loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Jiji la Dar sasa kuboreshwa zaidi

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ambayo awali ilitambulika kama Manispaa ya Ilala, itaboresha miundombinu yake zikiwemo barabara za maeneo yote ili iendane na hadhi ya kuitwa jiji.

Aidha, halmashauri nyingine zilizopo ndani ya mkoa wa Dar es Salaam, zina uwezo wa kuwa majiji kama ilivyokuwa Ilala, endapo zitakidhi vigezo vinavyohitajika, kama vile ukusanyaji wa mapato ya ndani, miundombinu ya barabara na vigezo vingine.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Nyamuhanga alipozungumza na HabariLEO jijini Dar es Salaam jana.

Alisema mabadiliko yaliyofanywa na Serikali juzi yana lengo la kuongeza ufanisi wa kiutendaji wa halmashauri zote za mkoa wa Dar es Salaam, hususani jiji hilo lililobeba taswira kubwa ya nchi.

“Mabadiliko haya ya kimfumo, imani yetu yataleta tija hususani kimaendeleo kwa Taifa letu ikiwemo kuongeza wigo katika ukusanyaji wa mapato ya uhakika, jambo ambalo litazidisha kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa ujumla” alisema Nyamuhanga.

Aliutaka uongozi wa jiji hilo, kuendelea kuboresha miundombinu yake yote, itakayolifanya jiji kuwa na hadhi ya kuitwa jiji. Aliwataka wakazi wa jiji hilo, kuboresha makazi yao kulingana na mazingira yote wezeshi yanayoratibiwa na Serikali.

Kuhusu manispaa nyingine zilizopo ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, Nyamuhanga alizitaka kupambana kwa kushindana kwa kila namna na uongozi wa sasa wa halmashauri ya jiji kwa ajili ya kuziwezesha pia kuwa na hadhi ya Jiji.

Aidha alisema kutokana na lililokuwa Jiji la Dar es Salaam kuvunjwa, wafanyakazi wake wote takribani 200 watahamishiwa vituo vingine vya kazi vilivyopo ndani ya mkoa wa Dar es Salaam na wengine nje ya mkoa, kulingana na mahitaji ya sehemu watakazopelekwa.

Alisema aliyekuwa Mkurugenzi wa jiji hilo, Sipora Liana ameshapelekwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuwa mkurugenzi mtendaji. Taratibu za kuwahamisha watumishi wengine zinaendelea.

Alisema Serikali inazo ofisi mbalimbali katika mikoa yote, hivyo mahali popote watumishi hao wanaweza kupelekewa kwa ajili ya kuendelea na majukumu yao ya ujenzi wa taifa. Februari 24 mwaka huu, Rais John Magufuli alitangaza rasmi kuvunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na majukumu yake kuhamishiwa kwa iliyokuwa Manispaa ya Ilala.

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi