loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Nyumba 600 Nkuhungu zazingirwa na maji

NYUMBA zaidi ya 600 katika kata ya Nkuhungu jijini hapa zimezingirwa na maji na chanzo  cha maji hayo inaelezwa kuwa ni kutoka katika madaraja makubwa matatu katika barabara kuu Dodoma- Singida ambayo yapo eneo la Mnadani, Nyanza na Nduvini.

Nyumba zilizozingirwa na maji  hayo   zipo katika mitaa minne ya  Bochela, Mtube, Salama na Mnyakongo na halmashauri ya jiji la Dodoma ikisema inaandaa viwanja kwa ajili ya wananchi hao ili wakaishi maeneo salama.

Wakizungumza wakati wa mahojiono wananchi wa maeneo hayo walidai kuwa hii si mara ya kwanza kwa nyumba zao kuzingirwa na maji na kuwa  changamoto hiyo imekuwa ya muda mrefu.

Mmoja wa wanakamati wanaofuatilia changamoto hiyo, Paulo Yohana alisema awali nyumba zilizokuwa zimezingirwa na maji zilikuwa 350 lakini kutokana na tatizo hilo kuzidi kuongezeka nyumba zaidi ya 600 zimezingirwa na maji.

“Tumekuwa tukifuatilia suala hili kuanzia   ngazi ya kata hadi mkoa na tuliambiwa  kuna wataalamu walioagizwa na Ofisi ya Katibu Tawala mkoa kwa ajili ya kupata suluhisho la jambo hili, tunaamini adha hii itapatiwa ufumbuzi na baada ya agizo hilo,  changamoto tuliyonayo ni kubwa, wananchi wanaishi kwenye mapagale unakuta chumba kimoja anaisha babu na wajukuu zake, kingine kaka na dada wanaishi pamoja hapo unategemea nini, serikali watusaidie changamoto hii,” alisema.

Mkazi  wa mtaa Mnyankongo Patra David alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto hiyo licha ya kuahidiwa kuwa tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi haraka.Alisema wakazi wengi wa nyumba hizo hawana makazi wanaishi kwa ndugu, jamaa na marafiki huku wengine wakijihifadhi kwenye mapagale ambayo usalama wake ni mdogo.

Mkazi wa mtaa wa Bochela Hadija Ramadhani  alisema zipo taarifa kuwa wao wamevamia maeneo madai ambayo  si kweli kwani wameishi kwa zaidi ya miaka 20 na kuongeza kuwa miaka hiyo tatizo hilo halikuwa kubwa kwani  nyumba chache ndio zilikuwa zikizingirwa na maji na kuiomba serikali kuwapatia msaada.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Mtube, Julius Machea alisema katika mtaa wake kaya zaidi ya 170 zimezingirwa na maji na tayari kaya 53 zimehama makazi yao na wamehamia katika mtaa wa Mbuyuni,  kata ya Kizota jirani na kata ya Nkuhungu.

Alisema licha ya madaraja hayo pia yapo makorongo zaidi ya manne ambayo maji yake yanaelekea kwenye makazi ya wananchi na kuongeza kuwa njia pekee ya kuondokana na adha hiyo ni jiji la Dodoma liwahamishe wananchi hao katika maeneo ambayo ni salama.

Mkurugenzi wa jiji la Dodoma Joseph Mafuru alisema kuwa zipo hatua mbalimbali wamezichukua ili kuwanusuru wananchi wa maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kuwaandalia viwanja eneo la Mahungu kwa ajili ya watu waliothirika ili wajenge makazi yao katika maeneo salama na kuwa hatua nyingine wanayoweza kuifanya ni kuyazuia maji hayo yanayotokea mlima wa Itega ili kuyaelekezea kwenye mtaro mkubwa wa maji.

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi