loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JPM atoa siku 3 wizara ikabidhi hekta 52

RAIS John Magufuli ametoa muda wa siku tatu kwa Wizara ya Mifugo kuachia eneo lenye ekari 52 na kulikabidhi kwa jimbo la Kibamba ili lifanyie shughuli za maendeleo.

Agizo hilo lilitolewa na Rais Magufuli wakati akizindua Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi jijini Dar es Salaam baada ya kuwasilishiwa maombi na mbunge wa jimbo hilo Issa Mtemvu.

Awali, mbunge huyo alipopatiwa fursa ya kuzungumza katika hafla hiyo aliwasilisha maombi yake kwa serikali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara tatu za Mpiji Majohe, Kibamba na Mbezi Makabe.

Alisema tangu aingie madarakani na kuwa mbunge wa jimbo hilo, barabara iliyojengwa kwa lami ni moja tu ambao ina kilometa tano tu.

Pamoja na hayo pia aliomba serikali itatue tatizo la maji kwa wakazi wa Kibamba ambapo kwa Dar es Salaam ambayo takwimu zinaonesha kuwa asilimia 92 ya wakazi wake wana maji, asilimia nane iliyobaki ni ya wakazi wa Kibamba ambao hawajapa huduma ya maji.

Pia alielezea kuhusu kuwepo kwa ekari 52 za Wizara ya Mifugo ambazo kwa sasa ni pori tu hazijaendelezwa na kuziomba ili zitumike kwa ajili ya masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwemo maeneo ya mikutano ya hadhara, viwanja vya michezo, vituo vya afya na maktaba ya jimbo.

“Unaona hata leo tunafanyia mkutano huu hapa, hatuna eneo la mikutano mikubwa kama huu ya hadhara. Eneo lile, mheshimiwa Rais akitupatia tutalibadilisha kwa faida ya wana Kibamba,” alieleza Mtemvu.

Rais Magufuli akizungumzia maombi hayo, aliridhia kumpatia mbunge huyo eneo hilo na kutoa siku tatu kwa wizara husika kukabidhi hati kwa Halmashauri ya Kibamba kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi