loader
JOYCE KALINGA Aanzisha sekondari bila mwalimu, mwanafunzi

JOYCE KALINGA Aanzisha sekondari bila mwalimu, mwanafunzi

“WAKATI nafi ka maeneo haya na namna nilivyopokewa haikuwa rahisi, wananchi wa kawaida walinishangaa na kunibeza kwa lugha mbalimbali za kejeli.

Walisema maneno mengi wakihoji inawezekanaje mwanamke nikaongoza watoto wao na kuwa mkuu wa shule; kwao, waliona hicho ni kitu ambacho hakiwezekani kabisa, lakini Mungu alinisaidia na mimi kujitoa kwa hali na mali; kwa juhudi na maarifa hadi nikashinda maneno na imani zao; nikawaonesha kuwa, kuwa mwanamke si kikwazo cha kuongoza au kufanya jambo jema katika jamii,” ndivyo anavyosema Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mkalala iliyopo katika Kata ya Mninga, mkoani Iringa Joyce Kalinga. Joyce mzaliwa wa Kijiji cha Ifwagi katika mazungumzo na HabariLEO, Kijijini Mninga anasema mtazamo wa jamii katika eneo hilo ulikuwa kwamba mwanamke hawezi kuwa kiongozi wa jamii na haweza kuongoza taasisi yenye watumishi wengi wakafanikiwa na kupiga hatua za kimaendeleo.

Anasema ndoto zake kuu zilikuwa kumkomboa mtoto wa kike dhidi ya ukandamizwaji, unyanyaswaji na hasa dhidi ya kubaliwa kwa mtoto wa kike katika katika nyanja za elimu kukataa mila potofu, baguzi na kandamnizi dhjidi ya mtoto wa kike kijijini Ifwagi.

“Nilianzisha mwenyewe Shule ya Sekondari Mkalala, sikukuta mwalimu wala mwanafunzi, bali majengo na samani za kukalia wanafunzi na samani za walimu… kwa msingi huo, ilinibidi nianze mwenyewe kwa kusajili wanafunzi nyumba kwa nyumba kama mwalimu na pia kama mkuu wa shule, lakini niliweza kupambana mpaka serikali ikaajiri walimu miezi tisa baadaye,” anasema.

Kwa juhudi za Mwalimu Joyce mwaka 2008, Shule ya Sekondari ya Mkalala ikaanza na kidato cha kwanza. “Wakati huo, mwalimu Joyce alikuwa anafundisha wanafunzi hao masomo yote pekee yake, bila usaidizi wa mtu yeyote,” anasema mwakajijiji mmoja ilipo shule hiyo anayekataa kuandikwa gazetini.

Joyce mwenyewe anasema, “ licha ya ugumu niliokumbana nao, nilifanikiwa kuwasaidia na kuwapa msingi na mwelekeo ili waweze kusoma, mpaka serikali ilivyoleta walimu… hadi sasa shule hii chini ya uongozi wangu wa miaka 12 kama Mkuu wa Shule, ina walimu 17 wanafundisha masomo mbalimbali kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.”

“Nafurahi kuwa kila mwaka, shule yangu inapanda kwa kupeleka watoto kidato cha tano hasa katika masomo ya sayansi na nimekuwa nikihamasisha watoto wa kike kuchukua mchepuo wa sayansi kulingana na kizazi tulicho nacho sasa na pia, kuwahamasisha watoto wa kike kupenda kusoma, kwa sababu ukombozi wa mwanamke ni elimu… mwanamke ukipata elimu, unakuwa na uwezo mkubwa kutatua changamoto mbalimbali zinazokukabili wewe, zinazomkabili mtoto na zinazoikabili familia, jamii na taifa kwa jumla,” anasema.

Mwalimu Joyce amekuwa karibu sana na wanafunzi wake wa kike, kutokana changamoto wanazozipitia kijijini hapo, zikiwemo mila kandamizi dhidi ya mtoto wa kike. Kupitia mila kandamizi hizo, baadhi ya wanajamii kimakosa wanaamini kuwa, mtoto wa kike hastahili kupata elimu, bali kubaki nyumbani akisaidia kazi mbalimbai huku akisubiri kuolewa.

“Nimekuwa nikisimama mwenyewe kama mfano ili wanafunzi wangu wanitazame mimi niliyesoma kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari Mdabulo kijijini Ifwagi na nikafaulu kwenda shule ya sekondari Kilakala, mkoani Morogoro kumalizia kidato cha tano na cha sita na kwenda kusomea ualimu katika Chuo cha Ualimu mkoani Morogoro. Niliajiriwa kama mwalimu wa kawaida hadi kuteuliwa kuwa mkuu wa shule, licha ya vita kali nilizokutana nazo na kuzikabili, nilijua nipo msituni na lazima niibuke kuwa shujaa,” anasema.

Akitolea mfano wa aliyekuwa Makamu wa Rais na sasa ndiye Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Joyce anasema kiongozi huyo mwanamke wa kwanza kuwa rais Tanzania na katika historia ya nchi za Afrika, amekuwa hamasa kwa wanafunzi wake wanaoamini ipo siku nao watakuwa viongozi.

“Kwa sasa nao wanajua kuwa ili kufikia hatua hiyo, wanahitaji kupata elimu bora ili iwasaidie kufanya wanachotaka kufanya na kwamba wao wenyewe wanapaswa kuweka juhudi na nidhamu katika masomo na maisha yao,” alisema.

Katika mikutano ya walimu na wazazi, Joyce anasema amekuwa akielimisha wazazi kuhusu mahitaji maalumu ya mtoto wa kike na kwamba yanatakiwa kutatuliwa na wanahitaji kupewa msaada zaidi ili wazidi kusonga mbele. Mzazi anaposhindwa kumtatulia changamoto mtoto wa kike kama ‘zana za kila mwezi, yeye(Joyce) huhakikisha kuwa zinapatikana kwa uraisi shuleni hapo ili wanafunzi hao wa kike wasikose masomo.

Katika maadhimisho ya kuelekea Siku ya Mwanamke Duniani yaliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake (UN Women) pamoja na kampuni ya Chai Unilever, yaliyofanyika kijijini Mninga, Kata ya Mninga mkoani Iringa, mchango wa wanawake mbalimbali akiwamo Mwalimu Joyce katika maeneo mbalimbali. Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri William, aliyewapongeza wanawake kwa juhudi zao kupambana na umasikini kwa kupiga hatua na kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kijijini hapo kwa kujiamini kwani wanaweza.

“Nawapongeza wanawake kwa uthubutu mliouonesha kupinga mila potofu na kuwapeleka watoto wa kike shuleni ili nao wapate elimu, kwa kuwa serikali yetu imetoa fursa kwa Watanzania wote kupata elimu bila malipo na wanawake mmechangamkia vizuri fursa hiyo kwa kuwapeleka watoto wenu wa kike shuleni ili wapate haki ya elimu,” alisema Mkuu wa Wilaya, William.

Alisema amefurahishwa na wanawake wengi waliopita katika uchaguzi mkuu uliopita na kuongeza kuwa, wengi wamepata nafasi za uongozi kutokana na juhudi zao katika kutenda kazi.

Joyce (sasa ni mwalimu) kutoka katika familia masikini, alichaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Tunduru mkoani Ruvuma.Kutokana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa mkoani humo kutokuwa rafiki kwake, alirudi kijijini hapo na kumpumzika kwa ajili ya matibabu nyumbani kwa muda wa miaka minne.

Alipopona, Joyce aliomba kurudishwa shule ili atimize ndoto zake. Akajiunga na Shule ya Sekondari Mdabulo, wilayani Mufindi, mkoani Iringa na alianza tena masomo ya kidato cha kwanza upya wakati wenzake aliosoma nao wakiwa kidato cha tano.

“Safari yangu ya kuwa mwalimu haikuwa rahisi, kwa sababu nilivyochaguliwa kwenda chuoni, sababu ya kukosa karo, haikunikatisha tamaa, mimi sikwenda nyumbani wakati wa likizo kama wenzangu, bali nilikuwa nabaki chuoni na kufanya kazi mbalimbali za mikono kama vile kusafisha mazingira chuoni hapo, kufyeka nyasi, kusafisha vyombo jikoni, na kuhudumia wageni kutoka baraza la mitihani waliokuwa wanakuja kufanya kazi maalum ili niweze kupata ada na fedha za matumizi yangu binafsi,” anasema.

Joyce anawahimiza watoto wa kike pamoja na wanawake kwa jumla wasikate tamaa katika kutimiza malengo yao. Kwa sasa Joyce amekuwa mwanamke wa kuigwa kijijini Mninga, akiwa mstari wa mbele kupinga mila kandamizi dhidi ya mtoto wa kike.

Katika maisha yake, amepambana na vita vikali dhidi ya wanaume ambao mwanzoni wengi hawakukubaliana naye wakitaka kumuondoa kijijini hapo kwa madai kuwa, anawaharibia mabinti zao.

Miaka 12 baadaye, wanaume hao wanampongeza kwa jitihada zake kuhakikisha watoto wao wa kike wanashinda shuleni na kuepuka vishawishi mbalimbali ambavyo vimekuwa chanzo cha mimba za utotoni.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/d04fe7b69eabbf39918d75985049cbf5.jpg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi