loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Bil 137/- kuboresha miundombinu ya shule

SHILINGI bilioni 137 zinatarajiwa kupelekwa katika halmashauri zote nchini kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule za msingi na sekondari mwaka huu wa fedha kupitia Mpango wa Kulipa Kutokana na Matokeo(EP4R).

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema hayo mjini Kasulu wakati wa Tamasha la utoaji zawadi kwa shule, walimu na wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa ya darasa la nne, saba na kidato cha pili na nne.

Alisema serikali itahakikisha kuwa inawekeza zaidi katika sekta ya elimu ili kukabiliana na changamoto ya miundombinu  ili kuwezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora na kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji.

"Kuna watu wamekuwa wakilalamika kuhusu changamoto za elimu, napenda kuwahakikishia kwamba serikali ipo kazini kupambana na changamoto zilizopo katika sekta ya elimu," alisema.

Kwa upande mwingine alizitaka halmashauri zote nchini kuongeza kasi ya kupambana na changamoto katika sekta ya elimu kwa kuweka mikakati ya ndani kwani fedha za miradi zinazopelekwa na serikali ni kwa ajili ya kuongeza nguvu.

Alisema ili kurahisisha utendaji kazi wa maofisa elimu na wathibiti ubora wa shule kufanya kazi kwa ufanisi, serikali imenunua magari 165 yatakayosambazwa katika halmashauri nchini na magari 66 kwa ajili ya wathibiti ubora wa shule yatakayosaidia kufanya ufuatiliaji wa taaluma katika maeneo yao.

Vilevile  Profesa Ndalichako alizungumzia mradi wa kuboresha elimu ya sekondari ambao utajenga shule za sekondari 26 kwa ajili ya watoto wa kike  ambazo zitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000 hadi 1,500 kila moja

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Saimon Anange aliwataka wadau wa elimu wakiwemo wazazi na viongozi mbalimbali katika ngazi zote kushirikiana kuanzisha hatua za kujenga maboma ya miundombinu ya elimu katika halmashauri zote mbili za Wilaya ya Kasulu ili kuondoa upungufu wa miundombinu hiyo.

Alisema mwaka huu kwa kuanzia wanatarajia kufyatua matofali 400,000 kwa ajili ya maboma ya madarasa.

Mmoja wa Mwanafunzi aliyepata daraja la kwanza kutoka  Shule ya Sekondari Bogwe iliyopo wilayani Kasulu, Anitha Sunzu aliishukuru serikali kwa kutoa elimu bora kwa watoto wa kitanzania bila ya upendeleo huku akiwataka wanafunzi wengine kusoma kwa bidii na kuwa na nidhamu kwa walimu.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu 

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi