loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wamachinga 13,000 waandaliwa maeneo Stendi ya Magufuli

HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam imeanza utekelezaji wa agizo la Rais John Mgufuli la kupanua eneo la Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani na Nchi Jirani cha Magufuli ili kuwaruhusu wamachinga, mama lishe na baba lishe kufanya shughuli zao bila kusumbuliwa.

Ofisa Biashara wa  Halmashauri ya Jiji, Chacha Wandiba aliliambia HabariLEO kuwa awali waliandaa eneo la wafanyabiashara wadogo takribani 250, lakini baada ya kuwaruhusu watume maombi kupitia mfumo wa mtandao, idadi ilikuwa kubwa kupindukia.

Alisema mpaka sasa idadi ya wafanyabiashara wadogo, waliokwishatuma maombi yao kwa njia ya mtandao na na barua za kawaida, kutaka kufanya shughuli zao katika stendi hiyo ni zaidi ya 13,000 wakati eneo lililoandaliwa ni la wafanyabiashara wadogo wasiozidi 250.

“Kutokana na agizo la Rais Magufuli kuwa wafanyabiashara wadogo wanaojumuisha wamachinga, mama lishe na baba lishe wasisumbuliwe, tumeamua kuongeza eneo ili kuwachukua wote walioomba kufanya shughuli zao katika kituo hicho,” alisema Chacha.

Alisema kwa kuwa ujenzi wa kituo hicho unaendelea, kinachotakiwa kubadilishwa ni kutoka ramani ya zamani iliyoandaliwa kuchukua machinga 250 na kutengeneza ramani mpya itakayochukua wamachinga zaidi ya 13,000 kwa sababu eneo bado lipo.

Hivi karibuni Rais John Magufuli aliagiza wafanyabiashara wadogo (wamachinga), kuruhusiwa kufanya biashara katika kituo hicho cha mabasi cha Magufuli bila kusumbuliwa.

Alisema wakati stendi hiyo ikitarajia kupokea mabasi  zaidi ya 3,000, abiria watahitaji huduma na si wote wataingia katika kituo hicho, hivyo wamachinga watakaouza vyakula wanaruhusiwa wakiwemo mama lishe, kwani Serikali ya sasa inajali wananchi.

Alisema yeye ni mtetezi wa wanyonge na kwa kuwa kituo hicho kimepewa jina lake, anataka kuwa balozi wao. Alitaka mamlaka kutowafukuza stendi itakapoanza kazi kwa sababu ni kwao.

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi