loader
Dstv Habarileo  Mobile
Ripoti ya Benki ya Dunia itusaidie kupiga hatua zaidi

Ripoti ya Benki ya Dunia itusaidie kupiga hatua zaidi

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya mwaka 2021 inayotolewa na Benki ya Dunia imeendelea kuitambua Tanzania kama nchi yenye uchumi imara unaoendelea kukua Afrika, licha ya changamoto ya ugonjwa wa Covid-19.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, Mara Warwick, Tanzania inaonekana kufanya vizuri kiuchumi licha ya kwamba bado umasikini ni tatizo.

Amesema kuwa ukuaji endelevu wa uchumi wa Tanzania katika miaka ya hivi karibuni umesaidia maboresho katika viwango vya jumla vya maisha. Alisema ili kuitekeleza vyema Dira ya Maendeleo ya Tanzania ifikapo mwaka 2025, nchi itahitaji juhudi za pamoja za kurudisha kasi ya ukuaji wa uchumi wakati ikipanua ufikiaji wa fursa za kiuchumi.

Alisisitiza inatakiwa kuendelea kuimarisha maisha ya wananchi wake, kuwa na sera bora za kiuchumi na kuboresha viashiria vya masuala ya kijamii.

Tunaipongeza Serikali ya Tanzania chini ya Rais John Magufuli kwa uongozi imara na thabiti ambao umesimamia sera na miongozo mbalimbali iliyofanikisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati wa chini, lakini yenye uchumi imara licha ya changamoto mbalimbali na hasa janga la ugonjwa wa Covid-19 ambao umeathiri nchi nyingi kiuchumi.

Kama ilivyoeleza Benki ya Dunia, Tanzania inazo programu nzuri ikiwamo ya kusaidia jamii zisizojiweza kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ambazo imeshauri kuwa zinapaswa kuwafikia watu wengi zaidi.

Tunaamini ushauri huu utafanyiwa kazi na serikali na Watanzania wengi watanufaika na programu za kuwakwamua kiuchumi. Na siyo eneo hilo tu, hata maeneo mengi ambayo ripoti hiyo ya Benki ya Dunia imeshauri, ni muhimu kuwekewa mkazo mkubwa ikiwamo kuzalisha zaidi ajira, lakini pia kulinda biashara changa, ndogo na za kati.

Pia kuboresha zaidi eneo la teknolojia katika biashara na kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Kama ambavyo serikali imekuwa ikiweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara kwa wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa, ni imani yetu kwamba Tanzania itaendelea kufanya vizuri katika kuzalisha ajira pamoja na matumizi ya teknolojia na hivyo kuifanya ipige hatua na kufikia uchumi wa kati wa daraja la juu.

Hili linawezekana kutokana na jinsi Serikali ya Awamu ya Tano ilivyojipambanua katika kusimamia rasilimali za Watanzania na kutoa fursa kwa wananchi wengi hasa wanyonge kufaidi matunda ya nchi yao.

Kubwa ni kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili kufikia malengo ambayo nchi imejiwekea. Lakini pia tuendelee kutoa vipaumbele ambavyo vitalitoa taifa katika umasikini kwa watu wake hasa vile ambavyo kama ilivyoeleza Benki ya Dunia vitagusa wananchi wengi na hivyo kuwafanya watoe mchango wao katika kujenga uchumi wao wenyewe na wa Taifa kwa ujumla. Inawezekana kila mmoja akitimiza wajibu wake.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/88a02b31e6acd02323981500a36be5d1.jpg

KWA mara ya kwanza leo dunia inaadhimisha ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi