loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kilimo cha viungo Z'bar sasa kinakuja kivingine

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), awamu ya nane inayoongozwa na Dk Hussein Ali Mwinyi imejipanga kufanya kazi kwa kushirikiana na sekta binafsi pamoja na wawekezaji katika kukuza sekta ya kilimo cha biashara ili kuboresha maisha ya wakulima.

Kilimo cha mazao ya viungo kinatajwa kwamba endapo kitasimamiwa vyema ndiyo mkombozi wa wakulima kutokana na mazao hayo kuwa na bei kubwa katika soko la dunia.

''Tumeupokea mradi wa kilimo cha mazao ya viungo ambao matumaini yetu ni kuwa mkombozi katika kuongeza kipato chetu," anasema Semeni Hamada Simai, Mkulima  wa Maweni katika kijiji cha Mtende, Mkoa wa Kusini Unguja, baada ya kutambulishwa mradi huo.

Meneja wa Mradi wa Mazao ya Viungo na mbogamboga, Amina Ussi Khamis kutoka taasisi ya Jukwaa la Maendeleo ya Watu (PDF), anasema mradi huo wa miaka minne unatekelezwa kwa pamoja na SMZ kwa ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya kwa kushirikiana na asasi tatu nchini.

Anasema ni mradi ambalo upo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi  wanaojishughulisha na mazao ya kilimo cha matunda, mbogamboga na viungo na kwamba unalenga kuwawezesha kifedha.

Anasema mradi huo unakwenda kuwasaidia wananchi 21,000 na kufungua fursa za kilimo cha mbogamboga na viungo pamoja na kuongeza thamani ya wakulima kutokana na mazao wanayozalisha.

Anafahamisha kwamba miongoni mwa walengwa wa mradi huo ni wanawake ambao watafaidika kwa asilimia 55 pamoja na vijana kwa asilimia 33.

''Mradi huu miongoni mwa walengwa wakubwa ni wanawake na kundi la vijana katika uzalishaji wa bidhaa za mazao ya viungo na mbogamboga,'' anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa PDF kutoka Tanzania Bara, Jorua Kizito, anasema mradi huo ni fursa nyingine muhimu kwa wakulima kuchangamkia kwani mazao ya viungo na mbogamboga soko lake lipo kubwa na la uhakika.

Kwa mfano anasema soko la mbogamboga la ndani linatosheleza kuwawezesha wakulima kupata kipato kikubwa kama watalima kwa kutumia utaalamu ambao utatolewa na mabwana shamba na mabibi shamba nchini.

Anaongeza kwamba Zanzibar kuna hoteli nyingi za kitalii ambazo pia ni soko kubwa la kutumia mbogamboga na viungo vinavyozalishwa na wakulima wa ndani badala ya sasa ambapo mahoteli  yanaagizia nje ya nchi mazao hayo kwa kutumia fedha nyingi.

''Mradi huu umelenga kuwawezesha wajasiriamali wanawake kupiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kuzalisha bidhaa za viungo na mbogamboga zitakazoingia katika soko la kitalii," anasema.

Meneja miradi huo wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Zanzibar, Ali Mohamed Abdalla anasema wakati umefika kuirudishia Zanzibar hadhi yake ya kuwa kisiwa cha marashi ya karafuu na mazao ya viungo na hivyo kuwanufaisha wanawake katika uzalishaji wa bidhaa hizo.

Anasema utafiti unaonesha kwamba Zanzibar inao uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao mbalimbali ya viungo  yanayoweza kuingia katika soko la nchi za Ulaya, Uarabuni na India.

Anasema bidhaa za viungo zinazozalishwa Zanzibar ni za kipekee kutokana na ladha yenye ukali wa kuvutia  katika matumizi ya vyakula.

''Zanzibar tangu asili katika miaka ya 1930 ilikuwa ikisafirisha bidhaa za mazao ya viungo na kutamba katika soko la nchi za Ulaya hadi Bara Hindi na Asia huku bidhaa zake zikiwa na utambulisho wa aina yake," anasema.

Mazao ya viungo ambayo yamepewa kipaumbele kulimwa kwa wingi na wakulima wa Zanzibar ni pilipili manga, pilipili hoho, hiliki, uzile, mdalasini na vanila.

Kilimo cha mazao ya viungo na mbogamboga kimepokelewa kwa mikono miwili na wananchi wa shehia 50 ambazo mradi huo unatekelezwa huku wakiamini kitawasaidia kupunguza umaskini.

Sheha wa kijiji cha Mtende, Mkoa wa Kusini Unguja, anasema mradi huo ni muhimu kwani utawawezesha wakulima kulima kilimo cha biashara zaidi badala ya kilimo cha mazowea cha kujikimu.

Anasema utafiti umeonesha kwamba ardhi ya Maweni ambayo ni maarufu katika ukanda wa Kusini Unguja inao uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao mbalimbali ikiwemo mbogamboga hadi viungo.

''Wakulima wa kijiji cha Mtende walikuwa hawajishughulishi na kilimo cha mazao ya viungo na mbogamboga kwa kisingizio kwamba mazao hayo hayastawi vizuri, kumbe si kweli. Tumeona mabadiliko makubwa ya kilimo hicho baada ya wakulima kupewa utaalamu na mabwana shamba na mabibi shamba," anasema.

Kwa upande wa kitengo cha utafiti wa ufuatiliaji kupitia mradi katika taasisi ya Uhifadhi wa Misitu ya Pemba (CFP), Ali Mbarouk, anawataka wakulima kujipanga na kujiandaa kuupokea mradi huo ambao ni mkombozi katika kujikwamua na hali ngumu ya maisha.

Anasema ardhi ya Pemba ni miongoni mwa ardhi zenye rutuba nzuri na bora kwa ajili ya kilimo cha aina mbalimbali kuanzia cha mbogamboga, vyakula hadi viungo.

''Mradi huu umekuja kuwakomboa wakulima wa viungo na mbogamboga ambao wapo tayari kuzalisha bidhaa na kuingia katika soko la kimataifa, hatua ambayo itasaidia kuingiza kipato," anasema.

Mradi wa mazao ya viungo unatekelezwa kwa pamoja na Jukwaa la Maendeleo ya Watu (PDF) kwa kushirikiana na taasisi ya Uhifadhi wa Misitu ya Pemba (CFP) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar (Tamwa) chini ya ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya (EU). Jumla ya Euro milioni tano zimetengwa ili kutekeleza mradi huo.

Katibu mkuu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili na Umwagiliaji Maji, Mariyam Abdalla Juma, anasema Kilimo cha viungo na mbogamboga ni sehemu ya malengo na mikakati ya wizara yake katika kuona wakulima wanapiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kuchangamkia soko la ndani na fursa za uwekezaji nchini.

Anawataka wakulima kuongeza juhudi kuingia katika soko la viungo katika nchi za Urabuni na India ambalo halijatumiwa na wakulima nchini vya kutosha.

Anasema Wizara ya Kilimo ipo tayari kushirikiana na taasisi mbalimbali za ndani na nje ambazo zitasaidia katika kuwainua wakulima wa mazao ya viungo na hivyo kupiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kuingia katika soko la kimataifa.

''Serikali ya Zanzibar ya awamu ya nane tumejipanga kuhakikisha wakulima wanapiga hatua kubwa katika kilimo cha viungo na mbogamboga na kuingia katika soko la nje na ndani kwa mafanikio makubwa. Serikali imeimarisha taasisi zake za kilimo na utafiti kwa ajili ya wakulima wa aina hiyo," anasema.

 

WATANZANIA kama walivyo watu wa mataifa ...

foto
Mwandishi: Khatib  Suleiman

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi