loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mganga wa kienyeji adaiwa kuishi kinyumba na mwanafunzi

JESHI la Polisi mkoani Katavi linamshikilia mganga wa kienyeji, Mayala Hinyali (32) kwa tuhuma za kumtorosha na kuishi kinyumba na mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 16.

Msichana huyo anadaiwa kujiunga na Kidato cha Kwanza Januari mwaka huu katika Shule ya Sekondari Usevya iliyopo Halmashauri ya Mpimbwe Wilaya ya Mlele mkoani humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga alithibitisha kukamatwa kwa mganga huyo wa kienyeji, Hinyali. Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa na polisi Machi 3,mwaka huu nyumbani kwake Kijiji cha Kasekese katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.

Kamanda Kuzaga alisema wawili hao walikutwa wakiishi kinyumba kama mume na mke. “Baada ya mtuhumiwa huyo kumrubuni na kumtorosha msichana huyo alienda kuishi naye kinyumba nyumbani kwake” alidai Kamanda.

Alisema kukamatwa kwa mtu huyo, kulitokana na taarifa kutoka kwa wasamaria wema.

Alisema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani ili liwe fundisho kwa mtu au kikundi cha watu wenye tabia ya kukatisha ndoto za wasichana wanaoendekeza ndoa za utotoni.

Katika tukio lingine, Kamanda Kuzaga amesema wanawashikilia watu 15 wanaotuhumiwa kujihusisha na wizi wa pikipiki 14. Pikipiki hizo zinashikiliwa katika Kituo cha Polisi katika Mji wa Mpanda.

Alisema watuhumiwa hao wamekamatwa kufuatia msako mkali uliofanyika maeneo mbalimbali mkoani humo.

“Mbinu walizotumia watuhumiwa hao ni kwamba baada ya kuiba pikipiki hizo walifuta namba za chesisi na injini ili zisigundulike kirahisi kuwa zimeibwa,” alibainisha.

Kamanda Kuzaga alieleza kwamba watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na polisi na baada ya upelelezi wa awali wa shauri lao kukamilika, majalada yao yatafikishwa katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Katavi kwa hatua zaidi za kisheria.

Alitoa rai kwa wananchi walioibiwa pikipiki zao, wafike Kituo cha Polisi mjini Mpanda wakiwa na viambatanisho vitakavyowatambulisha kuwa wamiliki halali.

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: Peti Siyame, Mpanda

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi