loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mpango aanza na vigogo 3

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amemwagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kupandisha makusanyo ya kodi hadi Sh trilioni mbili kwa mwezi na kupatia ufumbuzi changamoto za mgawanyo wa mapato kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Kwa sasa, Zanzibar inapata asilimia 4.5 ya mapato yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kikokotoo hicho kilitokana na ushauri wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na kupitishwa na serikali mwaka 1994.

Akizungumza baada ya kuapishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga, mawaziri wanane na naibu mawaziri wanane katika Ikulu ya Chamwino mkoani hapa jana, Makamu wa Rais alisema inawezekana kuongeza makusanyo ya kodi Sh trilioni mbili kwa mwezi kama wakijipanga.

“Sijaomba ridhaa kwako Rais (Samia) lakini ningependa kabla ya mwisho wa mwaka huu tufikie trilioni mbili kwa mwezi, inawezekana tukajipange vizuri,” alisema Dk Mpango ambaye kabla ya uteuzi wake mapema wiki hii alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango tangu Novemba mwaka 2015.

Pia alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu asimamie maduhuli na matumizi katika wizara bila kupepesa macho.

Alisema kama ataona mapato hayaongezeki atarudi kwa Rais kulalamika kwamba huyo hafai katika kuendana na kasi yake.

Dk Mpango alisema wananchi wamepata matumaini makubwa kwa Rais Samia ameikamata nchi vizuri kwa kipindi kifupi hivyo wizara zote lazima kusimamia mapato.

Alisema Dk Mwigulu anatakiwa kwenda kusimamia upande wa kodi kwani mapato kutoka taasisi hasa mashirika ya umma bado ni madogo.

Dk Mpango alisema hivi sasa amepata mrithi Dk Mwigulu akataka ikawe kazi ya kwanza akisaidiana na Naibu Waziri Hamad Yussuf Masauni na timu nzima pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo kuhakikisha wanatatua tatizo la uhusiano wa kifedha haraka.

Alisema atasimamia kwa nguzu zake zote kuhakikisha changamoto hiyo ya mapato ya Zanzibar inapatiwa ufumbuzi.

Dk Mpango alikumbusha namna Rais Samia alivyokemea mawaziri na naibu mawaziri kuvutana. Akawataka mawaziri  kuwapa kazi naibu mawaziri, wanatakiwa kujenga nyumba moja hakuna sababu ya kuvutana na kugombana.

Hivyo alimtaka Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Kattanga akasimamie kuhakikisha mvutano miongoni mwa makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu ambao wamekuwa wakivutana.

“Wapo baadhi makatibu wakuu ambao manaibu makatibu wakuu wakifanya vizuri, inakuwa shida hasa wanapojaribu kuweka sauti zao kwa upande kuweka taratibu za pesa taratibu zifuatwe, inakuwa nongwa,” alisema.

Akamwagiza Katibu Mkuu atakapokaa na makatibu wakuu awaambie kwamba waache mivutano hiyo na wajue kwamba wanafuatiliwa na wakaopuuza watachukuliwa hatua.

Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai amewataka mawaziri na naibu mawaziri kuchapa kazi kwa kufuata utaratibu, maadili na uadilifu kwani “Rais Samia hatabiriki, hata leo hatujui kama tutatoka salama.”

Alisema Katibu Mkuu Kiongozi ni mfano kwa watumishi wengine kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na nidhamu kwani wanaweza kufuata nyayo zake na kuwa mbali katika utumishi wa umma kwa kufanya kazi vizuri.

Balozi Kattanga amesema kwamba wizara na taasisi mbalimbali zina wajibu wa kushirikiana katika kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya 2025.

Alisema wao kama wizara wanatakiwa kuleta ufanisi katika utekelezaji wa kazi na kitaaluma, kufika kwenye Dira ya 2025, lazima iwe serikali inayofanya kazi pamoja.

Alisema wajibu wake ni kuunganisha wizara kwani serikali kwa umuhimu wake inakatwa vipande vipande, wizara na taasisi zake. Alisema katika kupata mafanikio, matokeo ya wizara moja ni nyenzo katika wizara nyingine ili kupata matokeo katika wizara nyingine.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alimhakikishia Rais Samia kwamba yupo tayari kupokea maelekezo na kuwatumikia Watanzania kama inavyoelekeza na kama Ilani ya CCM 2020-2025 ilivyoelekeza.

Alisema atachapa kazi ili kuwaondolewa mashaka Watanzania kwa kushirikiana na Rais ambaye ni Amirijeshi Mkuu. Kila sekta inayoguswa wananchi watahakikisha inafanyiwa kazi ili kufikia malengo yao na matumaini yao yanafikiwa.

Naye Jaji Mkuu Ibrahim Juma amewapongeza wateule wote na akamtaka Waziri wa Fedha na Mipango ambaye anaijua Mahakama kuwasaidia kupata fedha kwa ajili ya kukamilisha majengo ili wahamie Dodoma.

foto
Mwandishi: Maulid Ahmed na Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi