loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Usafirishaji shehena kwenda  Burundi waongezeka maradufu

USAFIRISHAJI  shehena kwenda nchini Burundi kupitia bandari ya Kigoma mkoani Kigoma, umeongezeka maradufu.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko alisema hayo akitoa taarifa kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Maendeleo wa Burundi, Balozi Albert Shingiro.

Mawaziri hao walifanya ziara kutembelea miradi ya kimkakati ya kukuza ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi.

Kakoko alisema kuwa mwaka 2016 shehena yenye tani 320,000 ilisafirishwa kwenda Burundi na kufikia mwishoni mwa mwaka jana, usafirishaji huo uliongezeka na kufikia tani 550,000.

Mkurugenzi huyo TPA alisema kuwa usafirishaji huo wa shehena, unatarajia kuongezeka kutokana na upatikanaji wa mabehewa ya Shirika la Reli (TRL) huku meli tatu za Mv Liemba, Mwongozo na Sangara, zinafanyiwa ukarabati mkubwa utakaoongeza usafirishaji wa shehena kwa meli kwenda Burundi.

Wakati huo huo Kakoko alisema kuwa uboreshaji mkubwa wa miundombinu katika Bandari ya Kigoma, unatarajia kufanyika hivi karibuni chini ya Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).

Vitawekwa vifaa vya kisasa vya kushusha na kupakia mizigo, jambo ambalo pia litachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka usafirishaji wa shehena kwenda nchi hiyo jirani.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,  Dk Leonard Chamuriho alisema kuwa maboresho ya miundo mbinu yanayofanywa, yanalenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, maendeleo na kiuchumi kati ya Tanzania na Burundi kuleta maendeleo kwa wananchi wa nchi hizo mbili.

Pamoja na kutembelea Bandari ya Kigoma na Bandari kavu ya Katosho, Profesa Kabudi na Balozi Shingiro walitembelea Uwanja wa Ndege wa Kigoma na eneo maalumu la uwekezaji Kigoma (KISEZ), ambako walishuhudia mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia mionzi ya jua.

 

Akizungumza kwa nyakati tofauti akiwa kwenye ziara hiyo, Waziri Kabudi alisema utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati, unaonesha dhamira ya kweli ya Tanzania kutekeleza kwa vitendo ushirikiano wa kimaendeleo na kiuchumi uliopo kati ya nchi hizo.

Kabudi alisema kuwa ni lazima kila nchi ioneshe dhamira ya kweli ya utekelezaji wa mipango wanayokubaliana, ambayo ina manufaa makubwa kwa uchumi wa nchi hizo na maendeleo kwa ajili ya watu wake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Maendeleo wa Burundi, Balozi  Shingiro alisema kuwa kuimarika kwa uchumi wa Tanzania, kuna maana kubwa katika kuimarika kwa uchumi nchini mwake kutokana na ushirikiano na uhusiano mkubwa walio nao viongozi na wananchi wan chi hizo.

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: Fadhili Abdallah, Kigoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi