loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Waomba kusaidiwa kukamilisha ujenzi wa shule ya sekondari

WANANCHI wa kata ya Mbawala iliyopo halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara wameiomba serikali kusaidia kukamilishwa kwa ujenzi wa shule ya Sekondari ya Umoja B inayojengwa kwa nguvu za wananchi ili iweze kuanza kutumika mwishoni mwa mwezi huu.

Kauli hiyo imetolewa katika risala yao wakati wakipokea vifaa mbalimbali vya ujenzi kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Mtwara Anastazia Wambura.Mbunge huyo alikabidhi  tofali 1,000, nondo 12 za milimita 12 na saruji mifuko 20.

Wameitaka pia serikali kuipa usajili ili iweze kujwapunguzia adha wanafunzi ambao kwa sasa wanalazimika kusafiri umbali mrefu kufuata sekondari maeneo ya Nanguruwe wilayani humo.

Wananchi wa Mbawala walimwambia mbunge huyo wa Mtwara Vijiji kwamba ujenzi wa  Sekondari  ya Umoja “B”   inayounganisha vijiji vitano ambavyo ni Mailikumi, Mduwi, Nachenjele, Makome  A  na B umefikia gebo na wana matumaini ya kuanza kutumika mwishoni mwa mwezi huu baada ya kupata usajili.

Wananchi hao wamesema kwamba walianza mradi Septemba 14, 2018 na hadi kufikia mwaka huu 2021, mradi huo ambao upo katika eneo lenye ukubwa wa ekari 12  umeshatumia Sh milioni 26 ambapo nguvu fedha zilizotokana na michango  kwa ajili ya ununuzi wa vifaa kutoka kwa jamii na wadau mbalimbali ni zaidi ya Sh 22,570,000. Hata hivyo taarifa ilisema kwamba mpaka kufikia  hatua ya gebo  wanadaiwa Sh 3,430,000 na  malipo ya fundi ya Sh 1,400,000 na hivyo kufanya mradi mzima mpaka hatua ya gebo kufikia Sh  milioni 26.

Aidha  wamesema wanaishukuru  ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri chini ya uongozi wa Erica Yegella na madiwani wake  kwa kupokea mradi  huo na kutoa mbao, misumari ya kupaulia na bati  kwa ajili ya vyumba vya madarasa vinne,vyoo vya walimu na wanafunzi.

Naye mbunge Wambura  akikabidhi vifaa hivyo vya ujenzi aliwapongeza wananchi wa vijiji hivyo kwa kuamua kuwapunguzia umbali wanafunzi wa vijiji hivyo kwenda na kurudi shuleni na hivyo kupunguza madhara yake ikiwamo mimba za utotoni na utoro.

Diwani wa kata hiyo Rashid Mohamed alisema maamuzi ya ujenzi wa shule hiyo ni kuwapunguzia adha ya usafiri watoto wao ambao hulazimika kutembea kilomita 42 kwenda na kurudi  kutoka shule ya sekondari Nanguruwe.

Aidha kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia kupunguza changamoto za kufikiria usafiri kwa wazazi ambao kwa sasa wanalazimika kutoa Sh 1,000 kwa watoto wao kulipia mabasi kwenda na kurudi kwa kila siku ya masomo.

Wakazi wa eneo hilo, Esha Ismail na Ally Amuri walisema uamuzi wa wananchi kujenga shule hiyo kwa kujitolea kulitokana na tishio kubwa lililokuwepo la utoro na mimba za utotoni ikiwemo wanafunzi wengi kukosa masomo ikiwemo uchelewaji .

Mratibu Elimu Kata ya Mbawala, Getrude Frank alisema kwamba kuwepo kwa shule hiyo kutasaidia kuongeza ufaulu kwani watoto watakuwa karibu na makazi yao na hivyo kutobughudhwa na umbali wa usafiri unaochosha pamoja na ushawishi wa waendesha bodaboda na magari ya abiria.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Mtwara

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi