loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Majaliwa aagiza uimarishaji mita za mafuta bandarini

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) iendelea kuimarisha usimamizi wa mitambo ya mita za upimaji wa mafuta ili kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali.

Pia, amesema serikali inataka kuona makusanyo yote ya mapato kutoka katika bandari zote nchini yanayokusanywa na TPA yanaingia katika mfuko mkuu wa serikali na haitakubali kubaki na mtu yeyote anayejihusisha na upotevu wake.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo jana baada ya kukagua mitambo ya mita ya mafuta Kigamboni na Kurasini Oil Jety (KOJ) kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

Hata hivyo, amesema ameridhishwa na utekelezwaji wa maagizo na maelekezo mbalimbali aliyoyatoa katika vipindi tofauti kuanzia mwaka 2016 alipofanya ziara katika eneo la mitambo ya mita ya mafuta ya Kigamboni na KOJ.

Alisema kipindi hicho teknolojia iliyokuwa inatumika haikuwa nzuri sana na ilikuwa inaifanya serikali kupoteza kiasi kikubwa cha mafuta na kusababisha mapato yaliyokuwa yakipatikana kuwa madogo, hivyo serikali iliyopita ilifanya maamuzi ya kununua mita ya Kigamboni.

Waziri Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuimarisha ununuzi wa mitambo hiyo kwa lengo la kuboresha bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara hasa kwenye sekta ya mafuta.

“Leo nimekuja kuona hatua sahihi tuliyofikia na nimeridhishwa na utekelezaji wake,” alieleza.

Alisema baada ya kuona mifumo ya upimaji si sahihi sana serikali ilipendekeza vinunuliwe viwanja Kigamboni ili kujenga matangi ambayo yatapokea mafuta kutoka bandarini, licha kupimwa katika mita yanapopelekwa kwa mteja yatapimwa tena kuhakikisha mteja anapata kiwango sahihi cha mafuta anachokihitaji.

“Nimefurahi kupata taarifa kwamba viwanja vimenunuliwa na sasa zabuni ya ujenzi wa matangi mapya inafanywa, tukishafika hapo Taifa litanufaika sana kuwa na mafuta mengi yaliyopo kwenye akiba yetu.

Pia hata wateja wanaotaka mafuta watakuwa wanaagiza wakati wowote kulingana na mauzo waliyoyafanya na kiwango wanachokihitaji kwa wakati huo,” alisema.

Alisema matangi hayo yatatoa fursa kwa nchi jirani ambazo zinatumia bandari hiyo kuagiza mafuta kwani watahifadhi mafuta yao na kuiwezesha bandari hiyo kufanya biashara ya mafuta ndani na nje ya nchi.

Ameagiza zabuni ya ujenzi wa matangi hayo iharakishwe ili ujenzi uanze mara moja.

Pia ameitaka TPA iimarishe usimamizi wa mita hizo za mafuta na ianzishe idara maalumu ya kuzisimamia katika bandari zote. Alisema watendaji wa idara hiyo ndio watakaowajibika kwenye utunzaji na utoaji wa huduma eneo hilo.

Awali, Mhandisi wa Idara ya Mafuta wa TPA, Yona Malago alimueleza Waziri Mkuu hatua zilizochukuliwa na TPA ili kuhakikisha ufanisi wa kushusha mafuta kupitia mita ya Kigamboni unafikiwa.

“Hatua ya awali ni ile iliyowezesha mita kufanya kazi bila kusimama na hatua ya pili ni kufanya ukarabati mkubwa wa mita ikiwemo kurekebisha machujio,” alisema Malago.

Alitaja hatua nyingine zilizochukuliwa kuwa ni kuweka wafanyakazi wenye sifa, vigezo na uwezo wa kusimamia mita hizo ikiwa ni pamoja na wahandisi, mafundi sanifu na mafundi mchundo wa umeme, mitambo na tehama na kufanya mafunzo kwa wafanyakazi wa TPA ambao wanasimamia utendaji wa mita hiyo.

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi