loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Takukuru yabaini ufisadi wakandarasi miradi ya Tanesco

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imebaini uchepushaji wa vifaa kwenye miradi ya umeme ya Shirika la Umeme (Tanesco), unaofanywa na wakandarasi.

Sasa Takukuru imekabidhi vifaa ghafi vya umeme, vyenye  thamani ya zaidi ya Sh milioni 420, vilivyokuwa hatarini kuchepushwa.

Akizungumza katika ofisi za Tanesco Tawi la Mikocheni, Dar es Salaam jana,  Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru,  Brigedia Jenerali John Mbungo alisema  uchepushaji huo umekuwa ukifanyika kwa mbinu mbalimbali.

"Tumeokoa vifaa hivi, kulikuwa na mchezo wa uchepushaji wa vifaa kwenye miradi ya umeme, sasa tunasisitiza wakandarasi wakimaliza miradi vifaa vinavyobaki virudishwe kwa Tanesco au Wakala wa Umeme Vijijini (REA)," alisema.

Alisema vifaa hivyo vimerejeshwa na mkandarasi aliyekuwa akitekeleza mradi wa umeme wa REA Awamu ya Pili katika Mkoa wa Kigoma. Alisema vifaa hivyo ni transfoma 30 zenye ukubwa tofauti na balbu zisizotumia umeme mwingi 20,000, vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 420.

Alisema vifaa hivyo alivyovikabidhi kwa Tanesco, vilitakiwa viwe vimerejeshwa Tanesco  tangu mwaka  2017 na mkandarasi M/S JV States Grid Electrical &Technical Works Limited, aliyetekeleza mradi wa Kigoma na kuukamilisha mwaka huo.

 "Natoa rai  kwa wakandarasi wote wanaodaiwa, ambao walitekeleza miradi ya REA II kutoa ushirikiano kwa Takukuru  wa kurahisisha urejeshaji wa vifaa ghafi vya umeme walivyochukua bila idhini ya Tanesco au REA," alisema.

Alisisitiza, “Maelekezo ya Takukuru kwa wakandarasi ni kukabidhi vifaa vinavyobaki kwenye miradi ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa vikichepushwa kwa mbinu mbalimbali." 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Desemba 29 mwaka jana walikabidhi vifaa kama hivyo kwa Tanesco Mkoa wa Iringa vyenye thamani ya Sh bilioni 1.2  ambavyo vilikuwa vimepotea kwa mbinu mbalimbali zilizofanywa na wakandarasi.

"Baada ya hapo nikatoa maelekezo kwa wakandarasi wote wanaodaiwa vifaa vilivyobaki kwenye miradi, wafanye marejesho ndani ya siku 14,” alisema.

Wakati huo huo, Takukuru imefungua kesi tano kufuatia operesheni za uchunguzi zilizofanywa ndani ya Tanesco kuanzia Julai 2020 hadi Februari 2021.  Kesi hizo zinahusisha makosa mbalimbali yakiwemo ya kusababishia shirika hilo hasara ya Sh bilioni 2.7

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco,  Isack Chanji alishukuru Takukuru kwa hatua hiyo na kusisitiza wakandarasi kuwa waaminifu.

Katika hatua nyingine, siku moja baada ya Rais John Magufuli kuielekeza Takukuru kuchunguza kuhusu mkopo uliochukuliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam,  taasisi hiyo imesema imeshaanza utekelezaji wa agizo.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo alisema jana kuwa maofisa wa taasisi hiyo, wameanza kulifanyia kazi suala hilo kwa kupitia nyaraka zilizohusika katika mkopo huo.

"Tumepokea maelekezo na tayari watu wapo kazini wameanza kupitia nyaraka zote zinazohusu mkopo huo kwa halmashauri na taasisi ya fedha ulikochukuliwa mkopo” alisema.

Rais Magufuli katika ziara yake mkoani Dar es Salaam juzi, alitoa agizo hilo  wakati akizindua majengo ya Chuo Cha Polisi Kurasini, baada ya mbunge wa Temeke kuomba serikali iwasaidie kulipa Sh bilioni 12 walizokopa benki ya CRDB.

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi