loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Vijana wahimizwa kukopa mikopo yenye riba nafuu

VIJANA nchini wamehimizwa kuchangamkia fursa ya mikopo yenye riba nafuu inayotolewa na Serikali kupitia halmashauri na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ili wajikwamue kiuchumi na kujiletea maendeleo.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi. Alisema hayo alipotembelea vikundi vya vijana mkoani Geita vilivyonufaika na mikopo yenye riba nafuu inayotolewa na halmashauri na Mfuko wa Maendeleo ya vijana,

Aliwaasa vijana kuchangamkia mikopo hiyo yenye riba nafuu ili waweze kuanzisha miradi ya uzalishaji mali kwenye jamii zinazowazunguka.

Alieleza kuwa Serikali kupitia halmashauri zilizopo nchini, imekuwa na ikitenga fedha asilimia 10 kupitia makusanyo ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kuanzisha miradi mipya au kuendeleza shughuli zao ambazo zitazalisha ajira zaidi na kuwasaidia kujiingizia kipato na hivyo kuchangia katika kuendeleza gurudumu la maendeleo.

Alisema lengo la Serikali kutoa mikopo hiyo ni kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira. Alisema Rais John Magufuli alipofungua rasmi Bunge la 12 jijini Dodoma Novemba 13, mwaka jana alieleza kuwa Serikali imeongeza jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwapatia mikopo isiyo na riba au yenye riba nafuu, ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri na pia kupitia mifuko na programu mbalimbali zilizoanzishwa na Serikali.

Katambi alitaka wakurugenzi wa halmashauri zote nchini, kuangalia namna bora ya kuanzisha mpango wa kutoa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara ili kabla ya kuwapatia mikopo vijana, wawajengee ujuzi utakaoimarisha biashara zao na kuzisimamia kwa weledi na kuwa na mbinu za kukuza biashara zao.

Alipongeza vikundi vya vijana alivyovitembelea, ikiwemo kikundi cha uzalishaji wa chaki kiitwacho Rubondo na kikundi cha vijana cha Geita Youth Group, kinachofyatua matofali. Alisema vikundi hivyo vimefikia hatua nzuri na vimechangia kasi ya ukuaji wa viwanda vidogo mkoani humo. Vikundi hivyo vitatengeneza ajira na kukuza uchumi.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Fadhil Juma alieleza kuwa halmashauri hiyo itaendelea kutoa mikopo na elimu kwa vikundi mbalimbali vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ili waweze kukuza mapato yao na kuongeza ajira kwa wengine zaidi.

Mnufaika wa kikundi cha Geita Youth Group, Jenifer Isaya aliishukuru Serikali kwa kuwaamini vijana kuwa wanaweza na kuwatengea mikopo hiyo yenye riba nafuu na kuwawezesha vifaa. Aliahidi vijana watachapa kazi kwa bidi na kurejesha mikopo kwa wakati ili kuwezesha wananchi wengine nao wanufaike.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi