loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Upepo waua mmoja, wabomoa nyumba 550

MTU mmoja amefariki dunia na wengine 20 kujeruhiwa katika kata nane zilizoko katika Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga kutokana na upepo mkali uliosababisha pia nyumba zipatazo 550 kubomoka.

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga,Dk Halfany Haule aliliambia gazeti hili kwamba upepo huo mkali uliovuma usiku kucha wa kuamkia Februari 13,mwaka huu na kuharibu idadi hiyo ya nyumba, umesababisha watu   2,217  kukosa makazi.

Uharibifu huo mkubwa umevikumba vijiji vilivyo katika kata za Mfinga,Kalumbaleza, Mwadui,Muze,Mtowisa,Zimba,Milepa na Ilemba.

Alimtaja aliyepoteza maisha  ni mkazi wa kijiji cha Muze,Gloria Msongole (47) akisema aliangukiwa na ukuta wa nyumba aliyokuwa amekimbiliia kwa usalama wake. Mwili wake ulisafirishwa kwenda  Mbeya kwa maziko.

Kuhusu watu 20 waliojeruhiwa katika sehemu mbalimbali ya miili yao, mkuu wa wilaya alisema walitibiwa katika vituo vya huduma za afya na kurejea makwao.

Alisema baadhi ya nyumba zimeanguka na nyingine kuta zimepata nyufa kubwa ingawa watu wanaendelea kuishi.

Alisema kati ya nyumba 550,  majengo 10 ni ya taasisi za umma hususani shule za msingi na sekondari pamoja na zahanati.

Alitaja majengo hayo kuwa ni ya zahanati ya kijiji cha Kalumbaleza B, Shule ya Msingi  Mnazi Mmoja.  Shule ya Sekondari Mazoka pia imeathirika kutokana na paa la jengo la choo kuezuliwa.

"Nyumba mbili za walimu katika Shule ya Msingi Nkwilo mapaa yake yameezuliwa pia paa la nyumba ya Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mzia limeezuliwa lote" alibainisha.

Alifafanua kuwa mashamba na samani zimeharibiwa. Alisema tathmini ya kubaini hasara halisi iliyosababishwa na upepo huo inaendelea kwa kuwa mashamba mengi yamefurika maji ya mvua.

foto
Mwandishi: Peti Siyame, Sumbawanga.

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi