loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Janeth Magufuli: Asante Maria Nyerere, nakupenda

MJANE wa aliyekuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, John Magufuli, Janeth Magufuli amemshukuru mjane wa Baba wa Taifa, Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere kwa zawadi ya ng’ombe aliyompa na kumhakikishia kuwa anampenda.

Mwishoni mwa wiki Janeth pia alieleza kufarijika kwa kutembelewa na familia ya Baba wa Taifa na akawashukuru Watanzania kwa maombi, sala, na dua kuomboleza kifo cha Rais Magufuli.

Hayati Rais Magufuli alifariki dunia Machi 17, mwaka huu kutokana na tatilzo la mfumo wa umeme wa moyo. Alizikwa Machi 26, mwaka huu kijijini kwake, Chato katika Mkoa wa Geita.

Katika safari hiyo Mama Maria Nyerere aliwapa salamu wamfikishie Mama Janeth Magufuli kuwa, anamtakia heri, nguvu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu.

Janeth alimshukuru Mama Maria kwa kumpa heshima na anatambua kuwa anaipenda familia ya Rais Magufuli, anampenda yeye na anampenda mumewe, Hayati Rais Magufuli.

"Msalimieni sana Mama Maria Nyerere, mfikishieni salamu, mwambieni nampenda, ni mama yangu, tuko pamoja. Asante kwa zawadi nzuri aliyonipa, amenipa heshima kubwa mama huyu na siku zote ana upendo na familia yangu, mimi mwenyewe na marehemu mume wangu, Mungu ambariki sana na nyie mliokuja Mungu awabariki," alisema.

Familia ya Baba wa Taifa, ilikwenda nyumbani kwa Rais Magufuli, Chato kutoa salamu za rambirambi kwa mjane wa Rais Magufuli, Mama Janeth Magufuli.

Katika safari hiyo, familia ya Nyerere kutoka Kabila la Wazanaki katika ukoo wa Borito, ilimkabidhi mjane huyo ng'ombe dume.

Msemaji wa familia hiyo, Chifu Japhet Wanzangi, alisema pamoja na kufika kumfariji mjane wa marehemu, mila na desturi za kabila hilo zinaelekeza watoe ng'ombe dume unapotokea msiba sehemu za watawala.

"Tumekuja kuwakilisha salamu za ukoo, tunashukuru kwamba baada ya mazishi, tumeweza kupata nafasi kufika nyumbani kuonana na mjane Mama Janeth na familia kwa tukio hili la kuhani msiba," alisema Chifu Wanzagi.

Alisema Rais Magufuli atakumbukwa kwa kuwa alifanya kazi nzuri na kubwa katika taifa na kwamba, kwa mujibu wa Neno la Mungu, kuwakumbuka wenye haki ni baraka.

Katika safari hiyo, Chifu Wanzangi alifuatana na wanafamilia wenzake akiwemo Daisy Nyerere, Neema Nyerere, Nashom Jirabi na Madaraka Nyerere.

foto
Mwandishi: Yohana Shida, Geita 

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi