loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mikakati yaanza Dar liwe jiji la mfano

MIKAKATI ya kuendeleza na kubadili mwonekano wa Jiji la Dar es Salaam imeanza kutekelezwa, huku uongozi ukisisitiza kuwa ndani ya miaka miwili ijayo, litakuwa  na maendeleo makubwa na kivutio kikubwa cha watalii kama ilivyo Dubai.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto aliliambia gazeti hili kwamba, kwa kushirikiana na watendaji, wameshaandaa mkakati ulioanza kutekelezwa  ukihusisha uboreshaji miundombinu, masoko, kukabili uchafu, kuimarisha makazi na kuboresha mazingira ya wamachingi ili liwe jiji la mfano nchini.

 Miundombinu

Kwa kuanzia, maeneo ya pembezoni kama vile Chanika, Kipunguni, Kisukulu, Kivule, Bonyokwa, yameanza kufunguliwa kwa kuimarisha miundombinu ya barabara, hatua ambayo itavutia watu kuhamia na kuchagiza shughuli za maendeleo hatimaye kupunguza msongamano katikati ya jiji.

Alisema, Sh bilioni nne zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha madaraja hususani maeneo ya Ulongoni na jirani.  Halmashauri ya Jiji  imeelekeza  Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini(Tarura), kuanza ujenzi hususani barabara za Tabata, Majichumvi na maeneo mengine.

Wamachinga

Akizungumzia mwonekano wa katikati ya jiji , meya alisema wamejipanga na kuanza kwa kusaidia wafanyabiashara ndogo walioko katika maeneo hayo wenye bidhaa zinazotangazwa chini.

Alisema licha ya wamachinga kupatiwa vibali vya kufanya biashara, ni lazima ahakikishe zinafanyika kwenye mazingira salama zaidi na yasiyokuwa kero.

"Sasa huo ni mfano tu wa namna ambavyo wafanyabiashara watawezeshwa kupewa mazingira bora zaidi ya kufanya kazi na kuchagia mapato ya taifa, hii inaonesha ni kwa kiasi gani tumejipanga kuliweka jiji kuwa Dubai ndogo na litakuwa safi kuliko sehemu yoyote Tanzania hii," alisema Kumbilamoto.

Masoko

 

Kumbilamoto aliema, iliyokuwa Manispaa ya Ilala ambayo ilipandishwa hadhi na kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ina masoko mengi yanayoweza kuboreshwa na kusaidia kuchukua idadi kubwa ya wafanyabiashara.

Alitoa mfano wa Soko jipya la Kisutu, litakavyosaidia kuhudumia wafanyabiashara wengi. Alisema kabla ya kuvunjwa lilikuwa na wafanyabiashara 669 na  lilikusanya ushuru wa Sh milioni 100, lakini kwa sasa linaweza kukusanya ushuru hadi Sh bilioni 2.5 kwa mwaka. Ndani yake kutakuwa na huduma za benki.

Mpango uliopo ni kuboresha pia masoko ya Buguruni na Ilala Boma, yawe ya kisasa yachangie kukuza uchumi na kuweka mazingira bora zaidi ya jiji.

Kukabili uchafu

Kuhusu kero ya uchafu ambayo imekuwa ikilalamikiwa, Kumbilamoto alibainisha kuwa jiji linatarajia kuanza ujenzi wa dampo la kisasa lenye thamani ya Sh bilioni 100 katika eneo la Kipunguni. Alisema hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kukabili uchafu.

Alisema Manispaa ya Ilala ilishapewa magari ya kisasa ya kubeba taka pamoja na kuanza kwa ujenzi wa vizima sehemu mbalimbali. Mkakati uliopo ni kuhakikisha mapato yanayotokana na uchafu unaokusanywa kwenye kata, sehemu ya asilimia zinabaki kwenye kata husika kusaidia kukabili uchafuzi wa mazingira.

Uimarishaji makazi

Katika eneo la kuimarisha mazingira ya makazi ya watu, alisema lengo ni kuhakikisha kunakuwa makazi bora na ya kisasa. Alitoa mfano wa eneo la Malapa na kusema serikali imeshatenga Sh bilioni 11 kusaidia nyumba 665 zisibomoke.

Alisema katika kuhakikisha mazingira yanakuwa bora zaidi, jiji litaweka mfumo wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia kinyesi huku akisisitiza kuwa miradi hiyo itawekwa kwenye magereza ambayo ni Ukonga, Segerea na Keko na kwenye shule mbalimbali.

Jiji la mfano

Mikakati mingine ya kuboresha jiji ni kuwa na usimamizi madhubuti wa mapato ikiwa pamoja na kusimamia uanzishwaji wa vyanzo vipya vya mapato. Alisema kwa kuwa ofisi nyingi makao yake makuu ni katika jiji, atahakikisha pia zinashiriki shughuli za maendeleo ya kijamii.

Akisisitiza malengo ya kulifanya jiji kuwa la mfano, meya alisema yatajengwa maegesho ya juu kwa ajili ya magari, vyanzo vya utalii wa kale na kihistoria vitatumika kuingiza mapato .

Kwa upande wake, Mbunge wa Ilala, Musa Zungu alisema vipo vyanzo vingi vya mapato na kuwa kama kukiwa na mkakati madhubuti wa kuvitumia, jiji litakusanya fedha nyingi zaidi.

Alitoa mfano wa mapato mengi yanaweza kupatikana kwa njia ya kodi ya nyumba. Alisema Kariakoo pekee inaweza kukusanya hadi Sh bilioni 10 kwa mwaka kupitia kodi ya nyumba peke yake.

 

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: Evance Ng'ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi