loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mtaalamu ahimiza kula mikunde kuongeza kinga

Mtaalamu wa Lishe ya Binadamu kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe, Dk Ester Nkuba ameihimiza jamii kula mazao jamii ya mikunde ili kupata protini, vitamini na madini na kuongeza kinga mwilini.

Mazao hayo ni maharage, mbaazi, kunde, choroko, dengu, njugumawe, soya, fiwi, ngwara na njengele.

Akitoa ushauri huo hivi karibuni, Nkuba alisema tafiti zinaonesha watu wanaokula mikunde kwa wingi, wanapunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo, shinikizo la damu, kisukari na saratani ya utumbo mpana.

“Mikunde ni chanzo cha protini kinachopatikana kwa urahisi zaidi ukilinganisha na nyama.  Pia ni chanzo cha virutubisho vingi ikiwemo vitamini, madini, antioxidant na nyuzinyuzi.  Mikunde ina wanga na pia ina asidi ya folic, kopa, madini chuma na magnesiamu," alisema.

Mratibu wa Kitaifa wa Utafiti wa Mazao Jamii ya Mikunde na Mtafiti mgunduzi wa mbegu za mikunde kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI), Meshack Makenge, alisema Tanzania ni ya 12 duniani kwa uzalishaji wa mazao hayo.

Alisema ingawa uzalishaji wake bado upo chini ambao ni chini ya tani 0.9 kwa hekta, juhudi kubwa zinatakiwa kwa ajili ya kuongeza matumizi ya teknolojia mbalimbali zilizozalishwa na watafiti TARI hususani teknolojia ya mbegu kwa kuzihaulisha.

 “Ushirikiano wa wadau wote kwenye sekta ya kilimo waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa mazao jamii ya mikunde kama vile wazalishaji, wasindikaji, wafanyabiashara, wasafirishaji nje ya nchi na walaji wote unatakiwa ili kuleta tija kwa wakulima,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk Geofrey Mkamilo alisema taasisi hiyo inachangia kuzalisha mbegu bora na kila kituo cha utafiti nchini kinatakiwa kuwa na mazao ya kimkakati.

Mkurugenzi wa TARI Ilonga, Dk Joel Meliyo alisema utengenezaji wa mbegu bora za mikunde ni moja ya majukumu ya kituo hicho.

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi