loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ma-DC, DAS Dar kushitakiwa kwa Dk Bashiru

NAIBU Waziri wa Ofi si ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Mwita Waitara amepanga kuwashitaki wakuu wa wilaya na makatibu tawala wao wa mkoa wa Dar es Salaam kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Bashiru Ally.

Atawashtaki kutokana na kutohudhuria kikao chake cha kujadili utunzaji wa mazingira, alichokifanya Karimjee jana.

Amesema kukosekana kwa viongozi hao katika kikao hicho bila kutoa sababu wala kutuma wawakilishi, ni dalili ya dharau kwa sekta ya mazingira.

Kikao hicho cha jana ni hitimisho la ziara yake ya siku tano aliyoifanya na waliohudhuria ni wenyeviti wa serikali za mitaa na maofisa.

Waitara alisema kutokana na umuhimu wa kikao hicho, ilikuwa ni lazima kwa wakuu wa wilaya au makatibu tawala wao kuhudhuria, kwa kuwa kilihusika na utoaji wa uamuzi kuhusu uboreshaji wa mazingira.

Alisema yapo mambo ambayo yangepaswa kujadiliwa kwa pamoja mbele ya wenyeviti wa mitaa na alitoa mfano wa agizo la uboreshwaji wa bajeti za mazingira na uundwaji wa kamati za mazingira za kata.

Alisema ameshangazwa kwa kutoshiriki kwao na kuwa kwa sababu ziara hiyo aliyofanya ni agizo la Katibu Mkuu Kiongozi. Alisema sasa atamwelezea kitendo hicho cha wakuu hao, kushindwa kufika kikaoni.

Alisema kukosekana kwao, anakuchukulia ni kama amefanya kikao hicho na watendaji wake kwa kuwa waliohudhuria ni watendaji kutoka Baraza la Taifa Utunzaji wa Mazingira (NEMC) na maofisa wa ngazi ya kata, jambo alilosema hata akitoa maagizo hayatakuwa na nguvu hasa kwenye utekelezwaji wake.

Kuhusu namna ambavyo watendaji hao walishiriki kwenye uandaaji wa kikao hicho cha jana, alisema wazo la kufanyika lilitolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ambapo kwa upande wake alikuwa akitaka baada ya kumaliza ziara za Manispaa aendelee na shughuli nyingine.

Alisema:“Najua hawa wakuu wa wilaya au hao makatibu wakuu hao kushindwa kufika kwangu naona ni kama dharau, mbona wakati nikiwa Naibu wa Tamisemi hawakuwa wakikosa kufika, na tena eti naambiwa kuwa hawajafika sababu wametingwa na shughuli nyingine.

” “Wafahamu kuwa mimi ni yule yule, nimebadilishwa ofisi tu na ninachosisitiza kuwa ni lazima hili suala liwe fundisho, haliwezi kupita tu hivi hivi, au wanichukulia sababu mimi ni Mbunge wa Tarime ndiyo wananichukulia poa, wajue mimi ni kijana wa Ukonga.

” Alisema Rais John Magufuli ametoa upendeleo kwa uimarishwaji wa jiji la Dar es Salaam lote kuanzia Ilala, ambapo ndio jiji lenyewe hadi Manispaa zake mbalimbali hasa kwa kuweka miundombinu bora za barabara, madaraja na mambo mengine makubwa.

Lakini, kunakosekana usimamizi bora wa mazingira na kuwa wakuu wa wilaya wanapaswa kujadiliana kwa kina namna ya kuboresha mazingira.

Hata hivyo, wakati akiendelea kuzungumza walifika wawakilishi wa ofisi ya Halmashauri ya Jiji, ambapo Waitara aliwaambia kuwa hawezi kuwapatia muda wa kusalimia kwa kuwa wamemuudhi kwa kuchelewa.

Kati ya mambo ambayo naibu waziri huyo alisisitiza kwenye ziara yake hiyo ni kubadilishwa kwa namna ya uzalishaji wa chupa za vimiminika hasa juisi, chupa zenye rangi zinazotumiwa kuwekea vinywaji, akisema ni ngumu kusagika, hivyo wanaosaga chupa wamekuwa wakikataa kuzichukua.

Alisema hatua hiyo imesababisha wakusanyaji wa mitaani nao waziache, hali inayosababisha chupa hizo kujazana mitaani.

foto
Mwandishi: Evence Ng’ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi