loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dk Abbasi: Msitoe holela habari za magonjwa

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi amevitaka vyombo vya habari nchini pamoja na wananchi, hususani wanaotumia mitandao ya kijamii, kuzingatia taratibu na misingi ya utoaji wa habari.

Alisema kazi ya kutoa habari zinazohusu serikali si ya kila mtu, bali zipo mamlaka zilizothibitishwa kwa ajili ya utoaji wa taarifa hizo.

“Hivi karibuni kumekuwa na tabia mpya ya baadhi ya vyombo vya habari, wananchi wa kawaida au maeneo mengine ya nchi, kujitolea tu taarifa nyingine zinazohusu serikali na taasisi mbalimbali za umma bila kuzingatia misingi ya utoaji wa taarifa,” alisema.

Alieleza kuwa hivi karibuni Rais John Magufuli, alitoa maelekezo na maagizo kwa serikali na viongozi katika utumishi wa umma watoe taarifa kwa umma, waeleze miradi na pia waeleze matukio mbalimbali yanavyotokea kwenye taasisi zao.

“Nimeona leo nisisitize tena kwamba serikali ina utaratibu wake wa kutoa taarifa mbalimbali, kwa hiyo watu wengine ambao hawahusiki na taratibu hizo, hawapaswi kuingilia huo mfumo au itifaki,” alisema Dk Abbasi.

Alisema kama ilivyo kwenye maeneo mbalimbali, hata kwenye magonjwa ya kuambukiza na magonjwa ya mlipuko, zipo taratibu kwenye Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari na Sheria ya Afya ya Jamii.

“Sheria hizo zimeeleza kwa mfano ni kiongozi kwenye sekta ya afya, wa kiwango gani anaweza kutoa taarifa.

Lakini vilevile mnakumbuka kwa mfano mwaka jana Tanzania ilipopata wagonjwa wa corona, Mheshimiwa Rais alitoa itifaki ya viongozi watakaosemea maradhi hayo,”

Aliongeza kuwa “Ukiondoa viongozi wakuu wa kitaifa akiwemo yeye mwenyewe (Rais Magufuli) na Waziri Mkuu, viongozi wengine waliopewa jukumu hilo walikuwa ni Waziri wa Afya wakati huo Ummy Mwalimu na mimi mwenyewe (Dk Abbas),” alisema.

Alisema kwa sasa wanashukuru ugonjwa wa corona umeendelea kudhibitiwa, lakini kutokana na maingiliano ya nchi na watu wengine duniani, wananchi wanapaswa kuendelea kuchukua tahadhari za dhati dhidi ya ugonjwa “Rais Magufuli ameendelea kusisitiza kuwa watu wasiwe na hofu, wafanye mazoezi, wale vizuri na waendelee na majukumu yao maofisini, mashambani na viwandani,” alisema

 Alisema wakati hayo yakiendelea vizuri, kumeibuka tabia ya baadhi ya watu kuanza kutoa takwimu zao za maradhi mbalimbali, vifo au wagonjwa, jambo ambalo alisisitiza kuwa si sahihi na kuvitaka vyombo vya habari kuachana na watu wa aina hiyo.

“Sasa naona kuna tabia mpya imejitokeza ya baadhi ya watu au mtu, anajitokeza anaanza kutoa takwimu zake kuhusu maradhi mbalimbali, kuhusu vifo na kuhusu wagonjwa. Hili kwa niaba ya Serikali naomba kusisitiza si sahihi. Tunaviomba vyombo vya habari viachane na watu wa namna hiyo.

“Narudia tena masuala ya utoaji wa takwimu na masuala ya kisera yanapaswa kubaki kwa wasemaji rasmi na wataalamu wenye dhamana ya kufanya hivyo.

Niombe sana jamii itambue kuwa mpaka sasa nchi yetu inakwenda vizuri, tumeondoa hofu, tunashiriki kwenye matamasha, tupo kwenye mipira na kwenye utalii watu wanakwenda,” alieleza.

Alisema kila mwanajamii, asasi za kijamii, viongozi wa dini na viongozi wa siasa, wanapaswa kushiriki kutoa elimu kwa wanajamii au watu anaowaongoza juu ya hatua za kuchukua zilizosisitizwa na serikali na wataalamu dhidi ya ugonjwa huo wa corona.

Alisema pia wanapaswa kushiriki na kuitoa jamii hofu na kuisisitizia kufuata yale mambo ambayo yapo kwenye miongozo. Alisema Watanzania wako viwandani, mashambani, maofisini, mashuleni na vyuoni, wakiendelea na shughuli zao.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi