loader
Dstv Habarileo  Mobile
Uyoga asili unavyonyanyua wanakijiji kiuchumi

Uyoga asili unavyonyanyua wanakijiji kiuchumi

UYOGA kwa mujibu wa watalaamu ni aina ya kuvu (fungus) na sio jamii ya mimea. Watafiti pia wanasema uyoga umejaaliwa kuwa na protini nyingi kuzidi nyama.
Zipo aina takribani 45 za uyoga hapa Tanzania, ukiwemo unaoliwa na binadamu na usioliwa na binadamu.  
Jamii ya Uyoga iko katika makundi mawili madogo ya jamii ya Basidiomycota na Ascomycota katika familia kubwa ya fangasi. 
Kutokana na kukosa chembechembe za kijani, uyoga hauwezi kujitengenezea chakula chake bali huchukua virutubisho kutoka katika vyanzo vingine vya nje vinavyozunguka maeneo yake. 
Kwa kawaida uyoga hujiotea porini, kwenye magome yaliooza au kwenye takataka za aina mbalimbali.
Kuna aina kuu tatu za uyoga ambazo zinaweza kuzalishwa na mkulima mdogo ambazo ni Mamama (Oyster Mushroom), Shiitake na Ganoderma.
Uyoga unampatia mlaji vitamini B, C, D, madini ya joto, fosforas, chuma na potasium. Pia uyoga unatajwa kuwa ni tiba asili, mbolea na huweza pia kutumiwa kama chakula cha mifugo. Uyoga unatibu maradhi ya kifua kikuu, kisukari, moyo, shinikizo la damu na figo.
Kutokana na fursa ambazo zinapatikana kupitia uyoga zimekuwepo juhudi mbalimbali za wadau kuwezesha jamii ya vijiji kunufaika na zao hilo.
Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao Misitu (FORVAC), inayotekelezwa na Idara ya Misitu na Nyuki na kufadhiliwa na Serikali ya Tanzania na Finland wameona jitihada za wanakijiji cha Amani Makoro ambao wanachuma uyoga wa asili na kujipatia kipato.
Kijiji cha Amani Makoro kipo kata ya Amani Makoro wilayani Mbinga mkoani Ruvuma ambapo akina mama watatu wa kijiji hicho, Hilda Komba, Veronica Sakwaya na Germana Mapunda wanatumia fursa ya uwepo Msitu wa Naghweve kuchuma uyoga wa asili na kujiingizia kipato.
Akizungumza na gazeti hili, Mchuma Uyoga Komba, anasema FORVAC ni mkombozi wa maisha yake kwani ameachana na utegemezi.
Anasema pia kupitia uyoga amekuwa akinunua mahitaji mengine kama mbolea ya kuweka kwenye mahindi yake.
Mchuma uyoga huyo anasema wamekuwa wakichuma uyoga wa asili kwa msimu hasa kuanzia mwezi Desemba hadi Aprili hivyo wanaomba FORVAC kuwawezesha ili waanzishe shamba la uyoga.
"FORVAC wamekuja kutuamsha na tumeamka, ninaahidi kuwa nitajitahidi kufikia malengo yangu," anasema.
Anatoa wito kwa akinamama wenzake kutumia fursa ya ujio wa FORVAC kijijini kwao kujikomboa kiuchumi, maendeleo na kijamii.
Anasema changamoto ambayo wanakabiliana nayo ni kukutana na nyoka na wadudu hatari ambao wanatumia uyoga kama chakula.
Naye Sakwaya anasema uchumaji uyoga unamuwezesha kuipatia familia yake mahitaji muhimu kama ya shule, afya na huduma nyingine muhimu.
Sakwaya anasema ipo changamoto ya vitendea kazi hivyo wakipata kasi ya uchumaji uyoga itaongezeka.
"Uyoga unalipa, hili halipingiki kwani sisi watatu maisha yetu yanategemea uyoga pamoja na ukweli kuwa tunajihusisha na shughuli nyingine za kilimo," anasema.
Anasema awali walikuwa wakichuma kama mboga ila kwa sasa ni biashara ya uhakika inayowasaidia kuendesha maisha yao.
Kwa upande wake Mapunda anasema naye amepata mafanikio kwa kuhudumia familia yake na msingi mkubwa ni uchumaji uyoga kwenye misitu wa asili wa kijiji.
"Awali msitu wetu wa Naghweve ulikuwa unatumika kwa uvunaji haramu lakini baada kugundua fursa zilizopo ikiwemo ya uyoga tukaamua kuwekeza kwa kuulinda na kuvuna kibiashara na faida zimepatikana," anasema.
Anasema katika msitu wao kuna aina uyoga wa aina mbalimbali kama Uwinda, Mkolombi na mingine.
Mapunda anasema uyoga umemuinua kiuchumi na kumpa uhakika wa kupeleka watoto wake shule bila kuomba msaada.
Anasema msitu una fursa nyingi ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuinua wakina mama vijijini kiuchumi na kwamba changamoto kubwa wanayokutana nayo ni kukosa vifaa vya kisasa vya kuchumia na kuandaa uyoga.
Mapunda anasema pia ana mizinga ya asali zaidi 20 ambapo siku chache zijazo anatarajia kurina asali hivyo kujiongezea kipato zaidi.
Anasema mikakati yao ni kuhakikisha wanafika mbali kupitia biashara ya uyoga kwa kuuza hadi nje ya nchi kwa kuwa bidhaa zao ni nzuri.
Mtaribu wa FORVAC Kongani ya Ruvuma, Marcel Mutunda anasema programu hiyo katika wilaya ya Mbinga inafanya kazi na idara mbalimbali kama Idara ya Misitu, Ardhi, Mangira, Maendeleo ya Jamii na wilaya kwa ujumla.
Pia Wakala Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ni wadau muhimu katika utekelezaji wa programu.
Mutunda anasema programu hiyo wilayani Mbinga inafanya kazi na vikundi na watu binafsi takribani 20 ambao wanajihusisha na mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu kama mbao, kurina asali, kuchuma uyoga, kusuka vikapu, nyungo na vingine vinavyotokana na mianzi.
Anasema pamoja na Amani Makoro pia vikundi vingine vinatoka vijiji vya Ukata, Ndongosi, Barabara, Kindimba Juu, Kiwombi na Kindimba Chini.
Mratibu huyo anasema katika eneo la uchumaji wa uyoga akina mama hao watatu wameonesha mfano mzuri hivyo FORVAC imeamua kuwasaidia kwa kuwapatia vifaa ambavyo vitasaidia shughuli zao za uchumaji uyoga asili.
"Hapa Amani Makoro kuna akina mama watatu Hilda, Veronica na Germana ambao wamejikita kuchuma uyoga FORVAC itawapatia vifaa vya kuchakata ili kuongeza thamani kwenye bidhaa hiyo.
“Katika shilingi milioni 100 ambayo imetolewa Mbinga akina mama hawa watapata vitendea kazi kama buti, nguo na vingine vingi,” anasema.
Anasema uyoga una protini nyingi kuliko nyama hivyo anashauri Watanzania hasa akina mama ambao wanaishi karibu na misitu watumie fursa hiyo ili kujikwamua kimaisha.
Anasema FORVAC imedhamiria kuongoza mnyororo wa thamani wilayani Mbinga hivyo kuwataka wanavijiji wenye misitu asili kutumia fursa hiyo ili kunufaika na misitu yao.
Anasema pia mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu katika Kongani ya Ruvuma inahusu wilaya za Nyasa, Songea, Namtumbo na Tunduru.
"Misitu ikitumiwa kwa njia endelevu ni fursa ya kiuchumi na maendeleo hivyo programu hii ambayo ni ya miaka minne imetoa matunda na tunaamini itakuwa endelevu hata ikiisha," anasema.
Ofisa Misitu Wilaya ya Mbinga, Halifa Singano anasema uyoga ni bidhaa muhimu sana na inapatikana kwa wingi katika Kijiji cha Amani Makoro hivyo ujio wa FORVAC umefungua fursa kwa wanakijiji.
Singano anasema uyoga unaotoka kijijini hapo ni mzuri na ndio maana anawaomba wafanyabiashara kujitokeza kuununua.
"Mwitikio wa wanakijiji kuchuma uyoga bado ni mdogo ila tunaendelea kutoa elimu ili fursa hii iweze kutumika kuinua maisha ya wananchi wengi zaidi," anasema.
Singano anasema FORVAC imewezesha uhifadhi, utunzaji wa mazingira, ungozeko la kipato na kila mwananchi kuwa mlinzi wa msitu kwa kuwa wananufaika na rasilimali zao.
Anasema katika vijiji ambavyo vina programu ya FORVAC inafanyika, wao kama Serikali wamepunguza nguvu ya ulinzi kwa kuwa wana vijiji wamekuwa sehemu ya ulinzi wa misitu yao.
Ofisa misitu huyo anasema matokeo chanya ambayo yanapatikana kupitia FORVAC wanayatumia kusambaza kwa vijiji vingine kwa kutumia asilimia 10 inayotengwa na halmashauri kwa vijana, wakinamama na watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake, Mtendaji Kata ya Amani Makoro, Joachim Kaponda anasema shughuli za uchumaji uyoga zimechochea maendeleo hivyo wanaendelea kutoa elimu ili kila mwanakijiji kutambua fursa hiyo.
"Kata yangu ina vikundi vinne jambo ambalo linanipa faraja sana katika majukumu yangu kwa kuwa nafanya kazi na watu wenye shughuli maalum," anasema.
Kaponda anasema wao kama kata wanashirikiana na akina mama ambao wanajihusisha na kuchuma uyoga ili kuhakikisha wanapata mafanikio.
Diwani wa kata hiyo, Ambrose Nchimbi, anasema shughuli za uchumaji uyoga zimekuwa na mchango mkubwa kwenye kuitangaza kata na kijiji.
Anasema watu wengi wamekuwa wakiulizia Amani Makoro pamoja na kuwepo bidhaa nyingine ila uyoga wa asili ni kivutio kikubwa.

**Mwandishi ni mchangiaji wa gazeti hili.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/21a3745a4a68f47302568405dce62af0.jpg

HISA milioni 15 zenye thamani ya shilingi ...

foto
Mwandishi: Suleiman Msuya

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi