loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kijaji: Wanawake acheni kujishusha Na John Nditi, Mvomero

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango wa zamani, Dk Ashatu Kijaji amewataka wanawake wajitafakari na kutambua kuwa nafasi ya mwanamke kuwa kiongozi ni kujiandaa, kujipanga, kuacha tabia ya kujishusha na kujirahisha kuwa hawawezi kitu chochote.

Dk Kijaji ambaye ni mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini mkoani Dodoma, alisema hayo katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake wa Chuo Kikuu Mzumbe mkoani Morogoro, yaliyofanyika Machi 4, mwaka huu chuoni hapo. Kijaji alikuwa mgeni rasmi.

Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu ya “Wanawake katika uongozi, chachu kufikia dunia yenye usawa.”

Wanawake wa chuo hicho walifanya maadhimisho hayo, kwa kuwa siku ya maadhimisho hayo duniani keshokutwa, Machi 8, watumishi na wanafunzi chuoni hapo watakuwa kwenye majukumu mengine ya kitaaluma.

Dk Kijaji alisema wanawake wanapaswa kupambana ili kufikia malengo yao ya kielimu, kijamii na kiuchumi ikiwemo kupambania fursa zilizopo na siyo kujirahisisha kwa namna moja ama nyingine.

Kaimu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Ganka Nyamsogoro alisema chuo kikuu kimeadhimisha siku hiyo huku kikihakikisha kuwa katika nyanja za taaluma na uendeshaji, chuo kinazingatia usawa wa kijinsia.

Profesa Nyamsogoro alisema wameweka mitaala maalumu ya wanawake ili waweze kuhitimu vyema kwa lengo la kuongeza idadi kubwa ya wahitimu wanawake

"Kwa mfano udahili wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2019/2020 ulikuwa na idadi na uwiano sawa ya wanawake na wanaume ;na kwa baadhi ya programu zetu idadi ya wanawake ni wengi kuliko wanaume,”alisema Profesa Nyamsogoro.

Risala ya Siku ya Wanawake chuoni hapo, iliyosomwa na Mhadhiri Mwandamizi wa chuo hicho, Verose Mushi, ilisema wanawake wa chuo hicho  wametoa elimu ya kujitambua kwa wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari zinazozunguka chuo hicho.

Mushi alitaja mafanikio mengine ni kuwezesha ukarabati wa vyoo vya wasichana na wavulana wa Shule ya Msingi Mzumbe, kutoa msaada wa vifaa na vyakula lishe kwa watoto wenye magonjwa sugu, wanaofikishwa kliniki ya Kituo cha Afya Mzumbe kilichopo chini ya Chuo Kikuu hicho.

foto
Mwandishi: John Nditi, Mvomero

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi