loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mtibwa yataka ubingwa wa FA

KOCHA Mkuu wa Mtibwa Sugar, Hitimana Thierry amesema licha ya kushindwa kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, wanataka wapambane katika michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) ikiwezekana wafike mbali na kuchukua tena ubingwa.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Thierry alisema wanataka wapambane kupata ushindi kuanzia mchezo ujao wa mzunguko wa nne FA dhidi ya JKT Tanzania utakaochezwa kesho.

 “Uzuri ni kwamba mchezo wetu ujao wa FA tunacheza nyumbani, tunataka kupambana kuhakikisha tunashinda kwasababu lengo letu ni kufika mbali,” alisema.

Alisema kufanya vizuri katika michuano hiyo huenda kukarejesha morali kwa wachezaji kujitahidi kwenye ligi na kufanya vizuri.

Kocha huyo wa zamani wa Namungo alisema anajua JKT Tanzania sio timu ya kubezwa kwani na wao hawana matokeo mazuri na ni moja ya timu zenye ushindani mkubwa.

“Tunawaheshimu wapinzani wetu JKT ni moja ya timu nzuri, tunajiandaa dhidi yao tukijua kuwa mchezo hautakuwa rahisi ila lengo letu ni kushinda,” alisema.

Mtibwa Sugar imetoka kupoteza mchezo uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga kwa kipigo cha bao 1-0 uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Timu hiyo iliwahi kuchukua Kombe la  FA msimu wa 2017/2018 baada ya kuwachapa Singida United mabao 3-2 katika mchezo wa fainali.

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi