NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema Tamasha la wanawake litumike katika kuhakikisha wanatangaza utalii kwa kuhamasisha watanzania wanatembelea vivutio vya utalii.
Hayo yalisemwa wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani hapa wakati alipokuwa akizungumza na wadau wa utalii.
Masanja alisema wadau wanatakiwa kutumia wiki ya wanawake kuweza kuhamasisha utalii wa ndani.Alisema mikoa yote nchini inatakiwa kuhakikisha inatumia wiki ya wanawake kutangaza vivutio mbali mbali vilivopo katika mikoa yao.
Alisema mikutano mbali mbali pamoja na matamasha mengine yanayoendelea nchini kwetu nayo yatumike kuhakikisha wanahamasisha utalii.
Alisema wizara yake ipo katika mipango ya kuanzisha utalii na vijana ambapo vijana wengi watahamasika kutembelea vivutio mbali mbali vya utalii.
Ameitaka wakala wa Misitu(TFS) kuhakikisha wanasimamia vyema misitu na kusimamia maliasili kama Nyuki.
Ameitaka bodi ya utalii kanda ya Ziwa(TTB) kuhakikisha inatangaza utalii wa mikoa yote ya kanda ya ziwa na sio kutangaza tu utalii wa kisiwa cha Saa nane pekee.
Kwa upande wake,Kamishina msaidizi wa wakala wa Misitu,kanda ya ziwa(TFS), Ebrantino Mgiye amewaomba wadau kuhakikisha wana wekeza kwenye maeneo ya uhifadhi wa misitu katika wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza. Alisema maeneo ya hifadhi yanayoweza kuwekezwa ni kama Shamba la miti la Rubya,Nyarubeka na Indebezio.
Msimamizi wa kituo cha Utalii kutoka kanda ya ziwa(TTB),Gloria Muhambo alisema kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Corona wameamua kuhakikisha wanahamasisha utalii wa ndani.
Alisema katika wiki ya wanawake watahakikisha wanatembelea vivutio mbali mbali vya utalii. Alisema watatangaza utalii kupitia shule za msingi na vyuo vya Elimu viliopo katika kanda ya ziwa.a