loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

NMB yapiga jeki ukarabati hospitali Mtwara

BENKI ya NMB Kanda ya Kusini imetoa mabati 105 yenye thamani ya shilingi milioni tano kwa hospital ya Rufaa ya Ligula Mkoani Mtwara ili kusaidia uongozi wa hospitali hiyo kukarabati wodi ya watoto ambayo kwa sasa inafanyiwa matengenezo.

Meneja wa Kanda, Janeth Shango amesema msaada huo wa mabati ni sehemu ya jukumu la NMB katika kusaidia upatikanaji wa huduma bora za afya kwa jamii.

Amesema moja ya jukumu la NMB ni kusaidia jamii katika sekta ya afya kwa kutoa vifaa mbalimbali vikiwemo vya matibabu, vitanda vya kujifungulia kwa akina mama na vifaa vya ujenzi za wodi.

Katika sekta nyingine kama vile elimu, benki hiyo pia imekuwa ikitoa msaada wa viti na madawati kwa ajili ya wanafunzi. Mwishoni mwa mwaka jana NMB Kanda ya Kusini pia ilitoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo chakula kwa waathirika wa mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa ilionyesha siku mbili mfululizo mkoani Mtwara.

Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Dunstan Kyobya, Katibu Tawala wa Wilaya, Thomas Salala aliipongeza benki hiyo kwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia serikali na jamii kwa ujumla kuboresha huduma za jamii mkoani hapa.

“Kwa niaba ya Mkuu wetu wa Wilaya, napenda kuipongeza bank ya NMB. Wamekuwa wadau wakubwa sana katika kusaidia serikali kuboresha huduma mbalimbali za kijamii. Napenda kuwaalika wadau wengine waige mfano huu wa NMB,” amesema.

Akizungumzia suala la afya katika hospital hiyo, Salala amehakikishia NMB kuwa msaada huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha wodi hiyo ya watoto. Amesema serikali imedhamiria katika kuboresha huduma za afya kwa kuongeza watumishi na kuhakikisha miundombinu bora hivyo msaada huo wa NMB utakuwa chachu katika kusaidia juhudi za serikali.

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Ligula, Lobikieki Kisaambu amesema hospital inakabiliwa na uchakavu wa miundombinu isiyokidhi mahitaji kwa wagonjwa na watumisho na hivyo kuathiri utoaji wa huduma bora za afya na kwamba majengo mengi yamekuwa ni chakavu na yanahitaji maboresho.

Amesema maboresho ya majengo hayo na miundombinu yanahitaji jumla ya shilingi bilioni 3.6. Amesema moja ya jengo linalohitaji ukarabati ni wodi ya watoto ambapo ukarabati wake unahitaji shilingi milioni 24.8. Ukarabati wa wodi huo ulioanza mwaka jana umefikia asilimia 50.

foto
Mwandishi: ANNE ROBI Mtwara

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi