loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

EAC yapata Katibu Mkuu mpya

RAIS John Magufuli  ameshiriki mkutano wa 21 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), uliofanyika jana 2021 kwa njia ya mtandao.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema wakuu wa nchi sita wanachama walihudhuria na kumchagua Dk Peter Mathuki kutoka Kenya kuwa Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo.

Chini ya uenyekiti wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame aliyekabidhiwa uenyekiti wa Jumuiya katika mkutano wa wakuu wa jumuiya hiyo jijini Arusha Januari Mosi mwaka 2019, mkutano ulimshukuru Katibu Mkuu aliyemaliza muda wake, Balozi Liberata Mfumukeko kwa utumishi wake katika jumuiya.

Mkutano ulimteua pia Nestor Kayobera, Anita Mugeni na Kathurima M’inoti kuwa majaji wa mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki kuanzia jana.

Vile vile imewateua Yohane Masara, Richard Wejuli, Richard Muhumuza kuwa majaji wa jopo la kwanza la Mahakama ya Afrika Mashariki.

Mkutano huo uliamua Kenya itakuwa mwenyekiti mpya wa jumuiya na itafuatiwa na Burundi.

Vile vile ulipitia maombi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kujiunga na na jumuiya na kulielekeza baraza la mawaziri, kufanyia kazi maombi hayo kulingana na utaratibu wa EAC wa kuingiza wanachama wapya na wawasilishe taarifa katika mkutano mkuu wa 22.

Pia mkutano ulielekeza baraza kufuatilia maombi ya Somalia ya kutaka kujiunga na jumuiya.

Wakuu hao wa nchi walizingatia pia ripoti juu ya hali ya utekelezaji wa maagizo yake ya kufanya utafiti juu ya utaratibu wa kujumuisha Kifaransa kama lugha ya jumuiya, kitumike pamoja na Kiingereza na Kiswahili na kuagiza baraza kuharakisha taratibu za utekelezaji wa maagizo.

Nchi wanachama wa EAC ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi