loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanesco yataka kipaumbele matumizi ya maji

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO)  limeomba kupewa kipaumbele katika matumizi ya maji ikizingatiwa kuwa wanapofua umeme, baadaye maji hutumika kwa shughuli nyingine.

Aidha, limesisitiza Tanzania inao umeme wa kutosha na kama zipo changamoto basi ni chache zinazotokana na mambo mengine na siyo upungufu wa umeme.

Meneja Mwandamizi Ufuaji wa Umeme, Stephen Manda alitoa kauli hiyo jana wakati akiwasilisha mada kwenye kikao kazi kati ya Tanesco na wahariri wa vyombo vya habari nchini kinachofanyika mkoani Morogoro.

Manda alisema Tanesco imewekwa namba nne katika kipaumbele cha matumizi ya maji ambayo wao huyatumia katika kufua umeme.

"Tungependa angalau tuwe namba mbili kwani sisi tunatumia maji na kisha baada ya kuyatumia tunayarudisha tena kutumika katika shughuli nyingine kama kilimo," alisema Manda.

 

"Umeme ni kila kitu, viwanda na hata shughuli za kilimo cha umwagiliaji zinategemea umeme. Ukituwezesha sisi umewezesha wengine kufanya kazi zao.  Ukituwezesha sisi umewezesha viwanda, ukituwezesha sisi umewezesha kilimo cha umwagiliaji kusukuma pampu zao," alifafanua Manda.

 

Alisema kwa hali hiyo wanazungumza na mamlaka za mabonde ya maji ya Rufiji, Pangani na Ruaha kuona  namna nzuri zaidi ya wao kupewa kipaumbele katika matumizi hayo ya maji.

Alisema hawakatai watu wengine kutumia maji lakini wanaona kuwa kwa sababu umeme unasaidia katika mambo mengi wangepewa kipaumbele cha kutumia maji hayo ili yakasaidie ukuaji wa sekta nyingine.

Tanesco inafua umeme kwa kutumia maji katika mitambo saba ikiwamo ya Mtera, Kidatu, Nyumba ya Mungu, New Pangani Falls, ambayo yote inatoa megawati 561.843.

Aidha, Manda alisema kwa sasa mabwawa ya Mtera na Kidatu yana maji ya kutosha ya kufua umeme kiasi kwamba hivi karibuni wanatarajia kuyafungulia maji ili kuepuka mabwawa hayo yasiharibike.

Kuhusu ufuaji umeme alisema Tanzania inao umeme wa kutosha wa megawati 1,604.81, na Desemba 22 mwaka jana,  nchi ilirekodi kiasi cha juu cha matumizi ya umeme ya megawati 1,180.53.

"Kwa sasa tunao umeme wa kutosha sana na upatikanaji wake ni asilimia 87.5. Kama zipo changamoto basi ni labda nguzo kuanguka wateja kukosa umeme. Lakini hadi vijijini umeme sasa ni mwingi," alisema Manda.

Manda alisema serikali kupitia Tanesco wanaendelea na miradi mingi ya umeme ukiwamo mradi mkubwa wa Julius Nyerere (JNHPP)  katika mto Rufiji.

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Morogoro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi