loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali yatumia ndege kuua nzige Siha

WAZIRI wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda amesema serikali ipo makini kudhibiti nzige waliovamia maeneo ya Tarafa ya Ngare Nairobi juzi jioni na tayari ndege imenyunyiza dawa kuwaua.

Profesa Mkenda alisema hayo jana alipotembelea Tarafa ya Siha Magharibi mkoani Kilimanjaro kujionea eneo lililovamiwa na nzige.

“Wananchi msiwe na taharuki nzige wote tutawamaliza na kazi imeanza jana kuwapuliza kiuatilifu kwa kutumia ndege inayomwaga sumu “ alisema.

Profesa Mkenda aliwaeleza wakulima wa Siha kuwa wizara hiyo inafuatilia kwa karibu maeneo yote endapo nzige wataonekana basi waangamizwe.

Alisema hakuridhishwa na kitendo cha Shirika la Kudhibiti Ndege wa Jangwani kumpeleka Kenya rubani wa ndege iliyopo Moshi na kuacha Tanzania ikikosa uhakika wa ndege endapo nzige wataendelea kusambaa.

“Sijafurahishwa na kitendo cha ndege yetu kupaki Moshi halafu rubani shirika la Kupambana na Nzige wa Jangwani wamempeleka Kenya wakati Tanzania ni mwanachama na michango tumelipia yote” alisema Profesa Mkenda.

Alisema, wizara katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 itatenga fedha za kuanzisha idara maalumu itakayoitwa Kilimo Anga na kuipatia vifaa vya kuangamiza wadudu wakiwemo nzige, kweleakwelea, na wengine.

Profesa Mkenda alisema, wizara hiyo itachukua hatua hiyo kutekeleza maagizo ya Rais John Magufuli kuhahikikisha kuna usalama na uhakika wa chakula .

“Hatutaki nzige watutoe kwenye mstari, tutawateketeza wote mahala walipo” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu alisema makundi ya nzige yalionekana juzi jioni kwenye mashamba ya Nanai, Nafco, Felisian kwenye kata ya Ngare Nairobi. Buswelu alisema wanashukuru serikali kwa kutoa ndege ambayo jana ilipulizia dawa kwenye mashamba hayo na kuwa wakulima wanaimani kuwa mazao hayataathirika.

Katika safari hiyo Profesa Mkenda alifuatana na Naibu Waziri Wizara ya Kilimo, Hussein Bashe.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Siha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi