loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Mazingira ni mazuri Z’bar mwanamke kupata uongozi’

“SINA kikwazo wala sababu za kuwanyima fursa za uongozi wanawake, cha msingi ni kuwa na sifa zinazotakiwa. Katika kipindi changu cha uongozi sitofanya ubaguzi wa aina hiyo katika uteuzi wa nafasi mbalimbali.”

Hiyo ni kauli ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi ambayo amekuwa akiitoa kwa nyakati tofauti hususani anapokutana na makundi ya wanaharakati. 

Kauli hiyo inaungwa mkono na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Zena Ahmed Said, anayesema hakuna vikwazo kwa wanawake kugombea nafasi za uongozi zikiwemo za kisiasa.

Ni kwa msingi huo anazitaka asasi za kiraia kuzipitia sheria zote ambazo zinaonekana kukwamisha juhudi hizo na kuziweka wazi ili zifanyiwe kazi.

Zena alikuwa akizungumza katika uzinduzi wa kitabu cha muongozo wa ushiriki wa wanawake kwenye uongozi na siasa kilichotayarishwa na asasi za kiraia ikiwemo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Zanzibar pamoja na Chama cha Wanasheria Wanawake (Zafela).

Anasema Dk Hussein Ali Mwinyi ameahidi na kusisitiza kwamba ataweka mazingira mazuri kwa wanawake kushiriki katika uongozi na harakati za kisiasa.

Anasema malengo hayo yamefikiwa kwa kuwepo uteuzi wa nafasi za wanawake katika uongozi ikiwemo mawaziri, makatibu wakuu na wakuu wa mikoa pamoja na wilaya.

''Serikali ya awamu ya nane chini ya Rais Dk Hussein Ali Mwinyi imedhamiria kuhakikisha kwamba wanawake wanafikia malengo ya kisiasa kwa kushika nafasi mbalimbali za juu za uongozi bila ya ubaguzi,'' anasema.

Anazitaka asasi za kiraia zinazojishughulisha na mapambano ya kuona wanawake wengi wanashika nafasi za uongozi kuhakikisha zinasaidia kutoa elimu ambayo ndiyo kigezo kikubwa cha kuteuliwa au kuchaguliwa kwenye uongozi.

''Miongoni mwa kigezo kikubwa cha wanawake kushika nafasi ya uongozi ni elimu... Asasi zinazojikita katika kutoa elimu zisaidie mapambano ya kuwapatia walimu watoto wa kike ili wapambane kikamilifu na wanaume,'' anasema.

Anasema bado vipo vikwazo ambavyo ni changamoto kwa wanawake kufikia malengo ya uongozi, moja wapo ikiwa ni hofu walizonazo wanaume dhidi ya wanawake.

Zena anaitaka jamii kuachana na hulka na dhana kwamba mwanamke hawezi uongozi na anapopewa nafasi hiyo ni kama upendeleo au zawadi kutoka kwa aliyempa wadhifa huo.

''Jamii imekuwa na fikra potofu kuwa mwanamke anapoteuliwa nafasi ya kuwa kiongozi basi atakuwa ana mahusiano na mteuaji au ni zawadi, hapana si kweli. Wanawake wanao uwezo na wanachaguliwa kwa vigezo vya uwezo wao,'' anasema.

Kabla ya kushika wadhifa hao Zena alikuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aliwahi pia kuwa katibu tawala mkoa wa Tanga.

Akichangia muongozo wa kitabu hicho kwa washiriki pamoja na kutoa uzoefu wake kufuatia nyadhifa mbalimbali alizopitia, Zena anawataka watendaji mbalimbali waliopo katika ngazi za maamuzi na uteuzi kutenda haki na pale wanapokuwa na fursa za kuteua nafasi za uongozi wafanye hivyo bila kuwabagua wanawake kama wanakidhi vigezo kwa sababu uwezo wa kuongoza wanao.

Anaitaka jamii kubadilika na kuamini kwamba mwanamke anao uwezo mkubwa wa kuongoza na uteuzi wanaoupata sio sehemu ya upendeleo au mahusiano na wateule.

Anasema baadhi ya watu wamekuwa pia na mtazamo hasi kuhusu wanawake kubeba uja uzito kwamba akiwa na hali hiyo atashindwa kutekeleza na kusimamia majukumu yake aliyokabidhiwa.

''Hizi mimba tusipozibeba kizazi kitapatikana wapi? Haya ni maumbile yetu ambayo tumejaaliwa na Mwenyezi Mungu na kamwe sio kigezo hata kidogo cha kudharau uwezo wa mwanamke katika uongozi,'' anasema.

Anawataka wanawake kujiendeleza kielimu zaidi na kila mwenye uwezo kugombea nafasi za uongozi hususani kuhakikisha wanakuwemo katika vyombo vya maamuzi na kutunga sheria.

''Moja ya kigezo ambacho humuengua mwanamke katika uongozi ni elimu... Wakati umefika kwa asasi za kiraia kuwapatia fursa za elimu na mafunzo wasichana na wanawake,'' anasema.

Aidha Zena anawataka wanaume wasiogope na kuingiwa na hofu kwamba mwanamke akipata nafasi ya uongozi ni hatua nyengine ya kuwadharau au kuwaona hawana maana.

''Ipo hofu kwa wanaume kwamba mwanamke akipata nafasi ni hatua moja ya kumtelekeza mume wake na kutafuta mwanamume anayelingana na hadhi yake. Hapana mimi nipo katika ndoa zaidi ya miaka 29 na licha ya kupanda ngazi mbalimbali sijamtelekeza wala kumdharau mume wangu,'' anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake (Zafela), Jamila Mahmoud anasema lengo la mradi wa miaka minne wa wanawake na uongozini ni kuwajengea msingi mzuri utakaowawezesha wanawake kuingia kwenye uongozi.

Anasema wakati umefika sasa kwa wanawake kugombea nafasi za uongozi katika majimbo ya uchaguzi na kwamba wapo wanawake waliofanya hivyo na kufaulu na wanaongoza vizuri.

Anasema mradi wa wanawake na uongozi unafadhiliwa na Serikali ya Norway na kwamba lengo lake kubwa ni kujengea uwezo kwa wanawake kutoogopa kuingia kwenye siasa na uongozi wa nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini, Pemba, Salama Mbarouk Khatib, anawataka wanawake wajitokeze kugombea nafasi za uongozi na kamwe wasikate au kukatishwa tamaa kwani mazingira ya kushiriki katika siasa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni mazuri.

''Wanawake wenzangu nawaomba mjitokeze kugombea nafasi za uongozi kila zikitokea, iwe katika majimbo ya uchaguzi au kwingineko. Hakuna vikwazo vitakavyowakwamisha kutekeleza dhamira hiyo,'' anasema.

 

Mwakilishi wa kuteuliwa na Rais ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Sada Mkuya anasema vipo vigezo ambavyo hutumiwa kujaribu kuwaengua wanawake hata kama wana sifa za uongozi ambavyo anasema kwa sasa vimepitwa na wakati ikiwemo kubeba uja uzito.

''Nilipokuwa Waziri wa Fedha na Uchumi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nilisoma bajeti ya Serikali katika Bunge kwa muda wa zaidi ya saa mbili nikiwa nimesimama. Ni watu wachache sana waliofahamu kwamba nilikuwa na ujauzito wa miezi minane,'' anasema Mkuya.

Naye Mkurugenzi wa Tamwa-Zanzibar, Dk Mzuri Issa anasema wakati umefika kwa vyama vya siasa kurekebisha sera na mifumo ya uchaguzi ili kutoa nafasi zaidi kwa wanawake kupenya na kuingia katika mchakato wa uchaguzi.

''Mifumo ya uchaguzi katika vyama vya siasa mingi sio rafiki na haitoi nafasi kwa wanawake kupenya na kugombea nafasi katika majimbo ya uchaguzi,'' anasema.

Zubeda Khamis Shaibu, Mbunge wa jimbo la Mfenesini kwa tiketi ya chama cha Mapinduzi anawahimiza wanawake wasikate tamaa licha ya mfumo uliopo katika maeneo mengi kutoa nafasi zaidi kwa wanaume kugombea nafasi za uongozi katika majimbo ya uchaguzi.

''Niligombea Ubunge mwaka 2015 katika jimbo la Mfenesini na kushindwa... Lakini nilisema sijakata tamaa na nilijitosa tena mwaka 2020 na kuibuka na ushindi mnono na sasa nipo katika mikakati ya kutekeleza ilani na kuwatumikia wapiga kura wangu,'' anasema.

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi