loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Takukuru yaanika wahusika uporaji viwanja, nyumba Kariakoo

UCHUNGUZI wa vitendo vya rushwa ikiwamo waliojipatia viwanja na majumba katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam kwa njia ya dhuluma, umeiva.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Ilala, imeeleza namna uporaji huo unavyofanyika. Imeeleza kuwa wahusika wa uporaji wa viwanja na majengo mengi uliofanywa katika eneo hilo ni waliokuwa wasimamizi wa mirathi, matapeli na baadhi ya wafanyabiashara.

Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Ilala, Christopher Myava aliliambia gazeti hili kuwa hivi sasa ofisi yake ipo katika hatua za mwisho, kurejesha moja ya nyumba zilizokuwa zimeporwa kwa dhuluma.

Pia alisema ofisi yake inaendelea kupokea taarifa nyingi za malalamiko juu ya waliohusika na uporaji wa aina hiyo kwa ajili ya kuzifanyia kazi, kisha kuwachukulia hatua wahusika.

Alisema tangu kutolewa kwa taarifa ya uchunguzi unaoendelea chini ya ofisi yake katika eneo hilo, wananchi wengi wamempigia simu.

Wengine wanafika ofisi ya Takukuru ya mkoa, kutoa taarifa wakieleza walivyoporwa majengo yao.

“Kwa sasa tupo katika hatua za mwisho kuirejesha nyumba moja iliyopo katika eneo hilo ambayo baada ya uchunguzi wetu tulibaini kuwa mlalamikiwa hana haki, isipokuwa alifanya ujanja kwa lengo la kutaka kujimilikisha,” alisema Myava

Alisema uchunguzi uliofanywa na Takukuru kwa nyakati tofauti katika eneo hilo la Kariakoo ukiwahusisha walalamilaji na wengineo, umebaini kuwa wengi wanaolalamikiwa kupora nyumba na majengo hayo, ama walikuwa wasimamizi wa mirathi au ndugu wa karibu wa wamiliki wa majengo hayo.

Pia, Myava alisema walalamikiwa wengine ni wafanyabiashara waliopangishwa katika maeneo hayo, ambao hushirikiana na baadhi ya ndugu wa karibu wa wamiliki wa majengo hayo kuwatapeli.

“Pamoja na hao pia wapo baadhi ya watu ambao baada ya kuona wamiliki halali wa majengo wamefariki, hughushi hati na kujifanya kuwa waliuziwa nyumba hizo wakati siyo kweli,” alisema Myava.

Myava aliwataka wananchi hususani kutoka eneo hilo la Kariakoo, kutoa ushirikiano kwa Takukuru kufanikisha mchakato wa kubaini wahusika. Alisisitiza kuwa mchango wao ni muhimu katika kufanikisha suala hilo.

Alisema Takukuru Mkoa wa Ilala ipo macho na itazidi kuzifanyia kazi taarifa mbalimbali zinazofikishwa katika ofisi hiyo na kuwachukulia hatua wote watakaobainika na ubadhirifu wa aina yoyote.

Katika taarifa ya utendaji wa Takukuru kwa kipindi cha robo mwaka kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka jana, iliyotolewa mwezi uliopita, taasisi ilisema inakamilisha uchunguzi kwa baadhi ya wafanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar es Salaam wanaodaiwa kujipatia viwanja na majumba katika eneo hilo kwa njia ya dhuluma na wengine wakidaiwa kukwepa kodi ya zaidi ya Sh bilioni saba.

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi