loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kabudi ataka bei za umeme zisiwe mzigo kwa wananchi

Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amezitaka kampuni zinazozalisha umeme na kuliuzia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuuza kwa bei ambazo hazitakuwa mzigo kwa wananchi.

Profesa Kabudi aliyasema hayo jana alipotembelea mradi wa kuzalisha umeme jua kwenye eneo la ukanda maalumu wa kiuchumi (KISEZ) mkoani Kigoma.

Aliyasema hayo baada ya Tanesco Mkoa wa Kigoma kumweleza kuwa wanatarajia kuanza kutumia umeme huo unaozalishwa na kampuni ya Next Gen Solawazi kwa kununua kwa Dola za Marekani 0.9 kwa uniti moja kwa mkataba wa miaka 20.

Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa Kigoma, Muhsini Kijemkuu alitoa taarifa hiyo kwa Profesa Kabudi akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Maendeleo wa Burundi, Albert Shingiro.

Kijemkuu alisema megawati tano zinatarajiwa kuzalishwa kwenye mradi huo na kutumiwa na TANESCO kwa ajili ya kusambaza umeme kwenye wilaya za Kigoma na Uvinza.

Alisema walikubaliana kuununua umeme kwa bei hiyo baada ya majadiliano ya zaidi ya miaka mitatu kwa kuwa kampuni ya Next Gen Solawazi ilikuwa ikiuuza kwa bei kubwa.

Kijemkuu alisema uamuzi huo unatokana na tatizo kubwa la upatikanaji wa umeme unaozalishwa kwa majenereta ya mafuta yanayotumia shilingi bilioni 25 kwa mwaka.

Kijemkuu alisema, mipango ya kuleta umeme kutoka kwenye gridi ya taifa mkoani Kigoma unaendelea na hadi Novemba mkoa huo utakuwa umeungwa kutoka mkoani Kagera (Nyakanazi) na pia mradi wa kuleta umeme kutokaTabora unaendelea.

Shingiro aliipongeza Tanzania kwa kutekeleza miradi inayolenga kuinua uchumi na kwamba mradi wa umeme wa gridi kwa mkoa Kigoma utachochea uwekezaji wa viwanda na Burundi iko tayari kutumia fursa hiyo kuwekeza Kigoma.

foto
Mwandishi: Fadhili Abdalla, Kigoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi