loader
FRANK AYUBU Ofisa wa Polisi aliyeweka hadharani kadhia ya kustaafu askari

FRANK AYUBU Ofisa wa Polisi aliyeweka hadharani kadhia ya kustaafu askari

HUENDA wewe ni miongoni mwa watu unaowaonea huruma sana wastaafu wa majeshi hasa jeshi la Polisi ambao wakirudi uraiani wanapata taabu sana kisaikolojia na hata kimaisha.

Kutokana na dhiki hiyo ungetamani wastaafu hawa kuwa na elimu ya pekee kuhusu maisha yao.

Tamaa hiyo ndio imemfanya Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi (ASP), Frank Ayubu kutengeneza kitabu kinachomwandaa askari polisi kustaafu, alichokiita Maandalizi Bora ya kustaafu kwa askari polisi.

ASP Frank ambaye pia ni mhadhiri(mkufunzi ) katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini mkoani Dar es Salaam anasema hiki si kitabu chake cha kwanza ingawa ana vitabu vingi ambavyo vinaangalia saikolojia ya kuwa na maisha yenye ustawi na ya usalama zaidi.

“Mimi ni askari, nikaguswa na maisha ya askari wenzangu wanayokutana nayo wanapostaafu hivyo nikaandika kitabu hiki ambacho kina kurasa 105,” anasema ASP Frank ambaye ana Shahada ya Uzamivu katika Afya ya Jamii (Community Health Nursing).

Anasema imemchukua takribani mwaka mmoja kuandika kitabu hicho na anatarajia kitakwenda kuwa msaada mkubwa kwa askari wanaotarajia kustaafu hapa nchini.

Katika mahojiano ASP Frank anasema kumekuwa na watumishi wa jeshi hilo ambao wamejikuta katika matatizo makubwa kutokana na kutojiandaa kwa maisha bila mshahara.

Kitabu hiki kinachoelezea maandalizi bora ya kustaafu kwa askari Polisi kikiwa na sura 11 na kurasa 105 zenye maandishi yanayosomeka vyema, mifano na uchambuzi wa kina wa maisha ya askari, anasema ameandika kupunguza pengo la mahitaji ya maandiko stahiki kwa ajili ya wastaafu wenye dhamana maalumu kama polisi.

Ukisoma kitabu katibu hiki unagundua kwamba fedha nyingi pekee haitoshi kuwa kigezo cha maisha bora baada ya kustaafu kwani wengi wa wastaafu wamekuwa katika matatizo makubwa pamoja na fedha walizopewa.

Kwa mtu ambaye ameona changamoto nyingi kama Frank, maandiko yake yanaweza kuwa dawa ya kukabiliana na changamoto hizo ili kufanya maisha ya wastaafu kuwa katika maisha yenye ustawi wa aina yake.

“Katika ulimwengu wa sasa maisha ya kustaafu yamekuwa na changamoto nyingi si kwa askari polisi pekee bali ni kwa watumishi kutoka idara mbalimbali za serikali na hata zisizo za kiserikali. Askari wengi wamekosa elimu hii kwa uzoefu wangu ndani ya Jeshi la polisi na nje ya polisi, kitabu hiki kinaweza kuwa msaada mkubwa kwao kama watakisoma na kukielewa,” anasema.

ASP Frank ambaye alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Ubungo NHC iliyopo Ubungo Dar es salaam mwaka 1997 alisoma Azania na Umbwe kwa kidato cha nne na tano na kukamilisha elimu hiyo ya sekondari mwaka 2004.

Aidha alipata Shahada yake ya kwanza kwenye BA Sociology (Medical) mwaka 2007 na mwaka 2015 akajiunga na Chuo Kikuu cha Central South cha China kwa ajili ya Shahada ya Pili katika Community Health Nursing au kwa lugha yetu ya Tanzania, afya ya jamii.

Katika masomo haya mtu anajipatia ujuzi wa kutosha wa masuala ya afya ya msingi na uuguzi katika ujamii inayomzunguka. Vile vile katika masuala haya mtu anatambua namna ya utoaji wa huduma ya afya, kudhibiti maradhi yakiwemo ya mlipuko na kutoa elimu ya afya kwa jamii inayomzunguka.

Kazi ya msingi hasa ya ofisa anayeshughulika na afya ya jamii ni kutoa elimu na pia kutoa tiba zinazoagizwa katika jamii na kubwa zaidi kutoa huduma zinaozhitajika za afya ambazo hazipatikani na kuisaidia jamii kutokuwa na maradhi kupitia elimu.

Ni elimu hii ambayo inamfanya askari huyu kuwaangalia askari wenzake na jamii kwa ujumla katika jicho la ziada la kutambua mahitaji yao ya sasa na ya baadaye, hivyo kujikita katika uragibishi ili kupeleka ufahamu kwa watu wengi juu ya suala la kustaafu na masuala mengine ambayo yanachangamoto katika jamii.

Akiwa amezaliwa Oktoba 21, mwaka 1982 mkoa wa Arusha, wilaya ya Arusha (DC), kijiji cha Kioga na kukulia maeneo ya Ubungo NHC, Dar es salaam ambako pia amesomea shule ya msingi, Frank ni mtu wa familia akiwa na mke na watoto wake wawili, Saitoti na Namayani.

Anasema upendo wa mkewe anayetambulika kwa jina la Emmanuela ama mama Saitoti umempa nafasi kubwa katika kukaa kuandika na kusaidia jamii sio tu katika mihadhara, kuandika makala na mada mbalimbali lakini kutulia na kuandika vitabu kwa ajili ya kuongeza maarifa kwa jamii.

“Unajua maarifa katika vitabu hayachuji yanampa mtu ari ya kujua zaidi, nimeandika baada ya kuona ipo haja, hatuna vitabu vya kutosha kusaidia jamii yetu kupata maarifa,” anasema.

ASP Frank anasema mengi ya mambo anayofanya sasa ni matokeo ya mafunzo na malezi ya wazazi wake Lotti Ngarabali na mama yake Christina Mollel.

Anasema enzi ya ujana wake baba yake alifanyakazi ya jeshi, kikosi cha maji na kustaafu kwa hiari kazi hiyo mwaka 1978 na kuajiriwa katika mashirika ya umma mpaka alipostaafu kwa mujibu wa sheria.

Akiwa na baba mwenye msingi wa kiaskari na mama mfanyakazi katika shule za Grace Schools alikuwa katika malezi ya kuchukia uonevu na kuongeza morali kwa wahitaji.

“Kiukweli sikuwahi kufikiria kuwa askari polisi wala sijawahi kuwa na character (tabia) za kuwa askari lakini baada ya kumaliza chuo kikuu niliwahi kukutana na changamoto moja ambayo ilinilazimu kufika kituo cha polisi kupata huduma, kitendo cha kwenda polisi kituoni na namna nilivopata huduma nilianza kuwiwa kujiunga na polisi,” anasema ASP Frank katika mahojiano kuhusu maisha yake na kitabu chake.

Anasema mwaka 2010 wakati jeshi linafanya maboresho walitangaza nafasi za wataalamu wasomi na yeye aliomba pia Jeshi la Magereza, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Watu wa Polisi waliwahi kutoa majibu na akatakiwa kuhudhuria mafunzo CCP lakini pia alipata majibu yaliyomtaka ajiunge na JWTZ lakini wakati majibu yanatoka yeye tayari alikuwa CCP akifunzwa uaskari polisi.

Pamoja na tukio lililomfanya kujiunga na jeshi la polisi lakini anasema yeye tangu akiwa mdogo alikuwa anachukia sana hali za uonevu. Alikuwa hapendi na mpaka leo hapendi kuona watu wakionewa, yaani mtu mmoja akimuonea mwingine, iwe kimamlaka au kikawaida.

Akizungumzia Jeshi la Polisi analotumikia sasa akiwa kama mkufunzi katika chuo chake cha taaluma na pia akishiriki katika kuwatia msasa wastaafu anasema jeshi hilo sasa limekuwa imara sana.

“Shukrani nyingi sana zimwendee Afande Mwema kwa maboresho ndani ya jeshi la polisi, halikadhalika IGP wa sasa Simon Sirro ambaye amekua msaada mkubwa sana katika kulipeleka Jeshi letu mbele zaidi, amekua imara na ameweza kutambua uwezo binafsi wa askari mmoja mmoja,” anasema.

ASP Frank alianza kazi ya polisi, Makao Makuu ya Polisi, kitengo cha polisi jamii, kisha kitengo cha kuzuia uhalifu, baada ya kwenda kozi ya nyota moja alipangiwa kuwa mkufunzi katika chuo cha Polisi Kurasini.

Uhadhiri umempa muda wa kusoma zaidi na kutambua shida zinazowakabili askari polisi katika kazi zao na pia maisha baada ya kustaafu.

Anasema kutokana na mazingira anayofanyia kazi na tafiti kadhaa alizofanya zimemfanya aandike vitabu kadha ikiwamo cha magonjwa mbalimbali yanayotokana na kazi ya polisi, kinachoitwa Kwa nini Ujiuwe? kingine kinafundisha mtoto kujilinda dhidi ya unyanyasaji na ukatili nyumbani na shuleni na hiki cha sasa cha namna bora ya kujiandaa kustaafu kwa askari polisi.

Kazi ya polisi ina shinikizo sana (stress) na ndio maana aliamua kuhakikisha kwamba kuna kitabu kumsaidia kila askari kuhusiana na kazi yake na namna ya kujitunza ili amalize kazi salama na kwa ufanisi mkubwa bila kudhuru maisha yake wala akili yake.

Kitabu kingine ambacho sasa anakiandaa ni kitabu cha namna ya kwenda na kufanya biashara nchini China. Kitabu hicho amekiandika kwa kuangalia uzoefu wa maisha yake nchini humo wakati akisoma.

Kwa nini anapenda kuandika? ASP Frank anasema ukiachia kazi yake ya kufundisha, anapenda zaidi kuandika mambo yanayohusu jamii na hasa changamoto zake ili kuisaidia kujitambua na kukabiliana na changamoto hizo.

“Hii ni hobby yangu, kuandika vitabu na mada mbalimbali nisipoandika nadhani nitaumwa. Kuna mambo mengi ya kusimulia na kufundisha jamii, yanawezekana katika kuandika ili kila mtu atafute maarifa katika kitabu,” anasema.

Anasema vitabu anavyoandika vinachukua muda mrefu kwa kuwa anafanya uchunguzi kifani ambao humlazimisha kukutana na baadhi ya watu wanaotakiwa kuwa funzo kwa wengine.

Mathalani kwenye kitabu cha kujiandaa kustaafu amezungumza na wastaafu na pia wanaoelekea kustaafu na viongozi wa jeshi, waliompa maneno yanayostahili kuzingatiwa na askari kujiandaa na pia maisha baada ya kustaafu.

Humo ndani ya kitabu ana mfano mwema wa mstaafu Kamisha Msaidizi wa Polisi (ACP) Abigael Kauga mwenye umri zaidi ya miaka 75 anayezungumzia uzoefu wake wa maisha ya kipolisi na sababu ambazo anaona zinachangia ustaafu mbaya kwa askari.

“Huwa nafanya uchunguzi wa kina ndio maana unaona kitabu hiui kilichukua mwaka mzima kukifanyia kazi. Kuna mambo mengi na mengine unayapima kwa kulingana na uzoefu, ” anasema.

Kwake yeye anahimiza maisha nje ya polisi ili kujindaa kwa kustaafu na hili ukisoma kitabu hiki anakujuza pia mipaka yake askari ndani na nje ya shughuli zake.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/ba3f40b2327044d9e170f6ca99031278.png

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Rahel Pallangyo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi