loader
THERESA MUKONA:   Adhihirisha nani kama mama

THERESA MUKONA: Adhihirisha nani kama mama

MWANAMUZIKI Christian Bella akimshirikisha  Ommy Dimpoz wameshawahi kuimba wimbo wa Nani Kama Mama wakielezea ubora wa mama kwa mtoto wake na hasa mapenzi ya kweli aliyonayo kwa watoto ambao amewaleta duniani.

Wimbo huu wa Nani Kama Mama uliwafanya watu waliokuwa wakishiriki kipindi kilichowaunganisha mama na watoto  baada ya miaka 43 kujikuta wakidondosha machozi ya uchungu na furaha, wakati unapigwa baada ya wahusika kuombwa kuchagua wimbo wa kuanzia kipindi.

Mwandazi wa kipindi cha Leo Tena cha Clouds, Gea Habib kwa mara nyingine tena aliweza kusaidia watu waliopoteana kwa miaka 43 kukutana kwa taarifa fupi tu aliyoiweka hewani Februari 25, mwaka huu, taarifa ambayo baada ya saa tatu ilizaa matunda.

Theresa Mukona (61) raia wa Kenya aliyeondoka nchini kukimbia uke wenza na kipigo cha mumewe akiwa na ujauzito na kuacha watoto watatu hapa nchini na kuishi kwa mateso makubwa kwa miaka 43 alirejea kwa bahati tu kupitia mtoto wake mwingine aliyekuwa anakuja hapa nchini kikazi na kuwaona watoto wake.

Anasema kwamba chanzo cha yote ni mtoto wake mmoja anayefanyakazi na kampuni iliyopo Dubai ya Swiss Brown ambayo ilimuagiza mtoto huyo kuja Dar es Salaam kuchukua mzigo ambapo mtoto alimuomba mama yake amsindikize. Pamoja na kutopenda lakini mama aliafiki na kumsindikiza Dar es Salaam.

Mukona anasema kabla ya kuondoka Mombasa alimpigia simu rafiki yake anayeishi Dubai kwa jina Saumu Tuma Kajiwe ambaye alimwelekeza kwa dereva wa gari ya kukodi Abasi na kumwambia kwamba atakuwa kwenye mikono salama na atamtembeza Dar es Salaam.

Mama huyo ambaye alizaliwa Tanzania katika mji wa Musoma kutoka kwa wazazi waliokuwa wafanyakazi nchini, alisomea shule ya Kiabakari na alipomaliza ndipo alipokutana na mume wake Juma Hassan Django aliyemzidi kwa miaka 12 na kuolewa naye.Waliishi katika kambi na anasema maisha yake hayakuwa mazuri kwa kuwa hakuwa anamwelewa mume wake.

Baba wa Mukona aliyesema kwamba anaitwa  Ryogi Moguche alikuwa akihudumu katika mgodi wa Kiabakari kabla haujafungwa na eneo hilo kukaliwa na Kikosi cha Jeshi, Kiabakari Bataliani ya 10 ambapo mumewe alikuwa anahudumu. Anasema pamoja na  kutomuelewa mume wake,aliolewa na kuwa na maisha ya furaha, lakini mume wake alipobadilika na kuwa zaidi ya mkorofi akaamua kuondoka. Aliachana na ndoa yao iliyofungwa kwa Mkuu wa Wilaya (Bomani).

Anasema kwamba wakati anaondoka baada ya kupokonywa watoto wake, mmoja akiwa na umri wa mwaka mmoja, huku akiwa na ujauzito alirejea kwao Kisii, Kenya akafanya kazi katika kiwanda cha Peremende cha Kisumu kabla ya kuingia Mombasa na kufanyakazi kazi katika hoteli sehemu ya huduma za kukanda maarufu kama masaji. Akiwa Mombasa ndipo alipokutana na mume wake wa sasa.

Kwa mujibu wa Theresa mwenye umri wa miaka 61 sasa, miaka yote alikuwa anamuomba Mungu amkutanishe na watoto wake na hata mwanae aliyetoka naye hapa nchini (ujauzito) alimweleza hali ambayo imewakuta akimwambia kwamba ndugu zake wengine wapo Tanzania lakini hajui namna ya kuwapata na wala hakumwambia mume wake kwamba ana watoto wengine.Katika ndoa hiyo imempatia mtoto mmoja.

“Mungu  anafanyakazi kwa njia za ajabu sana, wakati nimeshakata tamaa, mtoto wangu aliniambia kwamba anakuja Tanzania, ameagizwa na kampuni anayifanyia kazi ya Dubai na alinihitaji tuje wote, nimsindikize kwanza nilikataa,” anasema Theresa.

Lakini mtoto wake huyo aliendelea kumbembeleza na mama akakubali. Mama huyo baadaye alimpigia simu rafiki yake anayefanya shughuli Dubai akampatia namba ya simu ya dereva teksi wa Dar es Salaam, Abasi ambaye aliwapokea .

Wakati wanaelekea hotelini Magomeni Mwembechai, Theresa alikuwa anamsimulia dereva huyo shida yake ya kuwa na watoto anaowatafuta kwa miaka mingi na hana uhakika kama ataweza kuwaona. 

Bahati nzuri wakati wanaishi pamoja na mumewe walifanya makazi pia Magomeni karibu na hoteli ya Butiama, walifika hapo kuanza kuuliza maswali na walipomuuliza shemeji yake  Taji Malingumu walielezwa kuwa nyumba iliuzwa zamani na kwamba haijulikani Taji yupo wapi.

Baada ya mazungumzo ya hapo alikubali kwamba basi hawezi tena  kuwaona watoto wake. Lakini dereva Abasi alisema kwamba hajakata tamaa kwani  anaweza kumuunganisha na rafiki yake aliyeko Clouds, Gea ili aone namna atakavyoweza kusaidiwa.

Theresa anabainisha kuwa siku ya Jumanne  Februari 24 alipata nafasi ya kuunganishwa na Gea Habib ndani ya  Leo Tena ya Redio Clouds FM  akahojiwa na kujieleza kwamba  anawatafuta watoto wake ambao wakati akiondoka  aliwaacha wakiwa wadogo sana.Jumatano akaingia katika maelezo yakina.

Kwa mujibu wa mtangazaji kabla ya mama huyo kufika kituoni  hapo tayari alikua ameshaandaa  kipindi cha 'Heka Heka' lakini mara baada ya kumpigia simu mama Theresa aliamua kughairi na kumfanyia kipindi  mama huyo akionesha kuguswa na mazungumzo yake.

Kitendo cha kuelezwa kuwa mama huyo anatafuta watoto wake alionyang'anywa na mumewe na hajui kama wako hai ama kulimfanya amrushe hewani.

Gea anasema kuwa saa tatu baada kufanya kipindi na mama huyo  alipata simu iliyomueleza kwamba yuko mtu anajua watoto walipo.

Watoto hao  Mwanahamisi (Asha ) aliyezaliwa 1974 alisikia kipindi akitajwa baba yake mdogo na kwa kuwa alikuwa anajua kadhia nzima alimweleza mdogo wake fikra zake, yeye na nduguye Hassan aliyezaliwa 1977  walimpigia baba yao ambaye naye alikuwa na habari na baada ya kuambiwa na mpangaji wake kwamba jina lake limetajwa mara kadhaa katika kipindi kinachorushwa na Clouds.

Taji Malingumu akizungumza kwenye simu alisema alifurahishwa sana na taarifa za mtu huyo kiasi ya kwamba alihofia taulo linaweza kumvuka (kwani alikuwa ametoka maliwatoni kuoga), alichosema yeye ni kumtaka huyo mpangaaji wake kupiga simu na kuwaambia watu wa Clouds kwamba mama huyo amsubiri kwani anakuja. Mpangaji alijaribu simu akashindwa lakini akamwandikia Gea meseji.

Theresa alikuwa anamjua shemeji yake japo walipoachana yeye alikuwa chembamba na kujazia mwili wake akiwa mtu mzima, alipigiwa simu na Clouds na kutakiwa kurejea kwenye studio hizo na ingawa alikuwa kariakoo .

Akizungumza katika simu alisema aliangusha kilio baada ya kusikia kwamba watoto wake wamepatikana na kumtaka Abasi asikilize kwani hakuelewa anachoambiwa kutokana na mshtuko alionao. Anasema hajui hata alivyofika Clouds, pale Kawe lakini alipokewa na kupelekwa ghrofani alipoketi kusubiri watoto wake.

“Nilikaa juu hapa ghrofani niliwaona wanavyoingia nilihisi mtoto wa kike atakuwa ni yeye kwani alikuwa mweupe (mwangavu),” anasema mama huyo ambaye alifgichwa nyuma ya mlango shemeji yake alipoingia na kujikuta akiporomosha machozi baada ya kubaini kuwa shemeji yake bado anamkumbuka.

"Nilimkumbuka shemeji  yangu  kwani namkumbuka nilimuona  wakati ule akiwa kijana  na hajabadilika  na yeye haikuwa shida kunikumbuka, sababu nilikua mwembamba sana  ila sasa nimepata huu mwili kwa sababu ya utu uzima ndiyo maana ameweza kunitambua,” anasema mama huyo, akikumbuka jinsi shemeji alivyogeuka na kumuona na kumkimbilia.

Taji akizungumza kwa simu anasema mgogoro mkubwa uliingia katika familia hiyo baada ya kaka yake kuoa mke wa pili.

“Kaka yangu alikuwa askari,  alikuwa na hasira sana hivyo sikushangaa aliponiletea watoto watatu wa kulea. Mtoto mwingine alifariki,” anasema Taji ambaye ameishi muda mwingi na watoto hao.

Theresa  katika mazungumzo yake na Clouds anasema mume wake (sasa marehemu) awali walikua wakiishi  maisha mazuri lakini alikuja kubadilika ghafla  na hapo ndipo alipoona uchungu wa ndoa.

“Yule bwana hakuwa mtu mzuri kabisa mimi niliishi naye kwa kumuogopa wakati huo nikiwa na umri  wa miama 18 na  yeye  miaka 30 alikuwa akiniona nazungumza  na mtu  basi hapo nitapigwa sana huku akiniuliza nilikuwa nazungumza nini na watu walionizidi umri,” anasema.

Mama huyu aliwaomba  msamaha watoto  wake  kwa matukio yote yaliyotokea ambayo siyo makosa  yake  kwa sababu hakupenda  iwe hivyo hana  lawama  yeyote na wao.Anawapa wosia wanawe  kwamba  waishi na watu vizuri wawe na heshima  na wawe ni  watu  wa kusaidia wengine wenye uhitaji.

Anaendelea kusema kuwa hakuwahi kuwa na raha  kila alipokuwa akiwafikiria watoto wake, japo nchini  Kenya ameolewa na amezaa mtoto mmoja wa kike hajawahi kumwambia mume wake huyo  kama aliwahi kuolewa na kuzaa watoto nchini Tanzania na alipoulizwa  kama sasa mume akijua amejibu kuwa hahofii kitu kwani kila  mtu atakufa  na kilicho cha kwake.

“Nawashukuru Watanzania, nashukuru waandishi wa habari, Nashukuru Clouds wamenisaidia sana kuwapata watoto wangu, watoto niliookuwa nawafikiria katika moyo wangu” anasema Theresa na kuongeza kuwa watoto wake ndiyo furaha yake. Mama huyu kwa sasa yupo kwa mwanawe Mwanahamisi ambaye ni msomi wa Chuo kikuu wakizungumza na kucheka.

Kukaa kimya na maumivu ya moyoni bila hata kumweleza mwenzako unayeishi naye ni kazi kubwa, lakini mama huyo wakati anazungumza kwa simu anasema mume wake wa sasa amepokea habari hiyo kwa mshtuko mkubwa. 

Taji Malingumu   anasema haikuwa rahisi kulea watoto hao kwani mke wake wa kwanza hakuwa mtu  mwema hivyo wakaachana na kuoa mke mwingine ili watoto wake wasivurugike .

“ Nilikua naumia kuona kwamba nina watoto ambao wanalelewa na upande mmoja tu wa baba nikamuomba Mungu anisaidie kuwakutanisha na mama yao, hakika Mungu amejibu maombi yangu amefanya amenikutanisha naye.Watoto wake wamemuona mzazi wao”.

“Binafsi siku ya leo sina zaidi ya kusema kuwa namshukuru Mungu kwa kuweza kuwakutanisha watoto wangu pamoja na mama yao ambaye wote hatukufahamu  namna   ya kumpata niliona kama ni miujiza  kwani nilijitahidi kumtafuta shemeji yangu kwa kila  njia  ili aweze kucheza na wanawe  lakini  sikuweza kubahatika,” anasema.

Anaongeza kuwa, “ Mwanahamisi  kuna siku aliniambia anataka kwenda Kiabakari kumtafuta mama yao lakini  katika safari yake hakufanikiwa zaidi ya kukumbana na changamoto mbalimbali na akarudi bila ya mafanikio.”

Taji anasema kuwa changamoto za maisha ya ndoa ya kaka hajayaelewe vizuri kwani kakake hakuwahi kumweka wazi kwa sababu  alikuwa anampenda , anamheshimu na kumuogopa huku akimwagia sifa shemeji yake alikua mama mkarimu nyumbani na alikua akimkirimu sana pindi alipokuwa  akifika kuwatembelea na kumfungashia zawadi  nyingi za matumizi ya nyumbani ikiwa ni pamoja na mafuta ya Super Ghee, sukari, sabuni na vitu mbalimbali.

Hassan aliyezaliwa mwaka 1977 anaeleza kuwa alinyonyeshwa na shangazi yake ambaye alikuja kujua kuwa huyo siyo mama yake alipotimiza umri wa  miaka 14 na  shangazi yake alimkataza na kumwambia kuwa yeye siyo mama aliyemzaa ila yeye ni shangazi.

Alipopewa  nafasi ya kuzungumza Hassan mwenye umri wa miaka 43 mwenye mke na watoto wawili anasema siku ‘mama’ yake aliposema asimuite mama ila amuite shangazi, hakujielewa.

“Nilipolelewa na shangazi baadaye nikachukuliwa na babu  na baadaye nikachukuliwa na babangu (baba mdogo) , nakumbuka nilishawahi kumkwida baba ili anionyeshe alipo mama yetu lakini baba aliniambia mwanangu tuombe Mungu  kwani hakuna kitu kilichokua kikiniuma  hasa pale nikiugua  nauguzwa na mke wangu  tu  nilitamani kupata penzi la mamangu,” anasema hayo kwa uchungu.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e78ab90625577365f852c1fcf8f024af.jpg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Beda Msimbe

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi