loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Watu milioni 6.4 wapatiwa elimu ya sheria

SHIRIKA linalofanya kazi ya kukuza upatikanaji wa haki kupitia uwezeshaji wa kisheria nchini (LSF) kwa kushirikiana na wadau wake, wametoa elimu ya masuala ya kisheria iliyowafikia watu takribani milion 6.4 na kati ya hao asilimia 45 walikuwa wanaume na asilimia 55 walikuwa wanawake katika kipindi cha mwaka uliopita.

Hayo yalibainishwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala kwenye mkutano maalumu kati ya LSF na wadau wake ambao ni mashirika zaidi ya 200 ya wasaidizi wa kisheria nchi nzima pamoja na mashirika yanayotekeleza miradi ya upatikanaji wa haki mijini ili kujadili masuala ya kiutendaji katika suala zima la utoaji wa huduma hiyo.

Ng’wanakilala alisema kupitia mkutano huo, LSF na wadau wake walipata fursa ya kujadili kuhusu utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa makundi yenye uhitaji hususani wanawake na watoto.

Alisema LSF imekuwa ikitekeleza mradi wa upatikanaji wa haki nchini katika kipindi cha takribani miaka 10 kwa kutoa ruzuku kwa mashirika mbalimbali yanayotoa huduma za msaada wa kisheria na huduma za wasaidizi wa kisheria ili kusaidia watu mbalimbali hasa wanawake.

“Wadau hawa wa LSF wamefanikiwa kutoa elimu ya masuala ya kisheria iliyowafikia watu takribani milioni 6.4 kati yao asilimia 45 walikuwa wanaume na asilimia 55 walikuwa wanawake. Tumekuwa tukifuatilia kwa karibu kazi zinazofanywa na wadau wetu, tunatumia taarifa hizi kwa ajili ya kupanga mikakati mizuri ya kuwafikia watu wengi  hasa wenye uhitaji kama vile wanawake na watoto. Lengo letu ni kuleta maendeleo kwa kuwa tunaamini hakuna maendeleo bila haki,” alisema Ng’wanakilala.

Alisema mkutano huo ulikuwa mahususi kwa ajili ya kuweka mipango mikakati ya kuendelea kufanya kazi pamoja kati ya LSF na wadau   wake   wa masusala ya haki na hasa mashirika ya wasaidizi wa kisheria katika kipindi cha mwaka 2021.

Mkurugenzi wa Shirika la Wasaidizi wa Kisheria Bumbuli (BPO) mkoani Tanga, Ramadhani Mtana, aliishukuru LSF kwa kazi kubwa ya kutoa ruzuku kwa wadau wake na hasa wasaidizi wa kisheria kwa kuwa suala la fedha limekuwa changamoto katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Kwa mujibu wa LSF asilimia 68 ya matukio yote yaliyoripotiwa yalitatuliwa na wasaidizi wa kisheria kabla ya kufikishwa mahakamani, asilimia 11 ya matukio yaliyoripotiwa yalipewa rufaa ya kwenda mbele kwa hatua zaidi na asilimia 17 ya matukio yaliyoripotiwa bado yanashughulikiwa mpaka sasa.

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi