loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

SMZ, Mambo ya Ndani kuimarisha usalama

RAIS wa Zanzibar, Dk Husseini Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) itaendelea kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha amani na usalama vinaimarishwa hapa nchini kwa maslahi ya wananchi na kulinda sekta ya uwekezaji.

Dk Mwinyi alisema hayo wakati alipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Boniface Simbachawene Ikulu Jijijini Zanzibar akiwa amefuatana na ujumbe akiwemo Naibu wa Wizara hiyo, Khamis Hamza Chilo.

Katika mazungumzo Rais Dk Mwinyi alimueleza Simbachawene kuwa, ushirikiano zaidi unahitajika kuhakikisha Zanzibar na Jamhuri ya Muungano zinaendeleza amani na usalama kwa kuwa ni tunu ya Taifa.

Alimueleza juhudi zinazochukuliwa na SMZ kuimarisha na kuendeleza sekta ya uwekezaji nchini ukiwemo utalii na pia mikakati ya serikali kuingia uchumi wa bluu.

Dk Mwinyi alieleza haja kwa wizara hiyo kushirikiana na SMZ kuhakikisha sekta hiyo inazidi kuimarika hasa ikizingatiwa mchango wake katika uchumi wa Zanzibar katika masuala ya ulinzi kwa watalii wanaoingia nchini.

‘’Matarajio yangu wizara ya mambo ya ndani ya nchi itaendelea kutoa mashirikiano kwa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar katika masuala ya ulinzi na usalama ikiwemo kwa upande wa watalii wanaoingia nchini kuona wapo salama’’alisema.

Mapema katika mazungumzo hayo, Rais Dk Mwinyi alipokea pole kutoka kwa Waziri Simbachawene kufuatia kifo cha aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad na kumuelezea marehemu kwamba alikuwa kiongozi imara aliyeweka maslahi ya taifa mbele zaidi katika suala la maridhiano ya kitaifa ambayo yamepelekea kuwepo kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Zanzibar

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi