loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Yapangeni maeneo ya vijiji yanayochipukia kuwa miji-Lukuvi

WAZIRI wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amezitaka wilaya zote kutambua maeneo yote ya vijiji yanayochipukia kuwa miji na kuyapangia mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Lukuvi amesema hayo jana wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za sekta ya ardhi katika Halmashauri ya wilaya ya Magu akiwa katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Mwanza.

Alisema baada ya serikali kuweka jitihada katika kusambaza umeme vijijini kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini  sasa vijiji vinaishi kimji na maisha yamebadilika ambapo vijiji vingi vimekuwa miji.

Alisema ni vizuri halmashauri ambazo ni mamlaka ya upangaji kuangalia ni vijiji gani vimechipukia kimji na kuvipangia matumizi bora ya ardhi yatakayoainisha shughuli kama vile  kilimo, ufugaji na kusisitiza kuwa wasipofanya upangaji mapema watashindwa kuvipanga baadaye.

Hata hivyo alisema katika maeneo ambayo vijiji vyake havina sifa ya  kuchipukia kuwa miji, halmashauri isimamie ujenzi wa makazi katika vijiji hivyo kwa kuviwekea utaratibu wa kujenga nyumba kwa mpangilio ulio bora.

"Kazi ya kupanga vijiji ni ya halmashauri kama ambavyo mnapanga kujenga madarasa matano kwa mwaka katika halmashauri, basi muweke malengo ya kupanga vijiji 10 kwa mwaka," alisema Lukuvi.

Katika hatua nyingine Lukuvi alikagua mradi wa upimaji ardhi eneo la Kisesa katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu na kuitaka halmashauri hiyo kuwatumia watendaji wa serikali katika kazi ya upimaji, badala ya kutegemea kampuni za upimaji alizoeleza kuwa wakati mwingine zimekuwa zikiwatoza fedha nyingi wananchi.

"Tumieni watumishi walio katika halmashauri kushambulia kupima maeneo mbalimbali na vifaa vya upimaji vipo vya kutosha katika ofisi za ardhi za mikoa,"alisema.

Hata hivyo, alisema kama halmashauri zitashindwa kupima maeneo kutokana na uchache wa watumishi zichukue wanafunzi wa vyuo vya ardhi ambapo aliagiza kazi zote zilizoshindwa kufanywa na kampuni za upimaji sasa zifanywe na watendaji wa sekta ya ardhi wa serikali.

Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mwanza, Eliah Kamyanda alisema mkoa wa Mwanza ni moja ya mikoa 16 iliyopewa fedha na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya programu ya  kuwezesha kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kwenye maeneo mbalimbali nchini na programu hiyo katika eneo la kisesa na Bujora itapima takriban viwanja 3,000.

Lukuvi alisema "Halmashauri ziisaidie serilali kutengeneza walipa kodi, hawa 3,000 ambao Wizara ya Ardhi imetoa shilingi milioni 220 kwa ajili ya mradi wa kupima na kumilikisha ardhi, nimeelezwa ndani ya siku 90 wamiliki wake watakuwa wamemilikishwa, nataka mwaka mmoja mpime viwanja 12,000 katika kata za Bujora na Kisesa".

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Magu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi