loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

…Wasomi, wanasiasa wamkubali, wapongeza   

WANANCHI wa kada tofauti wakiwamo wanasiasa, wanadiplomasia na wasomi, wamepongeza uteuzi wa Dk Bashiru Ally kuwa Balozi na Katibu Mkuu Kiongozi, wakisema ni mtu makini na mwadilifu atakayeimudu nafasi hiyo.

Miongoni mwa waliozungumza na gazeti hili ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Magdalena Sakaya aliyesema Dk Bashiru anaweza kuvaa viatu vya Marehemu Balozi John Kijazi.

“Sina mashaka kuhusu utendaji na elimu ya Dk Bashiru,” alisema Sakaya na kushauri asichanganye na siasa ikizingatiwa kwamba alikuwa kiongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nafasi ya Katibu Mkuu, bali awe mtendaji kama mtangulizi wake.

Aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, David Kafulila, alisema anaamini moja ya sifa iliyomfanya Dk Bashiru kuteuliwa kuwa Balozi na Katibu Mkuu Kiongozi ni uadilifu alionao pamoja na uchapakazi.

Alisema pia kuongoza kwake kamati iliyosaidia kurejeshwa kwa mali za CCM na kujenga uwezo wa Chama kujiendesha, ni miongoni mwa sifa.

Alimtaja Bashiru kuwa ni mwanazuoni, mwenye nidhamu ya kazi na maono kuhusu nini anataka na uwezo wa kujenga falsafa ya chama.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda, alisema kazi ya Katibu Mkuu Kiongozi imempata mwenyewe kwa kuwa Dk Bashiru alisomea utawala wa umma na ni mbobezi kwenye eneo hilo.

Dk Mbunda alisema Bashiru ni mtu wa kusimamia misingi na mchapa kazi, hivyo kwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi ni mtu wa kutoa uongozi na sura ya utawala wa umma, anaamini ataifanya kazi hiyo vizuri.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif, alisema kwa kuwa Dk Bashiru alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,  hana shaka kuhusu uwezo wake katika kumudu majukumu.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Godwin Amani, alisema Dk Bashiru ni mtu mwenye akili nyingi, asiyetetereka kiutendaji, mnyenyekevu na pia ni mtu mwenye uchungu na fedha za umma na anayepinga matumizi mabaya ya fedha.

“Rais ana mamlaka ya kumteua mtu yeyote kuwa Balozi, kwa hiyo ubalozi aliompa Dk Bashiru ni cheo cha hadhi na angeweza kumteua Katibu Mkuu Kiongozi bila hata kumteua kuwa Balozi,” alisema Amani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Demokrasia na Utawala Bora Afrika (ForDIA), Bubelwa Kaiza, alisema Bashiru ataimudu nafasi hiyo ya  kwa kuwa hana makandokando, makundi na pia ni mchapakazi aliyesaidia CCM kushinda kwa asilimia 84 katika Uchaguzi Mkuu uliopita na kufanya aaminiwe zaidi.

Uhadhiri hadi Ukatibu Mkuu Kiongozi

Kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM mwaka 2018, Dk Bashiru alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Uteuzi kwa nafasi hiyo ndani ya chama, ulifanyika ikiwa ni siku chache baada ya kuongoza kamati iliyoundwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli  kuchunguza mali ya chama.

Mei 31, 2018 ndipo Dk Bashiru alikabidhiwa kijiti  cha kuongoza chama na mtangulizi wake, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, nafasi aliyoishika hadi jana alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.  

 

Makatibu Wakuu Viongozi waliotangulia

Katibu Mkuu Kiongozi wa kwanza alikuwa Dunstan Omari kuanzia mwaka 1962-1964, Joseph Namata (1964-1967), Dickson Nkembo (1967-1974), Timothy Apiyo (1974-1986).

Wengine ni Paul Rupia (1986-1995), Matern Lumbanga (1995-2006), Philemon Luhanjo (2006-2011), Ombeni Sefue (2012-2016) na Balozi John Kijazi (2016-2021).

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi