo iliyowakumba wengi, ndiyo ilikifanya Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) na wadau wengine chini ya ufadhili wa taasisi ya Women Fund Tanzania (WFT), kutoa mafunzo kwa wanahabari ili kuibua changamoto walizokumbana nazo wanawake katika kipindi cha corona.

Wadau wengine katika mradi huo ni pamoja na TGNP, African Women Leaders Network (AWLN), Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na taasisi ya Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF).

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tamwa, Joyce Shebe, kwa kuwa wanawake ndio walezi wakubwa wa familia na wazalishaji wakubwa katika sekta binafsi, yanapotokea majanga kama Covid- 19, wao huathirika zaidi sambamba na watoto.

Shebe anasema: “Kwa kuwa wanawake ni waathirika wakubwa wa majanga kama Covid, iwepo mikakati ya pamoja ya kuwasaidia badala ya kuwaacha wenyewe kwani kufanya hivyo, kunaleta madhara makubwa zaidi katika jamii nzima...”

Violet anasema: “Kwa kweli hakuna kipindi kilichokuwa kigumu kwangu na kilichonitesa, kama ilipoibuka corona mwaka jana maana corona ilinikuta kwenye deni na wateja wa biashara yangu wakapungua.”

Mbele ya Kamati ya Uongozi ya Mkurabita iliyokuwa mjini Njombe ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Daniel Ole Njoolay, Makamu Mwenyekiti, Immakulata Senje na Mratibu wa Mkurabita, Dk Seraphia Mgembe katika kiwanda chake, Violet anasema, wakati huo biashara yake ilikumbwa na changamoto nyingi ikiwamo ya kukatika hovyo kwa umeme na kuchukua muda mrefu kabla ya kurejea hali iliyomharibia bidhaa, pamoja na biashara kukosa wateja.

“Kipindi hicho nilikuwa na maadui wawili wa biashara yaani kukatika kwa umeme, na corona iliyoniondolea wateja…” anasema.

Awali katika mkutano wa kamati hiyo, Uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe na wajasiriamali walionufaika kwa kukuza mitaji yao kupitia mkopo benki kwa kutumia hati za hakimiliki za kimila, Violet anasema tatizo la umeme limekuwa likimsababishia hasara katika kiwanda hicho.

Anasema: “Umeme unaniathiri sana maana ukikatika na kukaa muda mrefu, kama ulikuwa umekanda unga wa mandazi au mikate, unachacha; unaharibika hiyo inakuwa hasara, na kama ulikuwa umeweka mikate kwenye oveni haijaiva sawasawa, au keki iko kwenye oveni, umeme ukakatika inakuwa ni hasara tupu na wakati mwingine, dukani unakuwa umechukua unga kwa ‘mali kauli’ (kukopa).”

“Unajua kama umeme umekatika, mikate au keki imeharibika, ukilazimisha kuuza, unafukuza wateja na ukiacha, mtaji unazidi kuteketea ndiyo maana kuna kijana mmoja kila siku alikuwa anakuja kuchukua mikate iliyoharibika kwenda kulisha kuku wake…”

HabariLEO lilipotaka kujua namna ugonjwa huo ulivyopunguza wateja, mwanamke huyo mjasiriamali anayeshukuru urasimishaji ardhi na makazi uliofanywa na Mkurabita anasema: “Kabla ya corona, wazazi wengi ambao ni wateja, walikuwa wanawanunulia watoto wanaokwenda shule mikate au mandazi kwa ajili ya chai asubuhi, lakini ugonjwa huu ulipoibuka na shule kufungwa, watoto wote walibaki nyumbani hivyo, mzazi anaona hawezi kuwanunulia wote mikate; wazazi wakahamia kwenye viazi.”

Anasema hali hiyo ilimyumbisha kibiashara maana wateja wake wakubwa ni wananchi wa kawaida.

Mjasiriamali huyo ambaye kwa sasa anamiliki na kuendesha kiwanda kidogo cha mikate kiitwacho ‘Eat More Bakery’ katika Mtaa wa Sido mjini Njombe, anaelezea namna nyingine alivyoathirika kiuchumi kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo.

Anasema: “Unajua licha ya kuwa na ‘bakery’ (kiwanda cha mikate), nina duka ninalouzia hiyo mikate na huko, nimepanga ninalipia kodi; sasa kwa wateja kupungua na wengine kuhamia kwenye viazi, marejesho yangu benki yalikuwa shida maana mauzo yameporomoka…”

Violet anaongeza: “Kwa kweli nilishuka sana kimtaji… Chukulia mfano kwamba, kama nilikuwa natengeneza labda mifuko saba ya ngano, nikashuka na kukanda mifuko miwili, lazima pesa yote itaishia katika marejesho ya mkopo wakati huuzi kitu hivyo, mtaji unakufa maana mauzo yanashuka, vitu vingine vinaharibika, na huku unapaswa kufanya marejesho…”

“Kwa kweli wakati huo, nilijaribu kutafuta fursa, lakini nikaona zinakuwa ngumu maana sikutarajia kufikia hali hiyo… Nilikuwa na stress (msongo) za bakery na kutafuta wateja… Kwa kweli corona ilinifanya niuone uchungu wa mikopo, japo ina faida ukiwa makini na kama hakuna tatizo kama hilo.”

Anasema kikubwa alichojifunza, ni mwanamke kutotegemea sehemu au aina moja ya kipato, bali kuwa ma biashara za aina tofauti mradi tu, ni halali na za kiuadilifu.

“Nimejifunza kutotegemea biashara ya ‘nature’ (asili) moja, bali kuwa na tofautitofauti…” alisema na kuongeza: “Hata wanawake wenzangu, waachane na tabia ya utegemezi, badala yake wathubutu kufanya kazi mbalimbali zikiwamo za ujasirimali, bila kuchagua kazi mradi tu, ni kazi halali.”

Lingine alilojifunza anasema: “Sikuwa najua kuwa katika mkopo ukiyumba kibiashara unaweza kwenda benki (mkopeshaji) mkazungumza na kupanga namna ya kukuwezesha kumudu marejesho huku ukiendelea na biashara; hilo nimelifahamu baada ya kuwaeleza wenzangu shida nilizopata hata kuyumba ndipo wakanifumbua macho.”

Mintarafu umeme kukatika hasa katika miezi ya Novemba , 2020 hadi Januari 2021, kamati hiyo ilipokuwa Njombe, anasema, hali ilikuwa mbaya na ilimtia hasara.

“Lakini, baada ya kamati hiyo ya Mkurabita kutembelea hapa (kiwandani) na mimi kuelezea kero hii, mambo yamekuwa mazuri haraka kuliko matarajio.”

 “Tatizo la kukatika ovyo kwa umeme limepungua kwa kiasi kikubwa sana… Kwa kweli ujio wa Kamati ya Uongozi ya Mkurabita hadi kwenye kiwanda changu mwezi uliopita, umeleta mabadiliko makubwa tena chanya maana kwa sasa unakatika mara chache sana na ikitokea umekatika, unawahi kurudi,” anasema Violet.

Mintarafu anavyonufaika na ujasiriamali wake mbali na kumudu huduma za nyumbani kama chakula, afya na elimu kwa watoto, anasema: “Mwanzoni nilikuwa nikitengeneza mikate, au maandazi, ninabeba kichwani kupeleka kwa wateja.”

“Lakini sasa,” anasema: “Baada ya kupata hatimiliki ya kimila na kukopa benki, nilinunua kirikuu (gari ndogo ya mizigo) na sasa nina uhakika wa usalama dhidi ya mvua na vumbi; bidhaa zangu zinakuwa salama.”

Wadau mbalimbali wanasema, wajasiriamali kama huyu wanapaswa kuungwa mkono na mamlaka katika maeneo yao kwa kusaidia upatikanaji wa soko  katika taasisi kama shule na ofisi ili kuwanyanyua na kuwaendeleza.

 

WATANZANIA kama walivyo watu wa mataifa ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi