loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

UNA yapongeza Tanzania mikopo makundi maalumu

ASASI ya UNA Tanzania imeipongeza serikali kwa kupitisha marekebisho ya kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotelewa na halmashauri nchini.

UNA Tanzania ambayo ni asasi ya Umoja wa Mataifa inayofanya kazi ya uwezeshaji vijana, wanawake na wenye ulemavu, imepongeza kile ilichoeleza ni usikivu wa serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Ofisa Miradi wa Vijana na Maisha wa UNA Tanzania, Lucas Fidelis, alisema wana imani kanuni hizo zitatekelezwa sawia.

Marekebisho hayo yalitangazwa katika Gazeti la Serikali Na 2017, Februari 26, 2021 kuhusu Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, (Sura ya 290), kanuni mpya zimetungwa chini ya Kifungu cha 37A (4).

“Sisi wadau tunaofanya kazi na vijana na makundi mengine mwaka 2019 tuliwasilisha marekebisho ya kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu baada ya wanufaika kueleza changamoto zinazowakabili,” alisema.

Akaongeza, “Maeneo yaliyokuwa na changamoto yalikuwa 10, lakini serikali imepitisha manne hivyo tunashukuru maana yatasaidia wanufaika kufanya kazi zao vizuri na kunufaika na mikopo hiyo kwa kuboresha maisha yao.”

Fidelis alisema idadi ya wanakikundi kupungua kutoka 10 hadi watano itawasaidia kunufaika na mkopo na usimamizi kuwa mzuri na wa karibu na itasaidia kuwavuta wengine kukopa zaidi na kuboresha maisha yao na kuwaondoa katika tabia na makundi hatarishi.

“Kikundi cha wanawake au vijana kitakuwa na idadi ya wanakikundi wasiopungua watano na kwa kikundi cha watu wenye ulemavu idadi ya wanakikundi wasiopungua wawili,” aliongeza.

Alisema kutengwa kwa fungu la ufuatiliaji kutasaidia kuondoa maombi yanayojirudia, kuweka mfumo mzuri wa waombaji na urejeshaji wa mikopo kwa vikundi husika.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, halmashauri yenye mapato ya ndani chini ya Sh bilioni moja, itatenga Sh 500,000 hadi Sh 1,000,000 kwa mwezi na yenye mapato ya ndani ya Sh bilioni moja hadi Sh bilioni mbili, itatenga Sh 1,000,000 hadi Sh 1,500,000 kwa mwezi.

Pia halmashauri yenye mapato ya ndani ya Sh bilioni mbili hadi Sh bilioni tano, itatenga Sh 1,5000,000 hadi Sh 2,000,000 kwa mwezi na  halmashauri yenye mapato ya ndani ya Sh bilioni tano na zaidi, itatenga Sh 2,000,000 hadi Sh 5,000,000 kwa mwezi.

foto
Mwandishi: Rahel Pallangyo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi